Na Veronica Romwald, Dar es Salaam
WIZARA ya Viwanda na Biashara imeanza kupigia chapuo ahadi iliyotolewa na Rais Dk. John Magufuli wakati wa kampeni, kupeleka mgao wa Sh milioni 50 kila kijiji nchini kote.
Wizara hiyo imeshauri fedha hizo zilizoahidiwa na Rais Magufuli zipelekwe kwa wananchi mapema ili wakopeshwe waweze kuanzisha miradi.
Akizungumza Dar es Salaam jana kuhusu maadhimisho ya Siku ya Viwanda Duniani, ambayo yanatarajiwa kufanyika Novemba 20, mwaka huu, Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Uledi Mussa alisema fedha hizo zikitolewa zitasaidia wananchi kuanzisha miradi ya uzalishaji katika maeneo yao.
“Sekta ya viwanda imechaguliwa kuwa sekta kiongozi ya serikali ya awamu ya tano. Kwa muda mrefu tumekuwa tukizungumza juu ya uanzishaji wa viwanda vidogo lakini tumekuwa tukijiuliza kwa nini havikui angalau kufikia kuwa viwanda vya kati.
“Sasa ili sekta hii iwe kiongozi mzuri ni lazima uendeshaji wake uwe shirikishi bila kubagua wafanyabiashara wa chini, kati na juu. “Kwa kuwa Rais Magufuli aliahidi kutoa Sh milioni 50 kila kijiji tumemua kulipigia debe ili zitolewe kwa ajili ya kuwakopesha wananchi waweze kuendeleza na kuanzisha miradi yao,” alisema Mussa.
“Lakini ili tufanikiwe kufikia lengo letu tunahitaji mitaji ya kutosha, ubunifu pamoja na maeneo ya kutosha kwa ajili ya uwekezaji,” alisema.
Mkurugenzi wa Sera na Ushawishi wa Shirikisho la Viwanda katika sekta binafsi nchini (CTI), Hussein Kamote alisema ili kufanikisha lengo hilo ni lazima serikali idhibiti uingizaji holela wa bidhaa kutoka nje ya nchi.
Naye Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo (UNIDO), Victor Akim alisema Bara la Afrika linaweza kuinuka kiuchumi iwapo watatambua fursa zilizopo na kuzifanyia kazi.
Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 iliyofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu kulikuwa na jumla ya vijiji 19, 200. Ili kila kijiji kiweze kunufaika na fedha hizo zinahitajika Sh bilioni 960.