Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete ameanza kujivua lawama kuhusu mchakato wa urais baada ya kusema mwanachama yeyote wa chama hicho anayetoka kwa sasa anafanya hivyo kwa hiari na mapenzi yake.
Ametoa kauli hiyo huku kukiwa na wimbi la makada wa CCM wakihama chama hicho kwa madai ya kutoridhishwa na mchakato wa kumpata mgombea urais
Kikwete amesema uamuzi huo ulifanyika kwa mujibu wa Katiba ya CCM na zilipigwa kura ndani ya Halmashauri Kuu ya Taifa baada ya mjadala mrefu ambako uamuzi ulifikiwa kwa pamoja.
Aliyasema hayo Dar es Salaam juzi alipozungumza na wajumbe wa Baraza Ku la Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM).
Rais alisema hakuna haki iliyovunjwa katika mchakato wa kutafuta mgombea urais wa CCM kwa sababu taratibu za chama hicho zinajulikana ingawa baadhi ya watu walikwisha kuamua kutoka CCM hata kabla ya vikao hivyo kuanza Dodoma.
“Aliyetoka katoka mwenyewe kwa uamuzi wake mwenyewe lakini pale tuliamua wote. Maana pale tulipokubaliana kupiga kura, tulikubaliana kupiga kura kwa majina yale matano, siyo uamuzi wangu pekee yangu bali ulikuwa uamuzi wa sote. Maana tulijadiliana na kukubaliana kwamba kwa mujibu wa Katiba yetu majina ni haya haya, tukapiga na kura yakaisha.
“Hivyo anayetoka, anatoka kwa hiari yake mwenyewe kwa sababu pale Dodoma sote tulikubaliana, tuliamua wote kwa mujibu wa Katiba yetu na kwa kweli wote wanaotaka kutoka CCM wanatoka kwa hiari yao wenyewe na wala siyo kwa sababu ya kunyimwa haki,” alisema Rais Kikwete
Alisema pamoja na hali hiyo mchakato wa kumpata mgombea urais umalizika na sasa kazi iliyobaki ni kusubiri Dk. John Magufuli arudishe fomu kazi ianze.
“Sasa mchakato umekwisha. Aliyepata kapata. Aliyekosa kakosa. Mchakato huo haurudiwi tena ule, hatuwezi kuitisha tena mkutano mkuu. Lililobakia sasa tunasubiri sasa Ndugu Magufuli arudishe fomu na baada ya hapo ni Hiyena Hiyena na mambo yanakwenda, haya ndiyo mapenzi ya Mungu,” alisema.
Katika mchakato huo wa Dodoma, CCM ilimteua Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli kuwa mgombea urais wa chama hicho.