‘AFYA YA MAMA, MTOTO BADO CHANGAMOTO’

0
582

Na LEONARD MANG’OHA-DAR ES SALAAM


HUDUMA duni za afya katika hospitali na vituo vya afya nchini, zimeendelea kusababisha vifo na matatizo mengine kwa mama na watoto wachanga kutokana na kukosa huduma stahiki baada ya kujifungua.

Akizunguma Dar es Salaam juzi, Mkuu wa Shule ya Afya ya Chuo Kikuu cha Aga Khan, Profesa Columba Mbekenga, alisema katika hospitali nyingi za Serikali mama hutakiwa kuondoka muda mfupi baada ya mama kujifungua ili kuwapisha wengine jambo ambalo si zuri kiafya.

Alisema kwa kawaida baada ya mama kujifungua anatakiwa kuendelea kuwapo hospitali ili afanyiwe uchunguzi wa kwanza, ambao hufanyika baada ya saa 24 tangu anapojifungua na kufuatiwa na ule wa siku saba, 28 na 42 ili kukamilisha mara nne.

Wakati akisema hayo, sera ya taifa ya huduma ya afya ya mama na mtoto ya mwaka 2007 inaeleza kuwa huduma hiyo inatolewa hadi siku 28. Inaeleza huduma hizo kuwa ni pamoja na chanjo, tiba, elimu ya uzazi na uzazi salama, mbinu shirikishi za udhibiti wa magonjwa ya watoto, afya na lishe.

Akiwasilisha utafiti huo uliofanywa katika vituo vya afya 27 wilayani Ilala, mtafiti Eunice Pallangyo ambaye ni mwanafunzi wa ngazi ya shahada ya uzamivu katika Chuo Kikuu cha Uppsala cha Sweden, alisema kila vizazi hai 1,000 wototo 25 hupoteza maisha, huku wanawake 556 kati ya laki moja wakipoteza maisha ndani ya wiki sita tangu kujifungua.

Alisema wanawake wanaohudhuria hospitali baada ya kujifungua ni asilimia 34, vichanga 42 na wajawazito 95.

“Watoa huduma wengi katika vituo nilivyofanya utafiti wanaelewa kuhusu huduma ya mama na mtoto baada ya kujifungua. Asilimia 64 walisema wanaelewa, lakini walilalamika kuwa watu wengi wanaofanya utafiti hawarudishi matokeo yanayoweza kuwasaidia kuboresha penye upungufu,” alisema Pallangyo.

Alisema licha ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kuwa na mwongozo wa huduma ya mama na motto, lakini watoa huduma wengi wamekuwa hawafanyi kwa kufuata mwongozo huo.

Alisema kwa mujibu wa utafiti wa Shirika la Afya la Kimataifa (WHO), watoto wanaofanyiwa utafiti ndani ya siku mbili tangu kuzaliwa wmeongezeka kutoka asilimia 13 mwaka 2004 hadi 34 mwaka 2015.

Alisema licha ya kuongezeka kwa kiwango hicho, bado ongezeko hilo ni dogo ikilinganishwa na idadi ya watu wanaopoteza maisha.

Naye Mkuu wa Chuo cha Aga Khan, Profesa Joe Lugalla, alisema kuwa mbali na kutoa mafunzo ya kielimu kwa wanafunzi, wanafarijika kujihusisha na kazi za kijamii, ikiwamo kusaidia jamii inayowazunguka.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here