Afya ya Clinton inapokuwa mtaji kambi ya Trump

Moja ya picha zinazodaiwa zinaonesha afya dhoofu ya Hillary Clinton.
Moja ya picha zinazodaiwa zinaonesha afya dhoofu ya Hillary Clinton.
Moja ya picha zinazodaiwa zinaonesha afya dhoofu ya Hillary Clinton.

NA JOSEPH HIZA,

WAKATI mpinzani wake Donald Trump akishambuliwa zaidi kwa kauli za kibaguzi dhidi ya jamii mbalimbali za wachache, Hillary Clinton ana madongo anayotupiwa, ambayo pia yanatishia ndoto yake ya kuwa rais wa kwanza mwanamke Marekani.

Amekuwa akiandamwa kuanzia uzembe alipokuwa Waziri wa Mambo ya Nje, uliopelekea kuuawa kwa wanadiplomasia wa Marekani nchini Libya, kashfa ya kutumia barua pepe binafsi katika masuala nyeti hadi kuihusu taasisi ya Clinton Foundation.

Katika hili la Clinton Foundation, kashfa zinahusishwa na wakati alipokuwa waziri katika muhula wa kwanza wa Rais Barack Obama.

Licha ya kuwa asasi hiyo kusaidia mamia kwa mamilioni ya watu katika nchi zaidi ya 100, inadaiwa ilipokea fedha chafu kutoka kwa ‘wahalifu’ waliolenga kununua ushawishi.

Anadaiwa licha ya kuwa alimuahidi Obama kuanika wahisani wa taasisi hiyo kila mwaka, akiwa waziri lakini hadi anaondoka wizarani hakufanya hivyo, hali inayowafanya akina Trump waishikie bango kutaka ichunguzwe.

Kutokana na wasiwasi wa wafuasi wake kuhusu kashfa hizi, Clinton anayeongoza kura za maoni dhidi ya Trump, wiki iliyopita aliahidi kuwa hazitatokea nyingine zaidi kubwa kuihusu asasi hiyo, wala masuala ya barua pepe au kitu kingine chochote kinachoweza kumkwamisha kumshinda Trump Novemba mwaka huu.

Alisema programu za Clinton Foundation zitaendelea hata akichaguliwa rais licha ya kuwa anafahamu fika Trump na wakosoaji wake watashupalia uwapo mgongano wa maslahi.

Lakini katika hilo hakugusia utata unaovumishwa kuhusu afya yake, ambao bila shaka ni miongoni mwa aliyomaanisha aliposema ‘…kitu kingine chochote kile.’.

Kipindi cha zaidi chini ya mwezi mmoja, madai yasiyothibitishwa kuhusu afya ya Clinton yametamba katika mitandao ya jamii kuanzia Twitter hadi kuwa silaha muhimu ya mashambulizi ya kambi ya Trump.

Ijapokuwa ni uvumi uliopo tangu mwaka jana, mwezi mzima uliopita wa Agosti ulitawala zaidi.

Bila kutoa ushahidi wowote, wiki iliyopita, Trump alikaririwa akisema akiwa katika jimbo la Ohio kuwa Clinton hana ukakamavu wa afya kiakili na kimwili kuweza kupambana na wanamgambo wajiitao Dola la Kiislamu (IS) wala changamoto nyingi zinazolikabili taifa hilo.

Na kitendo cha daktari wa bilionea huyo wa New York mwenye umri wa miaka 70, kutoa ripoti ya afya yake, ikionesha yu fiti, imezidisha jeuri ya mashambulizi dhidi ya Clinton ambaye kiumri amemzidi miaka miwili.

Sehemu kubwa ya ripoti za hivi karibuni kuhusu afya ya Clinton zinadai hakupona kutokana na maradhi ya mgando wa damu (blood clot) aliougua mwaka 2012 na analifanya hilo siri.

Lakini madaktari wake wanasema alipona maradhi hayo baada ya upasuaji. Barua ikiambatana na ripoti ya uchunguzi mwaka jana ikiwamo kutoka daktari wake binafsi Lisa Bardack ilisema ‘Clinton yu mwenye afya njema na anafaa kuhudumia nafasi ya urais wa Marekani.

Kinachoonekana wazi, kambi ya Trump kwa namna fulani inaweza isiwe na ushahidi wa madai yake, lakini inajua fika nadharia hizi za njama zina uwezo wa kuwateka wapiga kura, hasa wale wasio na muda au uwezo wa kutenganisha ukweli na uongo na au wanaoamini kile kinachosemwa au kuvumishwa na fulani.

Ilianzaje? Mapema wakati wa kiangazi hiki: watumiaji wa Twitter walianza kunong’ona kuhusu afya ya Clinton wakitumia ‘hashtag’ # HillaryHealth.’’

Agosti 4: tovuti ya Infowars, inayoendeshwa na mwananadharia wa njama mhafidhina Alex Jones, ilianza kuchapisha mfululizo wa habari kuhusu uduni wa afya yake.

Simulizi zilienda sambamba na kipande cha video kikimuonesha Clinton akitaniana na mwandishi wa Shirika la Habari la Associated Press Juni mwaka huu.

Mwanablogu huyu alikitumia kipande hicho kama ushahidi kuwa mke huyo wa zamani wa Rais wa 42 wa Marekani, Bill Clinton hupatwa na kifafa hata akiwa mbele ya hadhara.

Mwandishi Lisa Lerer aliandika, akipinga madai hayo. “Pale nilipoona akiepa, wao wanadai kuona kifafa,” anaandika.

Siku tatu baadaye, mwanablogu mwingine mhafidhina Matt Drudge alisambaza picha za Clinton akisaidiwa na wasaidizi wake baada ya kuteleza ngazini huku kukiwa na kichwa kisemacho ‘Hillary aziteka ngazi’.

Hata hivyo, kuna kasoro katika madai yake hayo aliyoyaita mada kuu ya kampeni 2016, ni kuwa picha hizo  zilichukuliwa Februari mwaka huu na habari ziliripoti wakati huo kuwa aliendelea na kampeni baada ya kuteleza kidogo.

Infowars pia iliitolea zaidi maelezo picha hiyo, ikidai mmoja wa wanaomsaidia ni daktari na kitu alichoshikilia mkononi ni sindano kwa ajili ya dawa ya diazipamu (diazepam).

Kwa taarifa; Diazepam husaidia kulegeza misuli, kutuliza maumivu na hutumika kusimamisha shambulio la mara kwa mara la kifafa.

Aidha mapema mwezi huo, jarida la udaku la National Enquirer, ambalo linamuunga mkono Trump katika mbio za urais, lilitoa habari isemayo ‘Usiri wa Afya Mgogoro ya Hillary Clinton.”

Kwa siku tatu mfululizo,  mtangazaji wa Fox News, Sean Hannity alirusha vipande mbalimbali vya video kuhusu afya ya Clinton, akidai anasumbuliwa na kifafa huku akigusia mazungumzo baina ya Clinton na Lerer kama ushahidi kuunga hayo.

Lakini Lerer amekana akisema hakuwahi kuwasiliana na Fox News.

Aidha Hannity alikuja na ripoti ya kitabibu kuonesha ukweli wa madai yake, lakini madaktari husika wamekana. Katika CNN, mfuasi wa Trump, Jeffrey Lord pia alirudia madai hayo.

Katikati ya Agosti, vyombo vya habari ikiwamo CNN na Washington Post zilikana madai yanayotolewa na Hannity na Infowars huku mwandishi wa CNN, Brian Stelter akiita taarifa za Hannity kuwa za ‘hovyo.’

Wiki iliyopita, kambi ya Clinton ilitoa taarifa ikisema kambi ya Trump ilikuwa ikiendesha  njama za kipuuzi kuhusu afya ya Clinton. Taarifa hizo kwa wanahabari zilitoka pia kwa Dk. Bardack, daktari binafsi wa Clinton.

Aidha kipindi hicho, mtandao wa Drudge ilirudi na ripoti nyingine iitwayo ‘Mito kwa ajili ya Hillary’, ambayo ilienda na picha mbalimbali akiwa amekaa kitini na mito kuegeshwa kumlinda asianguke.

Baadaye siku hiyo, msemaji wa kambi ya Trump, Katrina Pierson alidai Clinton anaugua ‘dysphasia,’ ambayo ni maradhi hatari ya neva yanayoathiri matamshi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here