AG Masaju: Huu si wakati wa mazungumzo

George MasajuNA GABRIEL MUSHI

MWANASHERIA Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju, amesema huu si wakati wa kukaa katika meza ya majadiliano, hivyo viongozi wa dini watumie njia ya maombi kuliombea Taifa lisiingie kwenye uvunjifu wa amani kutokana na Operesheni Ukuta iliyoanzishwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Kauli hiyo ya Masaju imekuja siku chache baada ya Taasisi ya Maridhiano inayoundwa na viongozi mbalimbali wa dini nchini kutaka Serikali na viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kukaa chini kutafuta suluhu ya mvutano unaoendelea kuhusu operesheni ya Umoja wa Kupambana na Udikteta Tanzania (Ukuta), ili kuepusha vurugu zitakazojitokeza nchini wakati maandamano hayo yaliyopangwa kufanyika keshokutwa.

Katibu Mkuu wa taasisi hiyo, Mchungaji Osward Mlay wiki iliyopita alisema ili kuepuka machafuko yanayoweza kutokea wakati wa kutekeleza operesheni hiyo Septemba mosi, mwaka huu huku Jeshi la Polisi lilisema litauvunja Ukuta ni vyema pande zote mbili zikajadiliana na kupata mwafaka.

“Hakuna jambo lililoshindikana mezani. Sisi kama taasisi ya maridhiano, tunaiomba serikali ikae mezani na viongozi wa Chadema ili kumaliza tofauti hizo,” alisema.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Masaju alisema viongozi wa dini wasing’ang’anie majadiliano bali wawashauri waumini makanisani na misikitini kutoshiriki kuvunja amani.

“Viongozi wa dini wanaweza kuendelea kufanya maombi dhidi ya hofu inayokuja na Ukuta, dhidi ya hali ya kutoheshimu sheria, warumi 3: mstari wa 17 -20 inasisitiza umuhimu wa kutii mamlaka. Ina maana hizo mamlaka ni Mungu. Kwa hiyo mtu akiiba anakamatwa na serikali. Si Mungu. Licha ya kuzungumza natoa option (njia) ya pili wanaweza kuangalia kuitii malaka iliyopo. Wasipojadiliana wakiacha kwenye hii nyingine ya maombi nchi ikiingia kwenye uvunjifu wa amani hali itakuwa mbaya.

“Suala la amani na utulivu haikuwekwa kwenye mamlaka mtu mwingine zaidi ya Rais, haya mambo ya siasa yanaweza kusababisha kusiwepo na usalama, kwenda kujadiliana naye maana yake unakwenda kuvunja Katiba na sheria,” alisema.

Alisema hakuna udhibitisho unavyowalazimu viongozi wa dini na wa vyama vya siasa na Serikali kwa sababu polisi wanajua vitendo vya uvunjifu wa amani.

“Nyumbani nina Koran na Biblia, ninatambua umuhimu wa taasisi hizo za kidini, natambua wanasisitiza kufanya majadiliano, ila wawaambie waumini wao kuheshimu mamlaka hiyo ili kepusha shari, heri wapatanishi maana wataitwa wana wa Mungu, moja ya kupatanisha ni kuwaambia achana na haya, tunabaki wamoja.

 

Apinga Operesheni Ukuta

Masaju alisema agizo lilitolewa na Jeshi la Polisi limegusa vyama vyote baada ya kupata taarifa za kiupelelezi kuhusu uwepo wa uvunjfu wa amani.

“Kwenye suala hili tunahitaji kuwa na msimamo, hakuna haja ya ushabiki kwani hakuna atakayekuwa salama. Ombi langu kwa viongozi na wananchi, kiujumla watambue tamko la polisi linahusu vyama vyote na taasisi zake. Tusifikie hatua tukavinyanyapaa hivi vyombo vya dola tutavifanya viwe dhaifu.

“Vyama vya siasa viache kauli zinazochochea uvunjifu wa amani, mfano Operesheni Ukuta. Neno Operesheni ni hatua za kijeshi, mfano JKT zile operesheni zipo kwa mujibu za taratibu zao. Jeshi la wananchi Tanzania ndiyo siku yao ya kuzaliwa, maana yake ni kudharau lile jeshi,” alisema.

Alisema operesheni hiyo inakuja katika siku ambayo kuna tukio la kupatwa kwa jua mkoani Mbeya, hivyo inaweza kuwasababisha baadhi ya watalii watakaokuja kushuhudia tukio hilo kuogopa kuja nchini.

 

Magufuli havunji Katiba

Katika hatua nyingine mwanasheria huyo alisema kauli ya Rais Magufuli kuhusu kupiga marufuku mikutano na maandamano ya kisiasa hadi mwaka 2020, ilitokana na taarifa za kijasusi alizozipata.

“Rais alisema kwa uwezo wake kama amiri jeshi mkuu na Rais wa Tanzania na yeye tusimuingize humu ndani, Rais alitangulia kusema kabla ya Ukuta, Rais anafanyia kazi taarifa baada ya kupewa na mamlaka kamili ya usalama, Jeshi la polisi ndio wamesema haya, sasa anasababu gani ya kutoheshimu amani na usalama wa nchi hii,” alisema.

Alisema mikutano inayofanywa na Rais Magufuli na Waziri Mkuu Kasim Majaliwa, ni mikutano halali ya kiserikali na si ya kisiasa kama baadhi ya watu wanavyodai.

“Ibara ya 29, 30, inaruhusu kuchukua hatua kulinda amani na uhuru, hivyo lazima kuzingatia haki na wajibu, inategemea anafanya mikutano hiyo kwa nafasi hipi, kama ni ya kiserikali hakuna tatizo, kwa sababu tunaona mikutano hiyo ya hadhara si ya CCM anakuatana na wananchi wa pande zote, anazungumzia mambo ya maendeleo, si mambo ya vyama. Haendi kuomba kura,” alisema.

Hata hivyo Masaju alisema licha ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi kushauri kutumia sheria ya vyama vya siasa ambayo ina baraza mahsusi kumaliza tofauti zao, Chadema walimpuuza.

Alisema ingawa Chadema wamekuwa wakidai kupinga udikteta, tayari Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora iliweka bayana kuwa hakuna udikteta nchini.

“Iliwashauri kwamba waondoe neno dikteta kutoka kwenye misamiati yao,” alisema na kuongeza. “Wanaodai kuwa katazo za Jeshi la Polisi kuhusu operesheni Ukuta ni kinyume cha Katiba na Sheria ya vyama vya siasa hawana taarifa za kutosha.

“Katika Katiba ya mwaka 1977, Ibara ya 20 (1) inatoa uhuru na haki ya watu kukutana kwa ajili ya mambo yao ila kwa amani. Kuna pande mbili zinasigana kundi moja linasema litaandamana kupinga udikteta na lingine linasema litaandamana kupinga kauli hiyo, hivyo Polisi wana uhalali wa kuzuia hayo maandamano kwa sababu wana nguvu za kukusanya taarifa za kiupelelezi kwa kupitia idara zake.

“Inashangaza kuona watu wanashangilia polisi kuuawa wakati silaha zinachukuliwa bila kujua zitatumika kwa matukio gani, wanaoandaa mikutano ya kisiasa wanaandama kwa amani ila tutajuaje kuwa wanaweza kujipenyeza na kuvunja amani?.

“Ibara ya 20 (2) inapiga marufuku kwa chama kutumia nguvu kutimiza malengo yake. Ukaidi ambao ni amri halali za polisi, pia kuna maamuzi ya mahakama. Ibara ya 30 (1) inatilia mkazo juu ya kulinda heshima na mamlaka ya mahakama, kwa sababu mahakama ndio inayotoa haki, lazima iheshimike, sasa halijaisha hilo wanasema wanaendelea na maandamano. Hiyo mahamaka hadhi yake katika jamii itashuka,” alisema.

Aidha alisema polisi wapo wachache hivyo hawawezi kutosha kulinda maandamano hayo nchi nzima kwa sababu Watanzania wapo zaidi ya milioni 45.

“Ile sheria ya vyama vya siasa, kifungu cha 11 imewataka kuzingatia mamlaka, ambayo sasa wanapewa na Jeshi la Polisi. Polisi wamepewa mamlaka kifungu cha 43 cha sheria ya Jeshi la Polisi. Kwa mazingira kama haya kuna uhalali wa jeshi hilo kuzuia maandamano hayo,” alisema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here