29.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

AG asubiriwa utekelezaji marufuku wakurugenzi kusimamia uchaguzi

Na AGATHA CHARLES

-DAR ES SALAAM

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesema inasubiria nakala ya hukumu kutoka mahakamani kupitia Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) iliyobatilisha kifungu cha Sheria ya Uchaguzi namba 7(1) na 7(3) kinachowaruhusu wakurugenzi wa majiji, manispaa na halmashauri kuwa wasimamizi wa uchaguzi nchini ndipo ijue cha kufanya.

Hayo yalielezwa jana kwa njia ya simu na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Dk. Athuman Kihamia baada ya MTANZANIA Jumapili kutaka kufahamu walivyopokea hukumu hiyo na watakavyojipanga kusimamia uchaguzi.

“Hatujaipata hiyo hati ya hukumu kutoka mahakamani kupitia kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, hapo tukakapoipata ndipo tutakapojua,” alisema Dk. Kihamia.

Gazeti hili lilimtafuta Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Dk. Adelardus Kilangi lakini hakuweza kupatikana baada ya simu zake kuita pasipo kupokewa.

Juzi, Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam ilibatilisha kifungu cha Sheria ya Uchaguzi namba 7(1) na 7(3) kinachowaruhusu wakurugenzi wa majiji, manispaa na halmashauri kuwa wasimamizi wa uchaguzi nchini.

Katika kesi hiyo namba 8/2018, ambayo mjibu maombi alikuwa ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) ilifunguliwa na mwanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Bob Wangwe, aliyekuwa akiwakilishwa na Wakili Fatma Karume (ambao ndio waleta maombi) na walikuwa wanapinga kifungu cha sheria ya vyama vya siasa kinachotumiwa na NEC kuwateua wakurugenzi hao kuwa wasimamizi wa uchaguzi.

Akisoma hukumu hiyo mahakamani hapo juzi, Jaji Atuganile Ngwala, alisema kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi, kifungu namba 7(1) na 7(3) ni batili kwa sababu kinatoa nafasi kwa wateule wa Rais ambao pia si waajiriwa wa NEC kusimamia uchaguzi.

Alisema kifungu cha 7(1), kinasema kuwa kila Mkurugenzi wa Jiji, Manispaa na Halmashauri anaweza kusimamia uchaguzi wakati viongozi hao ni wateule wa Rais na si waajiriwa wa NEC wakati Katiba inasema NEC inapaswa kuwa huru na haki.

Jaji Ngwala alisema kutokana na hali hiyo, kifungu hicho kinakinzana na katiba mama ambayo inasimamia nchi.

Alisema lakini pia kifungu cha 7(3) kinasema kuwa NEC inaweza kuteua mtu yeyote kuwa msimamizi wa uchaguzi bila ya kuainisha ni mtu wa aina gani.

Kwamba Katiba inasema kuwa mtu yeyote aliyekuwa msimamizi wa uchaguzi hapaswi kuwa mwanachama wa chama chochote cha siasa.

Hivyo alisema kutokana na vielelezo vilivyowasilishwa mahakamani hapo na upande wa waleta maombi, vimeonesha pasi na shaka kuwa wasimamizi wa uchaguzi wana masilahi na wateule wao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles