31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

AKAMATWA NA MAGWANDA YA MAGEREZA

Na Agatha Chales – Dar es Salaam

JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, limemkamata askari ‘feki’ wa Jeshi la Magereza, B. 6034 CPL. Elia @SGT. Frank (28) akiwa amevaa sare za jeshi hilo.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Simon Sirro, aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa mtuhumiwa huyo ambaye alimtaja kama Elias Msigwa aliyekuwa akiwababaisha wananchi wa maeneo ya Kivule anakoishi, alifukuzwa kazi tangu Desemba mwaka jana.

Alisema wakati mtuhumiwa huyo anafukuzwa ndani ya jeshi hilo, alikuwa na cheo cha Koplo, lakini alipokamatwa alikuwa amevaa cheo cha Sajenti na alikiri kuwa alifanya hivyo kutokana na kukosa nauli ya daladala.

Kamishna Sirro alisema jadala lake litapelekwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa hatua zaidi ingawa alimtaka kuomba radhi jamii.

Akizungumza mbele ya waandishi wa habari kwa nia ya kuomba radhi, Msingwa ambaye alikuwa akifanya kazi katika gereza la Keko, alisema: “Bahati mbaya siku ya jana (juzi) sikuwa na nauli ya kwenda mjini ndio nikavaa hizi ‘uniform’ (sare). Nilikuwa nawaomba vijana wenzangu hata kama umeacha kazi, umefukuzwa au chochote, msivae ‘uniform’ na baada ya kutoka hapa nazirudisha hizi uniform katika kituo changu kilichokuwa cha kazi,” alisema Msingwa.

Kamishna Sirro pia alisema jeshi hilo lilikamata watu watatu wanaodaiwa kuwa ni majambazi katika maeneo ya Kivule, Ukonga wakijihusisha na wizi wa kutumia silaha aina ya mapanga, kuvuta bangi na kunywa gongo.

Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Justine Masiko (28) maarufu kama Yassin Masiko, Alex Sirari (33) na George Jiabe (47) ambao walidaiwa kukutwa usiku katika kikao cha kufanya uhalifu.

Katika tukio jingine, Kamishna Sirro alisema Kikosi cha Kupambana na Wizi wa Magari kimefanikiwa kulipata gari aina ya IST lenye namba T 396 CTH lililoibwa maeneo ya Tuangoma na kutelekezwa Kimara baada ya kukimbizwa na polisi.

Pia Kamishna Sirro alisema katika kipindi cha siku mbili, jeshi hilo kupitia Kikosi cha Usalama Barabarani, Dar es Salaam lilifanikiwa kukusanya jumla ya Sh mil. 218,463,500 kutokana na tozo mbalimbali za makosa barabarani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles