26.8 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 28, 2023

Contact us: [email protected]

Ahadi kupewa ng’ombe mwisho wa mwaka zinavyowatesa watoto Geita

FARAJA MASINDE

RIPOTI ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu ya mwaka 2019 imefichua namna watoto wanaoajiriwa kufanya kazi ya kuchunga mifugo mkoani Geita wakiwamo wale wanaohudumu katika sekta ya madini wanavyoteswa na kunyanyaswa ikiwamo kuchomwa moto sehemu za makalio na waajiri wao.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo inayoitwa Ripoti ya Haki za Binadamu na Biashara Tanzania Bara ya mwaka 2018/19, inasema kuna kundi kubwa la watoto walioajiriwa kuchunga ng’ombe mkoani humo ambao wamekuwa wakipitia mateso makali kutoka kwa waajiri wao.

Inaeleza kuwa waajiri hao wamekuwa wakiwalaghai kwa kuwaahidi kuwa watawapatia makazi na mshahara mnono lakini mara baada ya kukubaliwa matakwa yao hayo wamekuwa wakigeuka na kuwanyonya stahiki zao.

Ofisa Ustawi wa Jamii Wilaya ya Geita, Anderson Shimbi, anafafanua kuwa watoto wengi wamejikuta wakinyanyasika kwa waajiri wao kwa kuwa wamekuwa wakilaghaika kuajirika kwa lengo la kupewa ng’ombe na fedha mwisho wa mwaka ahadi ambazo hata hivyo, imekuwa hazitekelezwi na waajiri wao.

“Watoto hawa kwa kweli wanasikitisha kwani wengi wamekacha masomo kwa kulaghaiwa na matajiri wanaomiliki ng’ombe kwenda kufanyakazi ya kuchunga kwa makubalino ya kulipwa mshahara mnono au kupewa ng’ombe mmoja mwisho wa mwaka, ahadi ambayo sasa imegeuka mateso kwao.

“Pindi inapofikia mwisho wa mwaka kwa ajili ya kutimiziwa ahadi hizo kama walivyokubaliana, waajiri wao wamekuwa wakiibua visingizio kwa kuwabambikizia kesi na makosa mengine mazito ambayo huondoa utimizwaji wa ahadi hiyo jambo ambalo huwafanya watoto wenyewe washindwe kudai kwani hupigwa na kufukuzwa bila kupewa kitu,” anafafanua Shimbi.

Ripoti hiyo imefafanua kuwa utafiti wake ulikwenda mbali zaidi kwa kwenda katika moja ya kesi iliyokuwa inamkabili mtoto, Mabula Samora(14), kutoka Kijiji cha Nyungwa, ambaye alikuwa ameajiriwa kwa ajili ya kuchunga mifugo kwa makubalino ya kulipwa ujira wa Sh 200,00O kwa mwaka. Lakini ilipofika kipindi cha malipo bosi wake huyo alimsingizia kuwa ameiba spika za muziki, sola, betri ya sola na fedha Sh 200,000 mali ya mtoto wake wa miaka 19.

“Lakini kama hiyo haitoshi,  Samora alicharazwa na fimbo kubwa kipigo ambacho ilikuwa kidogo tu kikatishe uhai wake ndipo akalazimika kukimbia kwani tayari walianza kumchoma moto sehemu za makalio yake, hatua ambayo ilifanya yaanze kuoza.

“Baadaye walimchukua na kumpeleka hospitali ambako huko walimtelekeza na kumwacha kabla ya kupata msamaria mwema aliyemchukua na kumpeleka kwenye kituo cha afya kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi zaidi,” inaeleza ripoti hiyo.

Ripoti hiyo inaendela kufafanua kuwa Utafiti umeonyesha malalamiko ya wafanyakazi kufanyishwa kazi kupita saa za kazi zilizokubaliwa kisheria, jambo ambalo linaweza kuashiria pia uwapo wa kufanyakazi kwa shurti hususan kwa watoto.

“Tatizo la ajira za watoto zipo hapa Nyang’wale, kwa sababu wanamchukua kama ‘chiep labour’ na wanakimbilia kuchukua watoto wadogo wanaotakiwa kwenda shule kwa sababu ukimpa mtoto chakula tu atasaidia kuosha mchanga wa dhahabu na mambo mengine,” anasema Shimbi.

Vitendo hivyo vinaenda kinyume na sheria ya mtoto namba 21 ya mwaka 2009 inayokataza utumikishwaji wa watoto katika migodi.

Shimbi anaendelea kubainisha kuwa, “Chanzo cha ajira kwa watoto katika sekta ya uvuvi ni kutokana na matajiri wanaofanya biashara ya samaki jirani na kisiwa cha hifadhi ya Taifa Rubondo ambao huwalipa watoto Sh 3,000 kwa siku huku wengine wakipewa samaki kama malipo. Hivyo, inategemeana na siku yenyewe samaki wamepatikana kwa kiwango gani kwani siku ambayo kunakuwa hakuna samaki basi ni dhahiri kuwa watoto hao huambulia patupu,” anasema Shimbi.

Takwimu za kesi za ajira kwa watoto mkoani Geita hususan sekta ya uvuvi kwa mwaka 2018 /19 inaonyesha kuwa kesi za watoto watano zilirekodiwa kwa kipindi cha mwaka jana huku kipindi cha Januari hadi Julai mwaka huu, kesi zilizorekodiwa ni za watoto wenye umri kati ya miaka 12 na 17.

Wakati hali ikiwa hivyo mkoani Geita, upande wa Shinyanga nako utafiti umebaini kuwapo kwa ajira za watoto katika sekta ya madini husuan katika Kijiji cha Mwakitolyo, jambo ambalo limechangia kwa kiwango kikubwa watoto hao kukacha masomo huku sababu kubwa ya kujiingiza kwenye ajira hizo ikiwa ni umasikini.

“Hii imetokana pia na ugomvi pamoja na utengano wa familia jambo ambalo linasababisha watoto kukosa mwelekeo hatimaye kuangukia kwenye ajira hizo ambazo kwa kiasi kikubwa zimejaa mateso na manyanyaso.

“Watoto wengi waliofanyiwa mahojiano katika mgodi ulioko kwenye Kijiji cha Mwakitolyo, wameeleza kuwa hulipwa Sh 6,000 kwa siku kufanya kazi kwenye mgodi huo ambapo kazi huanza saa 12 alfajiri hadi saa kumi jioni hata hivyo, jambo la kushtua ni kwamba watoto hao hawana vifaa vya kujikinga wakati wa kufanya kazi hizo jambo ambalo linazidi kuhatarisha afya zao,” inafafanua ripoti hiyo.

Kama inavyofahamika kuwa ajira kwa watoto inatakatazwa katika mikataba mbalimbali, ikiwamo Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Mtoto (CRC) uliotimiza miaka 30 mwezi uliopita tangu kuanzishwa kwake 1989 na mkataba wa Afrika wa Haki na Ustawi wa Mtoto wa mwaka 1990.

Lakini pia, kazi za lazima zinakatazwa katika mikataba mbalimbali, ikiwamo Mkataba wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) wa kuondoa kazi za lazima uliopitishwa mwaka 1957.

Aidha, katika ngazi ya taifa, Sheria ya Ajira na Uhusiano Kazini ya mwaka 2004 inakataza ajira kwa watoto na kazi ya lazima. Kwa mujibu wa sheria hii `Mtoto mwenye umri chin’ ya miaka 18  haruhusiwi kuajiriwa kwenye mgodi, kiwanda au kufanya kazi katika sehemu nyingine za kazi ikijumuisha ajira isiyo maalumu na kilimo, kwenye mazingira ya kazi ambayo Waziri anaweza kuona ni hatarishi’ kifungu cha 5(3).

Kwa upande wa ajira kwa watoto na kazi ya lazima, mambo makubwa yaliyoibuliwa ni: Matukio ya ajira kwa watoto yaliripotiwa katika mikoa yote iliyofikiwa, lakini jambo hili liliainishwa kuwa tatizo hasa katika mikoa ya Geita, Dodoma na Arusha.

Kwa upande wa kulazimishwa kufanya kazi, washiriki katika karibia mahala pote pa kazi walisema hilo sio tatizo kwao, japo mtazamo huu unaweza kuwa umechangiwa na uelewa mdogo kuhusu haki za wafanyakazi na viwango vya kazi.

Huu ni wakati sasa kwa Serikali kuangalia kwa karibu aina hizi za ajira ambazo zimeendelea kuwa mwiba kwa watoto, ikiwa ni pamoja na kupiga marufuku ajira hizi ikiwamo kuwawajibisha wanaoajiri watoto ili kuwa na taifa imara hapo baadaye.

Kwanini inasikitisha kuona kuwa waajiri wamekuwa na mamlaka ya kufikia sehemu hata wakadiriki kuchoma watoto moto.

Ni lazima sasa serikali inyooshe mkono wake ili kutokomeza kabisa vitendo hivi kwani inasikitisha kuona kuwa mtu haoni ajabu kumuua mtoto jambo ambalo ni kinyume cha sheria za nchi.

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
579,000SubscribersSubscribe

Latest Articles