Gurian Adolf-Sumbawanga
WATU wanne wamefariki dunia katika matukio tofauti wilayani Nkasi mkoani Rukwa, likiwemo la mwanaume kujinyonga kwa kutumia kamba ya nailoni baada ya kugundua mke wake amemtoroka usiku na kwenda kwa mwanaume mwingine.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Justine Masejo, alisema katika tukio la kwanza lililotokea Novemba 24 saa 6 usiku, mwanaume aliyefahamika kwa jina la Rafael Leonard (49) mkazi wa Kijiji cha Bumanda Kata ya Korongwe wilayani Nkasi, alijinyonga chumbani kwake kwa kutumia kamba ya nailoni.
Alisema kabla ya kujinyonga alikuwa amelala na mkewe alipo shtuka usingizini alikuta mke wake ametoroka na kwenda kwa mwanaume mwingine ndipo alipokasirika na kupatwa na wivu wa kimapenzi na kuamua kujinyonga.
Katika tukio la pili lililotokea Novemba 23 saa 8 mchana, katika Kijiji cha Mwai Kata ya Namanyere, kamanda huyo alisema watu wawili waliofahamika kwa majina ya Japhet Jelazi (25) na Peter Silunde (8) walikufa papo hapo baada ya kupigwa na radi wakiwa wamejikinga mvua chini ya mti.
Alisema Jelazi ambaye alikua akilima shambani na Silunde aliyekuwa akichunga mbuzi baada ya kuona mvua imeanza kunyesha, waliamua kukimbilia chini ya mti ili kujikinga wasilowane na mvua hiyo ndipo radi ilipo wapiga na kufariki dunia papo hapo.
Katika tukio la mwisho lililotokea katika Kitongoji cha Milundikwa Kijiji cha Nkundi, Kamanda Masejo alisema mtoto Emiliana Kauzeni (3) alikufa maji baada ya kutumbukia kwenye dimbwi la maji yaliyokuwa yametuama nyuma ya nyumba yao kufuatia mvua zinazo endelea kunyesha mkoani humo.
Alisema mtoto huyo alikuwa akicheza peke yake alizunguka nyuma ya nyumba, alikwenda kwenye dimbwi la maji na kisha kutumbukia, na kufariki huku mama yake akiwa amelala ndani akijipumzisha kutokana na uchovu wa shughuli za kilimo.
Kamanda huyo alisema hakuna watu wanaoshikiliwa kufuatia matukio hayo bali aliwaasa wakazi wa mkoa huo kuwa waangalifu katika kipindi hiki cha mvua za masika ili kujiepusha na madhara yanayoweza kujitokeza.