Afya ya Rais mstaafu Moi yadaiwa kuzorota

0
543

NAIROBI, KENYA

RAIS wa zamani wa Kenya, Daniel arap Moi, amefikishwa hospitalini kufanyiwa ukaguzi wa afya yake kwa mara ya pili katika muda wa wiki mbili.

Vyombo vya habari vya Kenya vimeripoti kuwa msemaji wa kiongozi huyo, Lee Njiru, alisema yupo hospitali anahudumiwa na kikosi cha wataalamu wa afya wanaoongozwa na daktari wake, David Silverstein.

“Yupo macho (Moi) na anafahamu kinachoendelea,” alisema Njiru.

Awali gazeti la Daily Nation kwa kunukuu duru kutoka familia ya kiongozi huyo, lilisema Moi alikimbizwa hospitalini Jumapili baada ya kupata matatizo ya kupumua.

Hata hivyo, Daily Nation linaripoti kuwa jamaa mwingine kutoka familia ya Moi alikanusha taarifa hiyo.

Familia hiyo imeeleza katika taarifa yake kutofurahishwa na habari ambazo imezitaja kuwa ‘mbaya na za kuzusha mshtuko’ zinazosambazwa.

Gazeti jingine nchini humo la The Star, limeripoti kwamba Moi yuko katika hali mahututi.

Si mara ya kwanza taarifa za kiongozi huyo wa zamani kuugua kusambaa katika vyombo vya habari nchini.

Mwishoni mwa mwaka jana palikuwa na taarifa pia za Moi kufikishwa hospitalini kufanyiwa uchunguzi kama ilivyo kwa wakati huu.

Kwa mara nyingine, Njiru alinukuliwa na vyombo vya habari akisema; “Mzee aliruhusiwa kwenda nyumbani baada ya matabibu wakiongozwa na daktari wake Silverstein kuridhika na afya yake baada ya uchunguzi.”

Kwa mujibu wa taarifa kutoka ofisi yake iliyotumwa kwa vyombo tofauti vya habari, Machi mwaka jana kiongozi huyo mstaafu alipelekwa Hospitali ya Ichilov huko Tel Aviv, nchini Israel ambako taarifa zilieleza alikwenda kufanyiwa uchunguzi.

Baada ya kulazwa kwa muda aliruhusiwa kurudi nchini Kenya ambako ilibainika baadaye kwamba alikwenda kufanyiwa uchunguzi wa goti lake lililokuwa linamsumbua.

Raila Odinga ni miongoni mwa viongozi wa kisiasa waliofika Kabarak, ambako ndio anakoishi Moi, ili kumtakia afya njema baada ya kulazwa hospitalini nchini Israel kwa takriban mwezi mmoja.

Moi alizaliwa Septemba mwaka 1924 katika eneo la milimani huko Baringo eneo la Bonde la Ufa kaskazini mwa Kenya.

Aliinukia kutoka kuwa kijana aliyekuwa mchungaji mifugo na kuwa mwalimu katika shule ya kimisionari na baadaye kushikilia usukani wa taifa kama rais wa pili Kenya alipomrithi Jomo Kenyatta.

Chini ya utawala wa Kenyatta, alikuwa makamu wake wa rais. Alipokea wadhifa wa rais Agosti mwaka 1978 baada ya Kenyatta kufariki dunia.

Aliiongoza Kenya kwa miaka 24 kuanzia mwaka 1978 hadi 2002.

Moi alikuwa kiongozi pia wa chama tawala wakati huo cha Kanu, kilichofanikiwa kupata ushindi katika uchaguzi miaka kadhaa nchini Kenya.

Kanu kilipoteza ushindi mwaka 2002, wakati Mwai Kibaki akiwa na muungano wa kisiasa wa National Rainbow Coalition alipochaguliwa kuwa rais wa Kenya.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here