23.8 C
Dar es Salaam
Friday, September 22, 2023

Contact us: [email protected]

Ajali zaongoza kusababisha magonjwa ya ubongo, uti wa mgongo

Aveline Kitomary -Dar es salaam

IDADI ya wagonjwa wanaosumbuliwa na tatizo la kichwa na ubongo, imetajwa kuongezeka huku sababu kubwa ikiwa ni ajali za barabarani.

Akizungumza na MTANZANIA katika mahojiano maalumu,  Daktari Bingwa wa Ubongo, Uti wa Mgongo na Mishipa ya Fahamu katika Taasisi ya Mifupa (Moi), Profesa Joseph Kahamba, alisema hali ya mtindo wa maisha pia inachangia tatizo hilo.

 “Matatizo ya kichwa na ubongo yamegawanyika katika sehemu tatu, moja ni uvimbe kichwani (brain Tumour),  ya pili ni maambukizi kwenye ubongo mfano jipu, TB ya ubongo, minyoo na bakteria, na ya tatu ni damu kuvuja kichwani, hii huambatana na mtu kuumia kichwani, mishipa kupasuka na presha ya kupanda.

“Dalili nyingine ni kuumwa kichwa. Kuna watu wanaumwa na kichwa mara kwa mara, hata akitumia dawa kichwa kinauma tu, ingawa si kila anayeumwa kichwa ana tatizo la ubongo.

“Pia kuna maji kujaa kichwani, mara nyingi kwa watoto kichwa kikijaa maji kinaongezeka na kuwa kikubwa kwa sababu mifupa ya fuvu la kichwa ni milaini bado, lakini kwa watu wazima kichwa kikijaa maji mabadiliko hayatokei ila ukipima maji yanaonekana yamejaa kichwani.

 “Pamoja na sababu zote hizo, ajali ndio zinashika nafasi ya kwanza katika kusababisha matatizo ya kichwa na uti wa mgongo, na sababu zinazofuatia ikiwa ni mfumo wa maisha kama vile kula vyakula vyenye wanga mwingi, mafuta na kutokufanya mazoezi,” alisema Profesa Kahamba.

Alisema katika kliniki yake kwa wiki anaonana na wagonjwa wasiopungua 120 hadi 200 huku idadi ya madaktari wa ugonjwa huo wakiwa wachache.

“Kwa siku moja kwenye kliniki yangu nawaona wagonjwa 40 hadi 60, hapa bado kuna madaktari wengine wa hapa Moi na mikoani nao wanaona wagonjwa, hivyo inawezekana idadi ya wagonjwa ikawa ni kubwa zaidi kuliko hii niliyoitaja.

“Changamoto iliyopo licha ya wingi wa wagonjwa, madaktari ni wachache. Kwa nchi nzima wako madaktari 15, kwa hapa Moi kuna madaktari tisa, Mloganzila wawili, Lugalo mmoja, Aga Khan mmoja, Arusha Seliani mmoja, na Mwanza Uhuru hospitali ni mmoja,” alieleza Profesa Kahamba.

Aidha alisema changamoto nyingine ni wagonjwa wengi kuchelewa kufika hospitali pindi wanapopata maumivu ya kichwa na watu kutokuwa na utamaduni wa kupima afya zao mara kwa mara.

“Watu wanapoumwa kichwa wasichukulie kiurahisi, kichwa kinaweza kikawa na sababu kubwa kuliko wanavyofikiria, ukienda hospitali ukatibiwa labda malaria na kinaendelea kuuma ni bora ukaenda kupata vipimo vya juu zaidi ili upate matibabu sahihi,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,690FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles