30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Ajenda zitakazosukumwa na Tanzania mkutano wa SADC

NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM

MACHO na masikio ya dunia hivi sasa yameelekezwa Tanzania ambapo kunatarajia kufanyika mkutano wa 39 wa wakuu wa nchi wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) mwezi ujao.

Katika mkutano wa mwaka huu, Tanzania itapokea kijiti cha uenyekiti wa SADC kutoka kwa Namibia ambapo Rais Dk. John Magufuli, atakabidhiwa uenyekiti wa jumuiya kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Uenyekiti katika SADC ni wa mzunguko na kwa mara ya mwisho mkutano huo ulifanyika nchini mwaka 2003 ambapo Rais Mstaafu Benjamin Mkapa alichaguliwa kuwa mwenyekiti.

Maandalizi ya mkutano huo yanaendelea sambamba na shughuli mbalimbali kwa lengo la kuhakikisha unafanyika kwa mafanikio na kukidhi matarajio ya nchi wanachama.

Miongoni mwa maandalizi hayo ni pamoja na kuwajengea uwezo waandishi wa habari ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa weledi katika kuandika na kuripoti habari zinazohusu jumuiya hiyo.

Tanzania licha ya kuwa mwenyeji wa mkutano huo lakini kama nchi ina malengo mahususi ambayo yatawasilishwa katika mkutano huo na kwa kiasi kikubwa mengine yanashabihiana kwa karibu na ajenda za jumuiya hiyo.

KISWAHILI

Lugha ya Kiswahili ni mojawapo ya ajenda inayotarajiwa kuwasilishwa katika mkutano huo ili kitambuliwe rasmi katika jumuiya hiyo.

Kwa sasa lugha zinazotumika katika jumuiya hiyo ni Kingereza, Kifarasa na Kireno hivyo, iwapo Kiswahili kitakubaliwa kutakuwa na lugha nne.

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Dk. Faraji Mnyepe, anasema kumekuwa na kampeni ya kukifanya Kiswahili kiwe lugha rasmi katika jumuiya hiyo ndiyo maana hata Rais Magufuli alipokwenda nchi kadhaa aligawa vitabu vya Kiswahili.

“Suala la ukombozi wa nchi na uchumi maeneo hayo yameshakaa vizuri ndiyo maana Serikali inafikiria kusukuma ajenda ya Kiswahili.

“Kuna mambo mengi yanafanyika kwa kushirikiana na Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) kuhakikisha Kiswahili kinazungumzwa,” anasema Dk. Mnyepe.

Tayari nchi kadhaa kama vile Malawi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Afrika Kusini, Msumbiji, Namibia na Zimbabwe pia zimeanza kuzungumza Kiswahili.

VIWANDA

Mtazamo wa jumuiya hiyo unafanana na ajenda ya Serikali ya kujenga uchumi wa viwanda yenye lengo la kuiwezesha nchi kufikia kiwango cha uchumi wa kati.

Serikali imejikita kujenga uchumi wa viwanda utakaochochea ajira na ustawi endelevu wa jamii.

Katika kipindi ambacho Tanzania itakuwa mwenyekiti wa jumuiya hiyo inatarajiwa kuchochea mkakati wa viwanda wa SADC kwa kuweka mazingira yatakayowezesha kuongeza thamani katika kilimo, madini na bidhaa za madawa.

Katibu Mkuu Mstaafu Ofisi ya Waziri Mkuu, Mussa Uledi, anasema inapozungumzia SADC na uanachama wa Tanzania lazima tuangalie kwa muktadha wa masilahi ya biashara na kiuchumi.

“Tanzania inachukua uenyekiti wakati ambapo ajenda za jumuiya hiyo zinaakisi ajenda ya Tanzania hivyo, kinachotakiwa ni kuweka utekelezaji wa mipango.

Waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari wakiwa kwenye mafunzo ya kuwajengea uwezo waweze kutekeleza majukumu yao kwa weledi wakati wa mkutano wa SADC.

“Nchi wanachama wa SADC wana mategemeo makubwa na uenyekiti wa Tanzania, kwamba Tanzania itasukuma ajenda ya maendeleo hivyo, dhamana kubwa ambayo Tanzania tunayo ni kukidhi matarajio hayo ya nchi wanachama kwa sababu baada ya uenyekiti wa mwaka mmoja wanatarajia waone hiki na hiki kimetekelezwa,” anasema Uledi.

ULINZI NA USALAMA

Miongoni mwa masuala yanayoiletea heshima kubwa Tanzania ni suala la ulinzi na utetezi wa amani na usalama kwenye ukanda wa SADC na sehemu mbalimbali duniani.

Nchi wanachama wa SADC wamekuwa na imani kubwa na Tanzania katika kutatua migogoro na kusimamia amani katika kanda hiyo na kwa mara tatu mfululizo Tanzania iliteuliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Asasi ya SADC ya Siasa, Ulinzi na Usalama.

Hivyo katika kipindi ambacho itakuwa mwenyekiti wa SADC Tanzania inatarajiwa kuendelea kushiriki katika juhudi za kulinda amani na kuhakikisha kuwa dunia inakuwa sehemu nzuri na salama ya kuishi.

Mkuu wa Operesheni na Mafunzo Brigedi ya Magharibi Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Kanali Wilbert Ibuge, anasema thamani ya maisha ya wananchi katika jumuiya hiyo inazidi kukua kutokana na kuwapo kwa uhuru, ulinzi na usalama.

“Tunazo mbinu nyingi za kutatua matatizo yetu kikanda na kinchi pia, kwanza tunaheshimiana na ukiona nchi zimefikia hapa kuna kuaminiana kukubwa. SADC imefikia hapa kwa sababu watu wanaaminiana,” anasema Kanali Ibuge.

MIUNDOMBINU

Miundombinu ni mojawapo ya sekta zinazopewa kipaumbele katika SADC na Tanzania kama mwenyekiti mtarajiwa wa jumuiya hiyo inayo miradi inayoendelea kutekelezwa katika maeneo mbalimbali.

Hivi sasa Tanzania inatekeleza miradi ya kimkakati kama vile ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR), barabara na Mradi wa kuzalisha Umeme megawati 2,100 kwa kutumia maporomoko ya maji katika Mto Rufiji (Stiegler’s Gorge).

Reli inayojengwa (Standard Gauge), yenye upana wa mita 1,435 ndio mfumo unaotumika sasa ukikadiriwa kuchukua asilimia 50 ya mitandao ya reli duniani.

Nchi nyingi zilizoendelea duniani zinatumia reli kuchochea ukuaji uchumi na biashara kwa sababu usafirishaji kwa kutumia njia hiyo una uwezo wa kubeba mizigo mikubwa kwa mara moja na kwa gharama nafuu kulinganisha na aina nyingine za usafirishaji.

Wabobezi katika masuala ya SADC wanatolea mfano wa miradi ya nishati kwamba kukiwa na umeme mwingi unaweza pia kusafirishwa katika nchi wanachama wa jumuiya hiyo.

Katika bajeti ya 2019/2020 Serikali imetenga Sh trilioni 12.25 na kato ya fedha hizo Sh trilioni 2.48 ni kwa ajili ya mradi wa SGR, Sh trilioni 1.44 kwa ajili ya mradi wa kufua umeme katika Mto Rufiji, Sh bilioni 788.8 ni kwa ajili ya mifuko ya reli, maji na Wakala wa Nishati Vijijini (REA).

MATUKIO MENGINE

Zaidi ya wageni 1,000 wanatarajiwa kuhudhuria mkutano huo ambao wataanza kuwasili nchini kuanzia Agosti 4.

Kutakuwa na shughuli mbalimbali kabla ya Agosti 17 ambayo Rais Dk. Magufuli atakabidhiwa rasmi uenyekiti ambapo mamlaka mbalimbali za serikali zinaendelea kukutana na makundi ya wadau kuwafahamisha fursa zitakazokuwepo na kuwahimiza kujiandaa vizuri.

Matukio mengine yatakayofanyika kuelekea katika mkutano huo ni kufunguliwa kwa jukwaa la kibiashara (SADC Business Forum), Wiki ya Viwanda inayoratibiwa na Wizara ya Viwanda na Biashara na mjadala utakaofanyika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ambao utaongozwa na Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT), Dk. Kaanaeli Kaale, anavishauri vyombo vya habari kutoa kipaumbele kuandika habari za SADC kwa kipindi cha mwaka mzima ambacho Rais Magufuli atakuwa mwenyekiti.

“SADC bado haifahamiki kwa idadi kubwa ya Watanzania hivyo, jitihada kubwa zinatakiwa kujenga uelewa. Tuandike kwa usahihi na ufasaha na tusiishie kuandika kuhusu Tanzania tu bali na nchi zingine,” anasema Dk. Kaale.

Kwa upande wake Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk. Hassan Abbas, anasema kuna mambo mengi kuhusu jumuiya hiyo ambayo Watanzania wengi hawayafahamu hivyo ni nafasi ya vyombo vya habari kuwafahamisha.


“Mkutano huu ni mkubwa sana, mara ya mwisho ulifanyika nchini mwaka 2003 na sasa tumepata tena fursa hii, hili ni tukio letu tulibebe wote.

“Hoja siyo tu Tanzania inakwenda kuwa mwenyeji lakini kuna mambo mengi yanachanganya na kukanganya, tuwasaidie Watanzania kuelewa mengi kuhusu SADC,” anasema Dk. Abbas.

Dhamana kubwa iliyonayo Tanzania katika mkutano huo ni kukidhi matarajio ya nchi wanachama wa jumuiya hiyo katika utekelezaji wa miradi na programu za maendeleo kwa kipindi ambacho itakuwa mwenyekiti.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles