25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Ajali za mabasi ya mwendokasi zamshtua Waziri Mkuu

majaliwa* Amuibua Mwaibula, ampeleka DART kuongeza ubunifu

Na Jonas Mushi, Dar es Salaam

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, ameshtushwa na ajali zinazotokea katika barabara ya mabasi ya mwendokasi na kumwagiza Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Naibu Kamishna Mohamed Mpinga, kuwakamata watu wanaotumia barabara ya UDART kinyume na taratibu.

Hayo aliyasema jana wakati akizungumza na waandishi wa habari katika kituo cha UDART cha Kimara Mwisho mara baada ya kumaliza ziara yake ya kushtukiza ambayo pamoja na mambo mengine ililenga kuangalia matumizi ya njia za mabasi na pia kuona kama abiria wanaelewa vizuri namna ya kuitumia huduma hiyo.

Tangu kuanza kwa mradi huo Mei 10 mwaka huu tayari ajali kadhaa zimetokea ikiwemo ile ya Mei 19 ambapo basi la mwendokasi liligongana na pikipiki katika makutano ya barabara ya Morogoro na Shehkilango na kusababisha kifo cha mtoto Nasra Mkinze  mwanafunzi wa Darasa la Pili.

Katika kukabiliana na changamoto kama hizo, Waziri Mkuu alisema wamejipanga kuweka taa maalumu (special sensor) katika makutano ya barabara ili kusimamisha magari kupisha mabasi ya mwendokasi yanapokaribia.

“Tunafikiria kuweka ‘sensor’ maalumu za kuhisi pale basi la mwendo kasi linapokaribia ili ziwashe taa za kisimamisha magari mengine ili kuepusha ajali,” alisema Majaliwa.

Akieleza namna ya kukabiliana na matumizi mabaya ya barabara hizo Kamanda Mpinga ambaye naye alikuwa katika ziara hiyo alisema wamejipanga kuhakikisha chombo chochote cha usafiri kitakachopita kwenye njia ya mabasi hayo kinakamatwa na kuchukuliwa hatua.

“Tumeshajipanga kuanzia sasa gari yeyote hata iwe ya serikali au taasisi ya umma haitaruhusiwa kupita kwenye njia za mwendokasi,” alisema Mpinga na kuongeza:

“Pia bodaboda, bajaji na maguta yote yatadhibitiwa na wenzetu wa DART wana mpango wa kuweka fensi sehemu ambazo si za kuvukia ili wananchi wapite kwenye vivuko rasmi.”

Katika Ziara hiyo pia Waziri Mkuu alimuibua aliyekuwa Mwenyekiti wa Mamlaka ya Leseni za Usafirishaji Dar es Salaam(DTLA), David Mwaibula baada ya kusema watamtumia kama mshauri katika uboreshaji wa usafiri wa mabasi ya mwendokasi (UDART).

Majaliwa ambaye aliongozana na Mwaibula katika ziara yake hiyo alisema; “Nimeamua kuongozana na Mzee wetu Mwaibula kama mnavyofahamu alikua msimamizi mzuri wa mambo ya usafiri wa daladala hivyo tumekuja kujifunza changamoto zilizopo ili tukakae pamoja na aweze kutushauri wapi pa kuboresha ili usafiri uwe mzuri,”alisema Majaliwa.

MWAIBULA NI NANI

Akiwa katika nafasi yake ya Uenyekiti wa DTLA Mwaibula alijizolea umaarufu jijini Dar es Salaam kutokana na kusimamia vizuri utaratibu wa daladala huku akija na ubunifu wa kuboresha huduma hiyo.

Huyu ndiye aliyeanzisha utaratibu wa kuweka ufito wa rangi pamoja na maandishi kwenye daladala kuonyesha njia ya daladala husika katika jiji la Dar es Salaam.

Pia ndiye aliyeasisi utaratibu wa madereva na makondakta kuvaa sare huku akihimiza wamiliki wa daladala kuwapeleka madereva wao Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kabla ya kupata leseni.

Mara kwa mara alionekana barabarani akikagua daladala na mambo kama kukatisha njia, magari chakavu na uchafu wa makondakta yalipungua.

Kutokana kuboresha sekta hiyo ya usafiri jijini Dar es Salaam alipoondolewa mwaka 2007 watu wengi walilalamikia suala hilo.

Akizungumza baada ya Waziri Mkuu kumpa nafasi Mwaibula alisema anafurahishwa na serikali ya ‘Hapa Kazi Tu’ na kuahidi kuiunga mkono katika kuwaletea wananchi usafiri ulio bora.

“Hii serikali ya hapa kazi tu imeonyesha kuguswa na tatizo la usafiri kwa wananchi na naomba wananchi waiunge mkono na mimi nitaungana nayo kuhakikisha tunakuwa na usafiri bora,” alisema Mwaibula.

WAZIRI MKUU APANDA BASI LA UDART

Katika ziara hiyo waziri mkuu alitumia basi la mwendokasi akitokea Kivukoni hadi Kimara ambapo alitumia dakika 55  na kwa mujibu wa taarifa za UDART inatakiwa kutumia dakika 45.

Waziri Mkuu ambaye alilipa nauli kama abiria wengine, alipanda basi namba 23 lenye usajili namba T125 DGW  saa 3:30 asubuhi na lilianza safari saa 3:33 baada ya kusubiri wengine wapande. Kwa wastani ililtumia kati ya dakika mbili hadi tatu kutoka kituo kimoja hadi kingine na basi hilo liliwasili Kimara Mwisho saa 4:28 asubuhi.

Akielezea baadhi ya changamoto alizozibaini alisema wametumia muda mrefu kutoka Kivukoni hadi Kimara kutokana na baadhi ya makutano ya barabara kutokuwa na taa za kuongoza magari.

Alibainisha changamoto nyingine ni ukataji tiketi kwenda taratibu kutokana na kutumia mtandao wa simu na vyombo vingine vya usafiri kutumia njia ya mabasi ya mwendokasi.

Alibainisha maeneo yasiyo na taa kuwa ni makutano ya barabara ya Morogoro na Samora, Morogoro na Jamhuri na Morogoro na Libya.

Aidha alisema wataharakisha matumizi ya kadi pamoja na kuunganisha vituo vya ukataji tiketi na mkongo wa taifa wa mawasiliano.

WATUMISHI WA UMMA KUTUMIA UDART

Waziri Mkuu alisema baada ya kumaliza changamoto zilizopo ikiwemo kuongeza mabasi kutoka 140 ya sasa hadi 305 yanayotakiwa, yatatoa msukumo hata kwa watumishi wa umma kuacha magari yao nje ya mji na kutumia mabasi ya UDART.

Waziri Mkuu pia alitoa onyo kali kwa watu wanaolala kwenye madaraja ya kuvukia yaliyopo katika barabara hizo na kulitaka jeshi la polisi kuwakamata kwani wanatishia usalama wa watu wanaovuka hasa nyakati za usiku.

Pia aliwaasa wananchi kutotumia tiketi ambazo zimekwisha tumika na kusema hatua kali zitachukuliwa kwa mtu atakayejaribu kufanya udanganyifu kama huo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles