Agizo kuondoa vituo vya daladala shuleni litekelezwe

0
1748

FARAJA MASINDE

HIVI majuzi, Jeshi la Polisi kitengo cha usalama barabarani lilitoa takwimu zinazoonesha kuwa wanafunzi 56 wamepoteza maisha katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Septemba mwaka huu, kutokana na ajali za barabarani.

Kwa mujibu wa takwimu hizo, kuanzia Januari hadi Septemba, mwaka 2019, wanafunzi wa kiume 35 na wakike 21 walipoteza maisha kwa ajali za barabarani na hivyo kukatisha ndoto zao za kuwa viongozi wa kesho.

Wanafunzi 58 walijeruhiwa ambapo kati yao wanaume walikuwa 37 na wanawake 21 kwa nchi nzima.

Kutokana na takwimu hizi, Kamanda wa Polisi wa Kikosi cha Usalama Barabarani Taifa, Fortunatus Muslim, aliagiza wakuu wa polisi wilaya (OCD) kote nchini kushirikiana na mamlaka zinazohusika kuhamisha vituo vya daladala vilivyopo katika malango ya kuingia na kutoka shuleni katika maeneo mbalimbali nchini hususana yale ya mijini.

Aidha, Kamanda Muslim alitoa agizo hilo kutokana na malalamiko yaliyotolewa na wananchi kuhusu kuwapo kwa vituo vya daladala katika mageti ya kuingia na kutoka shuleni.

Ikumbukwe kwamba katika vituo hivyo magari husimama na kuziba wanafunzi kuona upande wa pili kama kuna gari wakati wa kuvuka.

Hata hivyo, siyo wanafunzi wote ambao huzingatia tahadhari hiyo hatau ambayo imefanya kuwapo kwa takwimu hizo zenye kuumiza.

Hivyo, ni wajibu kwa mamlaka zinazohusika kuhakikisha zinafranyia kazi changamoto hiyo ambayo kwa kiasi kikubwa hugharimu maisha ya watoto.

Sasa basi, agizo hilo ni muhimu kwa ustawi wa wanafunzi kwa kuwa litawasaidia kuvuka kwa usalama barabarani.

Ni vyema kwa wahusika walioagizwa hili kulitekeleza mapema kwa kuviondoa vituo vyote vilivyopo katika malango ya kuingilia shuleni.

Hii itatoa fursa kwa wanafunzi kuona vyema magari yaliyo upande wa pili na kuwawezesha kuvuka salama barabarani.

Wahusika ni vyema kulichukulia kwa uzito unaostahili suala hili kwa kuviondoa vituo hivyo ili kuepusha kuendelea kugongwa kwa wanafunzi watokapo shuleni.

Aidha, wanafunzi nao wanapaswa kuchukua tahadhari pindi wanapovuka barabara, kuhakikisha hakuna madhara yanayoweza kuwakumba.

Pamoja na utekelezaji wa agizo hilo, jamii wakiwamo madereva na abiria wanapaswa kuchukua tahadhari pindi wanapopita maeneo yenye shule ili kuepuka kuwasababishia ajali wanafunzi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here