31.7 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

AG Z’bar ‘Out’

Aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Othman Masoud Othman
Aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Othman Masoud Othman

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, amefuta uteuzi wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Othman Masoud Othman.

Kutokana na kumfuta kazi mwanasheria huyo, Dk. Shein amemteua aliyekuwa Naibu Mwanasheria wa serikali hiyo, Said Hassan Said kuwa Mwanasheria Mkuu.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana, Rais Shein amefuta uteuzi huo kwa mujibu wa mamlaka aliyo nayo chini ya Kifungu 55(1)cha Katiba ya Zanzibar ya 1984.

Hata hivyo, wachambuzi wa masuala ya kisiasa nchini walibashiri kutimuliwa kwa AG Othman kutokana msimamo wake alionyesha ndani ya Bunge Maalumu la Katiba, baada ya kupinga masuala kadhaa yenye maslahi kwa Zanzibar kutowekwa kwenye Katiba mpya.

“Mhe, Said Hassan Said, anachukua nafasi ya aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar Mhe, Othman Masoud Othman, ambaye uteuzi wake umefutwa kwa mujibu wa vifungu vya 53,54 (1) na 55(3) vya Katiba ya Zanzibar ya 1984 na kifungu 12 (3) cha Sheria ya Utumishi wa Umma Namba 2 ya 201,” ilieleza taarifa hiyo.

Uteuzi huo wa AG Said umeaza jana, ambapo kabla ya uteuzi huo alikuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Oktoba Mosi, mwaka huu aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Othman Masoud Othman, alitibua wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, baada ya kuikataa Rasimu ya Katiba iliyopendekezwa.

Baada ya kupiga kura ya hapana, baadhi ya wajumbe walimzomea mwanasheria huyo wakionyesha kutoridhishwa na msimamo wake.

Kutokana na hali hiyo, baada ya Bunge kuahirishwa saa nne asubuhi, askari wa Bunge walilazimika kumtoa bungeni chini ya ulinzi mkali kwa kutumia mlango anaotumia Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kuingia bungeni.

Kabla walinzi hao hawajamfuata mwanasheria huyo, awali baada ya Bunge kuahirishwa, alikuwa akizungumza na wajumbe mbalimbali huku akionyesha atatoka katika ukumbi wa Bunge kupitia mlango wa kawaida wanaotumia wajumbe wote.

Katika mazungumzo hayo yaliyodumu kwa sekunde kadhaa, askari hao waliongozana naye na kumpitisha katika mlango anaotumia Waziri Mkuu huku baadhi ya wajumbe wakipaza sauti wakisema; “msaliti huyo”, “Ukawa huyo”, “huyo si kamanda anakimbia vita”.

Wakati wa kupiga kura ya Hapana,  Othman aliitaja sura ya saba na kuzikataa ibara za 70 hadi 75 ambazo zinahusu muundo wa Jamhuri ya Muungano, ambapo msingi mkuu wa ibara hizo ni muundo wa Serikali mbili.

Alizikataa pia ibara za 128 na 129 zilizoko katika sura ya 10 ambazo zinaeleza muundo wa madaraka ya Bunge.

Baada ya kuzitaja ibara hizo, aliitaja sura ya 11 na kuzikataa ibara za 158, 159, 160 na ibara ya 161. Sura hiyo inazungumzia Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Baraza la Mapinduzi la Zanzibar na Baraza la Wawakilishi la Zanzibar.

Kutokana na msimamo huo aliyekuwa wa kwanza  kumjadii ni Mbunge wa Chwaka, Yahya Kassim (CCM) ambaye alisema anashangazwa na uamuzi wa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar wa kuikataa rasimu wakati hakushiriki mijadala yake.

“Mheshimiwa Mwenyekiti, wote tulioko humu tumepiga kura kwa sababu tulishiriki kujadili rasimu, lakini huyu Mwanasheria wa Zanzibar amepiga kura wakati hakushiriki mjadala.

“Hakushiriki mjadala si kwa sababu anaumwa bali ni kwa sababu ya kejeli na jeuri yake tu kutuonyesha kwamba amesoma. Sisi tulitegemea awepo hapa tangu mwanzo kwa sababu Rais wa Zanzibar alimteua ili awe msaidizi wake, lakini hamsaidii.

“Hivi mwanasheria kama huyu ana masilahi gani na Wazanzibari, yaani rais amemteua amsaidie halafu yeye anatoroka, hivi unaweza kutwambia nini juu ya mtu kama huyu?” alisema Kassim.

Wakati wa Bunge hilo, Othman alijitoa katika Kamati ya Uandishi ya Bunge hilo kutokana na kile kilichoelezwa kuwa ni baada ya kamati hiyo kuzikataa hoja 17 alizotaka ziwekwe katika Rasimu ya Katiba inayopendekezwa.

Akizungumza na waandishi wa habari kipindi hicho, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar , Balozi Seif Ali Idd, alisema kuwa hoja za Othman ambazo hazikukubaliwa ni nne na zilikuwa zikiendelea kufanyiwa kazi.

Kuhusu kitendo cha kupingana na serikali yake, Balozi Idd alisema Rais wa Zanzibar ndiye mwenye wajibu wa kumuondoa Othman kwa mujibu wa sheria.

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

  1. Inasikitisha Sana kumuona rais wa nchi akiipenda zaidi nchi jirani kuliko nchi take aliyozaliwa na anayoishipamoja na family take yote , hivi haoni nikiiuza nchi na watu wake wote kwa maslahi ya nchi nyengine ! Huyu shein ni bwege la kutupwa na hafai kuongoza hats family take wancha nchi na watu wake !

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles