27.6 C
Dar es Salaam
Friday, January 3, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Ahueni kwa wakulima wa korosho teknolojia ikizidi kushamiri

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Katika kuhakikisha asilimia 60 ya korosho zote zinazozalishwa nchini zinabanguliwa ifikapo msimu wa mwaka 2025/26, Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania (Tirdo) limefanikisha kufungwa kwa mtambo unaoondoa ganda laini la korosho.

Mtambo huo wenye uwezo wa kuondoa kilo 350 kwa saa umekabidhiwa kwa Kituo cha Zana za Kilimo na Teknolojia Vijijini (Camartec) ili kuendelea kuongeza thamani zao hilo kabla ya kusafirishwa.

Akizungumza leo Machi 29,2024 wakati wa kusaini makubaliano na makabidhiano ya mtambo huo, Mkurugenzi Mkuu wa Tirdo, Profesa Mkumbukwa Mtambo, amesema walipewa jukumu la kuleta mitambo itakayoondoa ganda laini la korosho kukamilisha mnyororo mzima wa ubanguaji korosho.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania (Tirdo), Profesa Mkumbukwa Mtambo (Kulia) na Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Zana za Kilimo na Teknolojia Vijijini (Camartec), Mhandisi Paythias Ntella, wakisaini makubaliano ya kufungwa mtambo unaoondoa ganda laini la korosho.

“Jukumu kubwa la Tirdo ni kufanya utafiti kuangalia teknolojia za nje na ndani kuona namna zinavyoweza kuleta mapinduzi ya kiviwanda, tunaishukuru serikali kwa kuziwezesha taasisi zetu na kuweza kupata mitambo kama hii,” amesema Profesa Mtambo.

Taasisi zingine zilizofanikisha kufungwa kwa mtambo huo ni Shirika la Uhandisi na Usanifu Mitambo Tanzania (Temdo) na Shirika la Viwanda Vidogo Vidogo (Sido).

Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Zana za Kilimo na Teknolojia Vijijini (Camartec), Mhandisi Paythias Ntella, akizungumza na waandishi wa habari baada ya kukabidhiwa mtambo unaoondoa ganda laini la korosho.

Naye Mhandisi Atupele Kilindu kutoka Idara ya Uhandisi Maendeleo Tirdo, amesema mtambo huo uliogharimu Sh milioni 40 una uwezo wa kuondoa ganda laini kilo 350 kwa saa.

Amesema lengo ni kuanzisha kiwanda cha mfano kwa ajili ya kufundisha wajasiriamali namna ya ubanguaji na kuongeza mnyororo wa thamani katika zao la korosho.

Kaimu Mkurugenzi wa Camartec, Paythias Ntella, amesema tayari wana kiwanda darasa cha kubangua korosho kilichoanzishwa na kituo hicho wilayani Manyoni mkoani Singida kwa lengo la kuwasaidia wakulima kubangua korosho na kuacha kuuza zikiwa ghafi na kushindwa kunufaika na kilimo hicho.

“Tulianza Machi na tumeshaanza kuzalisha korosho, tulikuwa tunapata changamoto ikifika hatua ya kumenya, watu wanamenya kwa mkono hivyo kupatikana kwa mtambo huu kutaongeza kasi.

“Tunafundisha wajasiriamali katika hatua zote ili kubangua na kumenya ili vitengenezwe viwanda vingi zaidi sehemu nyingine,” amesema Ntella.

Lengo la Serikali ni kuhakikisha ifikapo mwaka 2030 korosho zote zibanguliwe nchini na kuuzwa zikiwa ghafi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles