25.4 C
Dar es Salaam
Monday, January 30, 2023

Contact us: [email protected]

AJIUA BAADA YA VIROBA VYAKE KUKAMATWA

Mfanyabiashara aliyejiua

Na RAMADHAN HASSAN-DODOMA

MFANYABIASHARA maarufu wa vinywaji baridi na pombe kali mjini Dodoma, Festor Mselia, amejiua.

Mselia alijiua jana kwa kujipiga risasi tatu kichwani kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kutokana na kushindwa kuelewa apeleke wapi shehena ya pombe kali iliyofungashwa katika paketi za plastiki, maarufu viroba aliyokutwa nayo na Jeshi la Polisi.

Mfanyabiashara huyo alikuwa pia mmiliki wa Kampuni ya Mselia Enterprises ya mjini hapa.

Serikali kupitia kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, ilizuia kuanzia Machi mosi, mwaka huu, matumizi ya pombe za viroba kwa kile alichoeleza kuwa zinadhoofisha vijana nchini, wakiwamo wanafunzi.

Majaliwa alitoa kauli hiyo wakati wa uzinduzi wa Baraza la Taifa la Kudhibiti Dawa za Kulevya.

Aliirudia kauli hiyo hivi karibuni alipozungumza  na maelfu ya wakazi wa mji mdogo wa Mererani, wilayani Simanjiro, akiwa katika siku ya pili ya ziara yake mkoani Manyara.

Akizungumza na MTANZANIA mjini hapa jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa, alisema mfanyabiashara huyo alijiua juzi katika shamba lake lililopo Msalato, nje kidogo ya mji wa Dodoma.

“Tulimkuta akiwa hajitambui baada ya kujipiga risasi tatu mwilini akiwa shambani kwake kule Msalato.

“Kabla ya tukio hili, Machi 3 mwaka huu, tulimwita Mselia kumhoji juu ya kufanya biashara ya pombe za viroba.

“Pamoja na kumhoji, tulikwenda dukani kwake na kukuta katoni 1,269 za viroba na tulimzuia asiendelee kufanya biashara hiyo.

“Kwa hiyo, hizo taarifa kwamba alijiua kwa sababu ya kuzuiwa kuuza pombe hizo za viroba sizijui,” alisema Kamanda Mambosasa.

RAFIKI WA MAREHEMU

Akizungumza na MTANZANIA, rafiki wa marehemu, Jonas Mazengo, alisema Mselia alifika nyumbani kwake saa 3.00 asubuhi juzi.

“Alikuja nyumbani kwangu juzi na alinikuta naoga. Nilipomaliza kuoga, nilionana naye na katika mazungumzo yetu alinieleza jinsi alivyokamatwa na viroba vya pombe na kwamba anadaiwa na mfanyabiashara mwenye asili ya kiasia.

“Wakati tunaongea, ilipigwa simu na alipomaliza kuzungumza aliniambia alikuwa akiongea na RCO (Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa) wa Dodoma aliyekuwa akimtaka aende kituoni wakati huo.

“Lakini, yeye alisema alimwambia RCO kwamba yuko shambani kwake na hivyo asingeweza kwenda kituoni wakati huo na hivyo akamtaka amvumilie hadi saa 9.00 mchana.

“Ilipofika saa 9.00 nilimsindikiza kwenda polisi na tulipofika pale polisi, tulimkuta RCO anakagua gari moja lililokuwa na wahamiaji haramu.

“Baadaye tulikwenda na RPC kwenye stoo kulikokuwa na viroba kisha tukaruhusiwa kuondoka hadi hapo watakapomhitaji.

“Tuliondoka pale polisi na kwenda shambani kwake Msalato na wakati huo aliniambia hawezi kuendesha gari, hivyo akaniomba niendeshe mimi.

“Tulipofika shambani kwake ambako pia kuna mifugo mbalimbali, aliniacha mahali akaniambia anamfuata kijana anayetunza mifugo.

“Nilimsubiri hadi saa 12 jioni bila kurudi wakati yule kijana wa mifugo alikuwa amesharudi.

“Kwa hiyo, nilimwambia yule kijana aende akamfuatilie mzee.

“Baada ya muda mfupi huyo kijana alirudi na kuniambia amemkuta anagalagala chini akiwa ametapakaa damu na bastola ipo pembeni,” alisema Mazengo.

MUUZA DUKA

Naye Leslier Msigwa, muuza duka la marehemu lililopo eneo la Area D, mjini hapa ambako ndiko nyumbani kwa marehemu, alisema tukio hilo lina uhusiano na shehena ya viroba.

“Ijumaa alikamatwa na askari kwa madai ya kuuza viroba katika duka lake lililopo Barabara ya 11, Manispaa ya Dodoma.

“Baadaye alidhaminiwa na rafiki yake aitwaye Chola, lakini aliamriwa kurudi kituo kikuu cha polisi juzi Jumatatu.

“Baada ya kukamatwa na kudhaminiwa, alionekana ni mtu mwenye mawazo mengi sana kwa sababu alikuwa akiniuliza kila mara kuhusiana na suala la viroba linaendeleaje.

“Kibaya zaidi, siku moja tulikuwa tukiangalia taarifa ya habari kwenye televisheni, tukaona habari ya kukamatwa kwa viroba katika eneo la Tegeta, Dar es Salaam, tukio ambalo lilionekana kumtisha pia.

“Hata jana (juzi) saa 7.00 mchana, alifika dukani hapa akiwa ameongozana na magari mawili ya polisi akiwamo Kamanda Mambosasa,” alisema.

MTUNZA SHAMBA

Kwa upande wake, mtunza shamba la marehemu aliyejitambulisha kwa jina la Baraka John, alisema yeye ndiye aliyemuona akiwa amejipiga risasi.

“Nilitumwa na mgeni mmoja nikamtafute, nilimkuta akiwa amelala chini huku akihangaika.

“Nilirudi kwa yule mgeni na kumweleza nilichokikuta, naye akaamua kupiga simu polisi na kuwajulisha viongozi mbalimbali, akiwamo diwani na Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji,” alisema kijana huyo.

OFISA MTENDAJI

Akizungumzia tukio hilo, Ofisa Mtendaji wa Kata ya Msalato, Herman Malindila, alisema alipata taarifa za kifo hicho baada ya kupigiwa simu na mtu mmoja.

MGANGA MKUU

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk. James Kiologwe, alisema walimpokea Mselia juzi saa 2.00  usiku  akiwa mahututi kwa sababu alikuwa akivuja damu nyingi zilizotokana na majeraha ya risasi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,063FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles