27.5 C
Dar es Salaam
Sunday, December 3, 2023

Contact us: [email protected]

Aina mpya rushwa vita ya ujangili

Na Bakari Kimwanga

-Dar es Salaam

NAIBU Mkurugenzi wa Kuzuia Ujangili nchini, Robert Mande, amesema kwa sasa wanakabiliana na aina mpya ya rushwa inayowahusisha baadhi ya viongozi wa umma na taasisi binafsi ambao wamekuwa wakifadhili mtandao wa ujangili.

Mande alisema hayo hivi karibuni alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari wa Tanzania na Thailand walioko kwenye programu ya kuandika habari za kupinga ujangili na usafirishaji haramu wa wanyamapori.

Alisema baadhi ya watendaji serikalini na taasisi binafsi huwezeshwa kuratibu ujangili kwa kuharibu ushahidi au kesi za ujangili jambo ambalo husababisha kazi kuwa ngumu.

 “Kitaalamu hii ni aina mpya ya rushwa ambayo inahusisha watendaji na hata baadhi ya watoa maamuzi serikalini, tunaiita ‘White Color Crime’. 

“Unakuta mtu amekaa ofisini, lakini kazi yake ni kupindisha baadhi ya mambo, ikiwamo mikataba kwa kuingiza vipengele ambavyo vitawasaidia majangili.

“Hii ni biashara ambayo ilileta watu wenye uchu wa kutajirika haraka, inaunganisha makosa mengi kama rushwa, utakatishaji wa fedha na ujangili.

“Mtaalamu akijiingiza kwenye rushwa kughushi, inaitwa ‘White Color Crime’. Tumegundua hili ni tatizo kubwa, ushiriki wa wataalamu maeneo mbalimbali ndiyo unasababisha uhalifu kupitia ujangili ambao sasa tunapambana nao ili kuokoa rasilimali zetu za taifa,” alisema Mande.

Alisema ni rahisi kwa mtu mwenye nafasi kushawishiwa kushiriki kwenye uhalifu bila kujulikana kutokana na nafasi yake ya utendaji ndani ya Serikali.

 “Kupambana na mhalifu ambaye humjui na ana nafasi kwenye udhibiti wa sheria ni ngumu sana, kutokana na hali hiyo tunashirikisha vyombo vyote vya ulinzi na usalama katika kikosi chetu ili tuweze kupambana na watu wote kuanzia ngazi ya chini hadi juu,” alisema.

Alisema muungano wa vyombo vya ulinzi na usalama katika kupinga ujangili umeleta mafanikio.

“Ninachopenda kuwaeleza hapa ni kwamba kuanzia mwaka 2016 hadi sasa ujangili wa tembo umeshuka sana, haya ni matunda ya ushirikiano baina ya vyombo vyote vya Serikali na sekta binafsi,” alisema.

Alisema ujangili ulikuwa tishio miaka ya 2000 hadi 2014, ambapo asilimia 60 ya tembo walitoweka na ndipo Serikali ilianzisha mpango wa kitaifa wa kupambana na ujangili.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
579,000SubscribersSubscribe

Latest Articles