MWANASHERIA Mkuu wa Serikali (AG) amewasilisha maombi Mahakama Kuu kuzuia mali zote za mtuhumiwa wa dawa za kulevya, Muharami Abdallah maarufu Chonji na mkewe kuhamisha umiliki, kupangishwa ama kuombea mikopo.
Maombi hayo dhidi ya Chonji na mkewe Mwalibora Nyanguri yaliwasilishwa kwa hati ya dharura Septemba 13 mwaka huu na kupangwa kusikilizwa mbele ya Jaji Wilfred Dyansobela.
AG anaiomba mahakama imzuie Chonji, mawakala wake ama mtu mwingine yoyote kwa niaba yake kuhamisha umiliki wa mali, kupangisha nyumba au kuombea mikopo.
Mahakama inaombwa kutoa zuio hilo kwa nyumba sita zilizopo maeneo ya Magomeni, Tandale Ziota na Mbezi juu.
Nyumba hizo ni namba 95280 iliyopo kiwanja namba 43 kitalu O, namba 90292 iliyopo kiwanja namba 66 kitalu P, nyumba iliyopo kiwanja namba 68 kitalu X, nyumba yenye mita ya luku namba DRN43001304757 na nyumba nyingine yenye mita ya luku namba 04215118664.
Pia gari aina ya Canter yenye namba za usajili T376 BYY na mali nyingine zote zenye jina ama umiliki wa Kampuni ya Mumask Investment.
AG anaomba mke wa Chonji, Mwalibora, mawakala wake ama mtu mwingine yoyote kwa niaba yake asihamishe umiliki wa gari aina ya Toyota Verrosa yenye namba za usajili T326 BXF.
Katika maombi hayo anamwomba Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni na Ofisa Mtendaji wa Mtaa wasipitishe uhamishaji wa umiliki wa nyumba hizo na mahakama imwamuru Msajili wa Ardhi kutambua kwamba nyumba hizo zimewekewa pingamizi.
Maombi hayo kwa mara ya kwanza yalitajwa katika mahakama hiyo Novemba 12 mwaka huu, mahakama iliamuru wadaiwa kuwasilisha hati kinzani Novemba 26 na AG atajibu Desemba 3 na maombi yatasikilizwa Desemba 4 mwaka huu.
Chonji anakabiliwa na kesi ya jinai namba 50 ya mwaka 2014 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ambapo anatuhumiwa kujihusisha kusafirisha dawa za kulevya zenye thamani ya Sh 227, 374,500 na kesi hiyo inasikilizwa na Hakimu Mkazi, Janeth Kaluyenda.
Hata hivyo katika Mahakama ya Kisutu kesi hiyo itatajwa Novemba 25 mwaka huu.