KIUNGO wa klabu ya Arsenal na timu ya Taifa ya Nigeria, Alex Iwobi, juzi alikimbizwa hospitali baada ya kula chakula chenye sumu.
Mchezaji huyo alikula chakula hicho akiwa na kikosi cha timu ya Taifa ya Nigeria ambacho kinajiandaa na mchezo wao wa kesho dhidi ya Misri katika michuano ya kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika.
Kocha mpya wa timu hiyo ya Taifa, Samson Siasia, amethibitisha mchezaji huyo kula chakula chenye sumu.
“Ni kweli Alex Iwobi amekula chakula chenye sumu akiwa na kikosi cha timu ya Taifa, lakini kwa sasa anaendelea vizuri baada ya kupewa matibabu. Kutokana na hali hiyo hajaweza kufanya mazoezi ya pamoja na timu,” alisema Siasia.
Hata hivyo, kupitia akaunti yake ya Twitter, mchezaji huyo alieleza kwamba anaendelea vizuri na anaweza kujiunga na timu muda wowote.
“Namshukuru Mungu ninaendelea vizuri kwa sasa kutokana na matibabu niliyoyapata, napenda kuwashukuru wote ambao walikuwa wakiniombea baada ya kusikia nimepata matatizo hayo,” aliandika Iwobi.
Mchezaji huyo alikuwa anawaniwa na timu ya Taifa ya England kutokana na kukitumikia kikosi cha vijana chini ya umri wa miaka 16, 17, 19, lakini Iwobi ameamua kuitumikia Nigeria ambako alizaliwa.
Iwobi amekuwa na mchango mkubwa katika kikosi cha Arsenal na alifanikiwa kufunga bao moja katika ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Everton mwishoni mwa wiki iliyopita.