30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

AFRIKA SASA VIPANDE VIPANDE

9255646-detail-color-map-of-african-continent-with-borders-each-state-is-colored-to-the-various-color-and-ha-stock-vector

NA MARKUS MPANGALA

MBIO za kuwania rasilimali za wananchi wa Bara la Afrika zimeshika kasi, huku kukiwa na ushindani mkubwa katika medani ya biashara, uwekezaji, ushirikiano wa uchumi na diplomasia kati ya bara hili na mataifa makubwa ya kigeni pamoja na yanayokuja kasi kiuchumi kutoka barani Asia, Ulaya na Amerika.

Toka karne ya 19 kulikuwa na nguvu kubwa kutoka Bara la Ulaya kiuchumi na viwanda, kabla ya kupigwa kumbo katika karne ya 20 na Marekani, ambayo iliibuka kuwa taifa lenye nguvu kiuchumi, biashara na kijeshi.

Katika karne ya 21 kumeibuka mataifa ya Bara la Asia ambayo yamechukua nafasi kubwa ya ushawishi, ingawa nchi za Ulaya na Marekani haziko nyuma.

Kutokana na ushindani huo, umetengeneza mwanya mpya wa kuunda ushirikiano baina ya nchi mbalimbali la Ulaya, Asia, Marekani na Afrika. Mathalani, kumekuwa na makubaliano ya nchi na nchi (China na Tanzania au Angola).

Pia kuna makubaliano ya kijumuiya (China na Jumuiya ya Afrika Mashariki kisha ya Bara zima la Afrika). Kwa mfano, kuna makubaliano ya kiuchumi na biashara kati ya Afrika-Asia, ambayo ni ya kijumuiya.

Unapoongelea biashara, uwekezaji (Foreign Dirent Investment), masoko katika majukwaa ya kidunia Bara la Afrika lazima litawale mazungumzo hayo. Kwasababu linaonekana ndilo limekamata fursa nyingi za miaka ijayo ya rasilimali zake; watu, ardhi na malighafi za viwandani.

Swali kubwa linalobaki ni kwamba, wananchi na viongozi wa Bara la Afrika wamejitayarisha vipi ili kuweza kutumia fursa zinazoambatana na nafasi yake hiyo duniani katika maeneo ya biashara na uwekezaji?

Ndiyo kusema je, tutaweza kusimama kuhakikisha uvunaji wa rasilimali zetu unazalisha tija itakayotuwezesha kujikwamua na umaskini, ujinga na maradhi au tutashindwa na kuendelea kutumika kama daraja la kuwezesha jamii nyingine kuvuka kuelekea kwenye maendeleo na ustawi?

Je, tumejenga mifumo na uwezo wa kitaasisi, kisera na kisheria kutufanya tuwe na nguvu na mamlaka juu ya rasilimali zetu ambazo ndiyo hasa lengo la hayo makongamano?

Kufikia hapo tunaona Afrika imegawanywa vipande vipande na kila taifa kubwa linakumbatia kipande chake binafsi na kwa kutumia ukanda au bara zima kwa ujumla. Tunakumbuka miaka ya nyuma kulikuwa na mikutano kama Bandung (Bandung Conference) iliyowahusisha viongozi wa mataifa ya Afrika na Asia, hususan baada ya uhuru wa nchi hizo.

Kutoka Aprili 18-24 mwaka 1955 hadi leo mbinu zimeongezeka na kushamiri zaidi katika ushirikiano wa biashara na uwekezaji. Kwa ajili hiyo, tunasema Afrika imegawanywa kwenye vipande tofauti tofauti na kila taifa kubwa na lenye uchumi mzuri linavutia kwake.

MAREKANI-AFRIKA 

Februari 1 hadi 4, mwaka huu, kulifanyika mkutano wa marais wa Afrika na Serikali ya Marekani. Mkutano huo ulihusu ajenda zilezile za kibiashara baina ya Marekani na nchi za Afrika, ulifanyika mjini Addis Ababa, nchini Ethiopia.

Katika mkutano huo, wawakilishi wa makampuni ya biashara, mameneja, wataalamu wa sera na utawala, wawekezaji na maofisa wa serikali takribani 1,400 walialikwa. Malengo makubwa yalikuwa ushirikiano wa kibiashara, mafanikio, mikakati na mwamko mpya wa ushirikiano baina ya mataifa hayo.

Hiki ni kipande cha kwanza cha Afrika ambacho kinavutiwa kwenye mkondo wa biashara na uwekezaji kwa Marekani, mbali ya ushirikiano wao uliopo kwenye AGOA.

MIKAKATI YA CHINA KWA AFRIKA

Kongamano (China-Africa Summit) kati ya Serikali ya China na viongozi wa nchi 50 za Afrika ulifanyika Desemba 5, 2015, mjini Johannesburg, Afrika Kusini. Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete, alipewa mwaliko kama balozi wa heshima wa ushirikiano wa China na Afrika. Tanzania iliwakilishwa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu na Waziri wa Mambo ya Nje, Dk. Augustine Mahiga.

Mkutano huo wa 6 wa Forum on China-Africa Cooperation (FOCAC) ulikuwa chini ya uenyekiti wa Rais Xi Jinping wa China, ambaye anasimamia ajenda ya nchi yake ya ushirikiano wa kiuchumi na Afrika hadi mwaka 2063, ikiwemo hatua ya kwanza ya miaka 10.

Ushirikiano huo umo katika kilimo na uhifadhi wa chakula kupitia programu ya CAADP (Comprehensive African Agriculture Development Program), miundombinu, afya, utalii, nishati na madini, mabunge ya nchi, kikanda na Bunge la Umoja wa Afrika pamoja na NEPAD.

Mbali ya hayo, tunafahamu China imekuwa ikitumia misaada barani Afrika kama chambo cha kuatamia rasilimali muhimu za madini, mafuta na masoko. China imejifunga mkanda na kuwekeza zaidi ya pauni bilioni 7 katika sekta ya miundombinu barani Afrika pekee.

Novemba mwaka 2006, viongozi wa Afrika takribani 48 walihudhuria Kongamano la Kibiashara kati ya China na Afrika lililofanyika Beijing. Serikali iliahidi kuzidisha mara mbili misaada yake na kupanua soko la bidhaa za Afrika nchini China.

Kwa mujibu wa kitabu cha ‘Congo Masquerade’ kilichoandikwa na mwandishi Theodore Trejorn (Uk.55): “China imekuwa muuzaji mzuri wa silaha nchini Sudan na kwingine kwa miaka. China pia imewekeza katika sekta ya mafuta na gesi barani Afrika.

Faida anazovuna China barani Afrika zimeyashtua mataifa ya Ulaya na Amerika, kila moja likijikusanya kutumia kila aina ya mbinu kuhakikisha nazo zinanufaika.

SOKO LA AFRIKA NA UINGEREZA

Afrika Kusini ndiyo nchi inayoongoza Afrika kuwa soko kubwa la bidhaa za Mwingereza, ikifuatiwa na Nigeria. Mwaka 2005 pekee bidhaa za Mwingereza zilizouzwa Afrika Kusini zilifikia mauzo ya takribani pauni bilioni 3.2, huku uwekezaji uliofanywa na makampuni ya Mwingereza nchini Afrika Kusini ukifikia pauni bilioni 30 na zaidi.

Nchini Nigeria peke yake tuliona Uingereza iliuza bidhaa zinazokadiriwa kufikia kiasi cha pauni milioni 535 mwaka 2000 na zikapanda hadi kufikia pauni milioni 818 mwaka 2005.

Kuundwa kwa DFID (Taasisi ya Mwingereza inayohusiana na misaada) kulikuwa njia sahihi aliyoiona Mwingereza kuatamia maslahi na malengo ya kile akitoacho kama misaada, kuliko kutumia mlango wa Umoja wa Ulaya ambamo hakuwa na uwezo wa kuishikia rimoti na kuongoza.

Mwingereza aliona DFID kuwa njia sahihi zaidi kwa maslahi yake barani Afrika, kama vila mvuvi aliyeacha kutumia ndoano ya kijiji na kuamua kutumia ndoano yake binafsi kuamua kiasi na aina ya chambo atakayotumia kuvua samaki kulingana na aina ya samaki amtakaye.

Uingereza akaigeukia DFID kama ndoano yake kuvua samaki barani Afrika. Kuanzia mwaka 1997, Taasisi ya DFID ilikuja kuwa ‘kiendesha sera mjenzi’ wa Mwingereza barani Afrika.

Misaada ya Mwingereza iliyokuwa ikipitia DFID iliongezeka kutoka Pauni milioni 300 kwa msimu wa 1997 na 1998 hadi pauni bilioni 1.25 mwaka 2006 na 2007.

Asilimia 55 ya bajeti ya DFID ilitengwa maalumu kwa ajili ya Afrika, baadhi ya nchi zilizokuwa katika orodha ya kupokea misaada hiyo zilikuwa ni pamoja na Ghana, Nigeria, Sierra Leone, Sudan, Ethiopia, DR Congo, Rwanda, Uganda, Kenya, Tanzania, Zambia, Malawi, Mozambique, Zimbabwe, Lesotho na Afrika Kusini.

KONGAMANO LA ASIA-AFRIKA

Kama tulivyoona hapo awali kwamba, kuna ushirikiano baina ya nchi na nchi. Halafu kuna ule wa bara moja na jingine, kisha nchi moja yenye uchumi mzuri na bara moja la Afrika (yaani nchi 50 kwa nchi moja fadhili).

Miongoni mwake ni Kongamano la Bara la Asia na Asia. Kongamano hili ni la kibara, lakini China na Afrika ni kati ya nchi na Bara. Kwenye kongamano la Asia-Afrika nalo kunakuwa na mbano uleule wa ushirikiano wa kiuchumi.

Kwa mfano, mkutano wa Asia-Afrika uliofanyika Aprili 2015 mjini Jakarta, nchini Indonesia, mwenyekiti wake alikuwa Rais Joko Widolo na kuhudhuriwa na watu 109 na taasisi za kimataifa 25 kutoka Afrika na Asia. Madhumuni yalikuwa kusisitiza ushirikiano na maendeleo ya uchumi, diplomasia,

Akikaririwa na gazeti la Jakarta News wakati akizungumza kwenye mkutano huo, Rais Widolo alisema: “Tuwe na mtazamo kuwa kuendelea kutegemea uchumi wa dunia kutatuliwa na Benki ya Dunia, Shirika la Fedha na Benki ya Maendeleo ya Asia ni mawazo yaliyopitwa na wakati.”

JAPAN-AFRIKA

Kongamano kati ya nchi za Afrika na Japan lilifanyika Agosti 27-28 mwaka huu kwa mara ya kwanza barani humu mjini Nairobi, nchini Kenya, katika kipindi cha miaka 20 tangu lianzishwe.

Kongamano hilo linaitwa TICAD (Tokyo International Conference on African Development), ambapo mwaka huu lilikuwa la sita na lilihudhuriwa na wakuu wa nchi mbalimbali za Afrika, maofisa wa Umoja wa Mataifa, NEPAD, Kamati ya Uchumi ya Kikanda Afrika (RECs), mashirika ya sekta binafsi na kadhalika.

Ajenda kuu zilizojadiliwa ni utekelezaji wa mpango wa maendeleo wa mwaka 2030 na 2063 kwa kipindi cha miaka mitano ya awali. Maeneo yanayolengwa na mipango hiyo ni matatu; mapinduzi ya viwanda, afya na usalama wa jamii.

Je; Afrika itaweza kuzalisha bidhaa za viwandani katikati ya kuruhusu bidhaa za ughaibuni kutamba kwenye masoko yao?

 

KOREA KUSINI NA AFRIKA

Korea Kusini nayo imeingia mzigoni na kuunda kipande chake na nchi za Afrika ambacho kinaitwa “South Korea-Africa Summit”. Kongamano hilo litajumuisha wakuu wa nchi za Afrika na Korea Kusini, litafanyika mwaka huu mjini Addis Ababa, nchini Ethiopia.

Kwa mujibu wa Naibu Waziri Mkuu, Yoo II-ho, ambaye alikutana na Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika, Akinwumi Adesina mjini Seoul Machi 28, mwaka huu, Korea Kusini imeamua kupanua wigo wa ushirikiano wa kiuchumi kwa kutengeneza kipande chake cha kongamano na wadau wa Kiafrika.

Mikakati ya Korea Kusini na Afrika ni ushirikiano wa uchumi, nishati na madini, kilimo na chakula, viwanda na ushirikiano kwenye uchumi wa kikanda.

Kwa mujibu wa taarifa za wizara ya fedha ya nchi hiyo, katika awamu ya mwaka 2015/2016 Wizara ya Fedha ya Korea Kusini imetoa kiasi cha Dola 400,000 kufadhili mipango ya maendeleo vijijini, miundombinu pamoja na dola milioni 1 kwa ujenzi wa barabara mjini Cairo, Msiri, chini ya ushirikiano na Benki ya Maendeleo ya Afrika, iliyotoa dola milioni 270 na Taasisi ya misaada ya kiuchumi ya Korea Kusini (EDCF), ambayo imetoa mikopo yenye thamani ya dola milioni 600 kufadhili shughuli mbalimbali barani Afrika hadi ifikapo mwaka 2018.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles