Ajali ya basi yaua wawili na kujeruhi 20 Shinyanga

0
1023

Damian Masyenene – Shinyanga

WATU wawili wamefariki dunia na wengine 20 kujeruhiwa katika ajali iliyohusisha basi la abiria la Kampuni ya Bright Line (T 437 DFJ) lililokuwa linatoka Mwanza kwenda Dodoma, gari ndogo na bodaboda.

Ajali hiyo ilitokea jana asubuhi eneo la Isela Barabara ya Shinyanga-Tinde mkoani hapa baada ya basi hilo kugongana na gari dogo lenye namba za usajili T 173 ANW, lililokuwa linatoka Tinde kwenda mjini Shinyanga pamoja na bodaboda.

Mwendesha bodaboda aliyefahamika kwa jina moja la Said (25) alifariki hapo hapo baada ya kulaliwa na gari.

Akizungumza na MTANZANIA ofisini kwake jana, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, Dk. Roze Malisa alikiri kupokea majeruhi 20 na maiti mbili.

Dk. Malisa alisema miongoni mwa majeruhi hao ni Maria Said (9) na watoto pacha waliokuwa katika basi ambao walipakiwa ili wakapokewe na bibi yao.

Hata hivyo pacha hao hawajatambulika majina yao na wamelazwa wodi ya watoto huku hali zao zikiwa mbaya.

“Leo (jana) saa 4 asubuhi tulipokea majeruhi 20 wa ajali ya basi na gari ndogo iliyotokea eneo la Isela, majeruhi sita wako wodini wanaendelea na matibabu akiwamo Julius Agustine ambaye hali yake si nzuri, yuko chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) anaendelea na matibabu kwa sababu ameumia mbavu na mapafu yanatoa damu,” alisema Dk. Malisa.

Aliwataja waliofariki dunia katika ajali hiyo kuwa ni Pili Obedi (12) aliyekuwa abiria katika basi la Bright Line na Said (25) mwendesha bodaboda, huku majeruhi 11 wakiwamo wanawake sita na wanaume watano wakitibiwa na kuruhusiwa kuondoka.

“Waliolazwa ambao mpaka sasa wametambulika majina yao ni Eliza Ndalawa (20), Eliza Said na Maria Said (9),” alisema Dk. Malisa.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Shinyanga, Antony Gwandu, tayari magari hayo yamenyanyuliwa na kuondolewa eneo la tukio na abiria wa basi la Bright Line wametafutiwa usafiri mwingine.

Chanzo cha ajali hiyo imedaiwa kuwa ni mwendesha bodaboda kumkwepa mtembea kwa miguu na kujikuta akigongana na gari dogo, huku basi nalo likimkwepa mwendesha bodaboda na kuligomga gari hilo dogo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here