AG Kenya aliyewekewa vikwazo vya kuingia Marekani afunguka

0
557
Mwananasheria Mkuu wa zamani wa Kenya, Amos Wako.

NAIROBI, KENYA

MWANASHERIA Mkuu wa zamani wa Kenya, Amos Wako amepinga vikali hatua ya Marekani kumwekea marufuku ya usafiri yeye na familia yake nchini humo.

Wako amesema hatua ya Marekani dhidi yake ni kufufua kesi ya zamani ambayo haelewi lengo lake ni nini.

”Kwa miaka minane sipo serikalini. Tangu nilipostaafu japo visa vya ufisadi vimekithiri mno, jina langu halijatajwa au kuchunguzwa kuhusiana na visa vya ufisadi,” aliwaambia wanahabari.

Anasema sababu ya yeye kuwekewa marufuku ya kusafiri mara ya kwanza na hivi sasa ilikuwa ni kuhusishwa kwake na visa vya ufisadi na kwamba vyote vinatokana na kazi yake ya zamani kama Mwanasheria Mkuu.

Aidha Wako amesema kuwa haelewi kwanini anawekewa vikwazo vipya wakati kuna marufuku inayohusiana na suala hilo miaka 10 iliyopita.

”Badala ya kukabiliana na ufisadi wanafufua visa vya zamani ambavyo havina msingi wowote” alisema.

Hii mara ya pili kwa Marekani kumpiga marufuku Mwanasheria Mkuu huyo Amos Wako, ikidai alijihusisha kwa kiwango kikubwa na ufisadi.

Kulingana na waziri  mambo ya nje wa Marekani, Mike Pompeo marufuku hiyo ni kwa sababu ya Wako kuhusishwa na ulaji rushwa na ufisadi.

Hatahivyo, taarifa hiyo haijaelezea waziwazi ni vitendo gani vya rushwa au ufisadi Wako alihusika navyo.

Marufuku hiyo pia inamhusisha mkewe na mwanawe.

Hatua ya Marekani ya kumpiga marufuku Wako imechukuwa sura mpya, baada ya tume ya serikali ya kupambana na ufisadi maarufu kama EACC kusema kwamba ilishiriki kikamilifu katika hatua hiyo.

Mkuu wa tume ya EACC, Dk. Eliud Wabukala amenukuliwa na vyombo vya habari nchini Kenya akisema kuwa tume yake imekuwa mstari wa mbele kutoa habari na maelezo kuhusu ufisadi kwa Marekani na balozi za kigeni.

Wabukala ameashiria kwamba huenda Wakenya wengine mashuhuri wakakumbwa na hali kama iliyomfika Wako.

Wadadisi wa mambo wanasema kwamba huenda vikwazo vya usafiri vinavyomkumba Wako vilitokana na kashfa ya kifedha ya Anglo Leasing, ambayo ilisababisha Serikali ya Kenya kupoteza mabilioni ya fedha.

Kashfa hiyo ililipuka wakati Wako alipokuwa akihudumu kama mkuu wa sheria, na alinyoshewa kidole cha lawama kwa madai ya kuwa kizuizi katika uchunguzi wa sakata hilo.

Mwaka wa 2009,   aliyekuwa Naibu wa Waziri Mambo ya Nje wa Marekani, Johnnie Carson, ambaye alikuwa anazuru Kenya, alitangaza kwamba Wako amepigwa marufuku kuzuru Marekani kwa madai kwamba amekuwa kikwazo kwenye vita dhidi ya ufisadi nchini Kenya.

Hatua ya sasa ya kuwanyima vibali vya kusafiri Wako, mkewe Flora Ngaira na mtoto wake wa kiume, Julius Wako inamaanisha kwamba watatu hao hawawezi kuzuru Marekani au kufanya biashara na kampuni za Marekani.

Hatahivyo, Wako, ambaye kwa sasa ni Senata nchini Kenya, anaweza kukanyaga kwenye ardhi ya Marekani ila tu kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa, ingawa haruhusiwi kwende nje ya mipaka ya makao hayo.

EACC kupitia kwa mwenyekiti wake, Eliud Wabukala ilidai ilishirikiana  kwa kiwango kikubwa na wachunguzi wa Marekani kuwekwa kwa marufuku hiyo.

Marekani ilisema kuwa hatua hiyo inakusudiwa kuisadia Kenya katika vita dhidi ya ufisadi.

Wadadisi wanadai kuwa huenda matatizo ya Wako yalitokana na sakata ya Anglo Leasing iliyohusu kandarasi za usalama zenye thamani ya mamilioni ya madola ambapo Serikali ilipoteza fedha hizo zinazoaminika ziliishia kufichwa katika mataifa ya nje.

Wako alikuwa akihudumu kama Mwanasheria Mkuu wakati sakata hilo lilipoanza na analaumiwa kwa kuzuia uchunguzi wa wizi huo.

Mwaka 2009, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Johnnie Carson, alizuru Kenya, alitangaza kuwa Wako alipigwa marufuku ya kuingia nchini Marekani kwani alionekana kuwa kizingiti dhidi ya ufisadi.

Marufuku hiyo ilikuwa ya kwanza kwa Wako.

Marufuku ya sasa inamaanisha kuwa Wako na familia yake ya karibu mbali na kutoruhusiwa kuingia Marekani pia hawatakubaliwa kufanya biashara yoyote na serikali ama kampuni za Marekani.

Wako alikuwa mwanasheria mkuu wa Kenya kwa muda wa miaka 20, kati ya mwaka 1991 na 2011.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here