23 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Aisha kuing’ang’ania ODM akiisubiri Jubilee

ISIJI DOMINIC

KABLA ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2017 nchini Kenya, Aisha Jumwa ambaye ni Mbunge wa Malindi, alikuwa mtetezi wa mgombea wa tiketi ya urais kupitia muungano wa upinzani NASA, Raila Odinga, na akitajwa moja wa wanawake shoka ndani ya chama cha ODM.

Aisha alijitengenezea umaarufu kwa namna alivyokuwa akiinadi NASA na mgombea wake hususan kwa kutumia lafudhi ya Kiswahili cha watu wa Pwani.

Lakini ghafla upepo umebadilika na hii ni baada ya tukio la Machi 9 mwaka jana, wakati taifa lilishuhudia Rais Uhuru Kenyatta na Raila wakizika tofauti zao za kisiasa kwa nia ya kuwaunganisha Wakenya.

Mbunge huo wa Malindi akaanza kuonekana kwenye hafla zinazomhusu Naibu Rais, William Ruto na kusisitiza atamuunga mkono kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2022.

Mara nyingi hafla za Naibu Rais anapoenda maeneo mbalimbali nchini Kenya, yamekuwa yakitajwa kuzindua miradi ya Serikali lakini yanageuka ya kisiasa yenye lengo la kujiimarisha kuelekea uchaguzi mkuu ujao.

Kitendo cha Aisha kumuunga mkono hadharani Ruto kulimuingiza matatizoni na chama chake ambacho baada ya kikao cha baraza la ODM, kiliamua kumtimua kwa madai yeye alichaguliwa na ODM lakini anakikashifu huku akimmiminia sifa Naibu Rais. Mbunge huyo wa Malindi amepinga kutimuliwa kwake kwa kwenda mahakamani kuzuia jimbo lake kutangazwa wazi.

Aisha na baadhi ya wanasiasa kutoka chama cha Jubilee wanasisitiza hatua iliyochukuliwa na ODM ni ya uonevu na kushangaa iweje wakubali Raila kufanya kazi na Uhuru na si Aisha kushirikiana na Ruto?

Hata hivyo, ODM wanapinga hoja hiyo ya ushirikiano wakisema anachofanya Aisha ni kumkampenia Naibu Rais wakati yeye bado ni mwanachama wa ODM aliyechaguliwa na wananchi kupitia chama hicho.

Hivi karibuni katika mazishi ya baba mzazi wa Naibu Gavana wa Mombasa, William Kingi, katika kaunti ya Kilifi, Aisha alimkatiza Katibu Mkuu wa ODM, Edwin Sifuna, aliyekuwa jukwani akiongea na waombolezaji na kumnyang’anya kipaza sauti.

Hii ilidhihirisha ni jinsi gani mbunge huyo wa Malindi alivyo na ‘kinyongo’ kutokana na kitendo cha ODM, kumtimua huku akiona kama ni maamuzi binafsi ya Sifuna.

Swali ni je, mahakama ikiridhia uamuzi uliochukuliwa na ODM au hata yeye mwenyewe akakubali kuachana na chama hicho, atarudi tena bungeni? Na atarudi kupitia chama kipi?

Mwakilishi wa wanawake kutoka Homabay, Gladys Wanga, amemshutumu mbunge huyo wa Malindi kwa kuonyesha ODM utovu wa nidhamu na kumtaka ajiuzulu kama anaona anachokifanya ni sahihi.

“Kama yeye anajiamini ni mwanamke aliyekamilika kisiasa, ajiuzulu ubunge wake na kuthibitisha anaweza kutetea kiti chake,”alisema Wanga. 

Alisema kitendo chake cha kuunga mkono nia ya Naibu Rais kugombea urais mwaka 2022 ni kushindwa kuheshimu uongozi wa chama uliochangia kuupata ubunge na njia pekee ni yeye kujiunga na Jubilee.

Kuondoka ODM ni mtihani kwa Aisha kwa sababu atajiunga na chama kipi si tu kwa ajili ya uchaguzi mdogo mbali hata ule wa 2022?

Hata kama atajiunga na Jubilee ambapo anaweza kupata sapoti ya Ruto, anapaswa kutambua kiongozi wa Chama cha Jubilee ni Rais Uhuru anayefanya kazi na Raila ambaye Aisha alishawahi kumshutumu.

Aidha sehemu anayotoka ni ngome ya upinzani na endapo atajiunga na chama tawala atalazimika kufanya kazi ya ziada kuwashawishi wapiga kura waliomchagua.

Aisha anaweza pia kuwania ubunge akiwa mgombea binafsi kutokana na kukubalika na wapigakura wa Malindi lakini atahitajika kuwa makini kwa sababu Jubilee na ODM ni vyama vyenye ushawishi mkubwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles