27.3 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 17, 2024

Contact us: [email protected]

Afcon 2019 kukamilisha dili la Samatta na nyota hawa?

Na HASSAN DAUDI

FAINALI za mwaka huu zitakuwa za 32 tangu kuanzishwa kwake na safari hii zitafanyika katika ardhi ya Misri kuanzia Juni 21 na kufikia tamati Julai 19, mwaka huu.

Isisahaulike kuwa bendera ya Tanzania nayo itapeperushwa na Taifa Stars iliyopangwa Kundi C lenye Algeria, Kenya na Senegal, ikiwa ni baada ya kuikosa michuano hiyo kwa zaidi ya miongo mitatu.

Kama ilivyo kawaida, kila timu huwa na staa anayebeba matarajio ya mashabiki wake. Mfano; safari hii, Misri wanajivunia uwepo wa Mohamed Salah, kama ilivyo kwa Senegal wanaomtaja Sadio Mane, huku Algeria wakitamba kuwa wanaye Riyad Mahrez.

Hivyo basi, hakuna ubishi kuwa tumaini la mashabiki wa Stars na soka la Tanzania kwa ujumla litakuwa kwa nahodha wao, Mbwana Samatta, kutokana na kile anachokifanya sasa kule Ubelgiji akiwa na klabu ya Genk.

Lakini, wakati zikiwapo tetesi za saini yake kusakwa vikali barani Ulaya, Samatta si mchezaji pekee aliye kwenye kiwango cha juu na atakayeweza kuzitumia fainali za Afcon 2019 kuzifanya klabu kubwa ziharakishe usajili wao.

Baghdad Bounedjah (Algeria)

Ni mshambuliaji wa Al Sadd SC ya Ligi Kuu nchini Qatar, akitajwa kuwa na sifa zote za kucheza Ligi Kuu kubwa za barani Ulaya (England, La Liga, Bundesliga, Serie A na Ligue 1).

Akiwa na umri wa miaka 27, msimu huu pekee ameshafunga mabao 39 katika mechi 22 tu. Hivyo, endapo atang’ara nchini Misri, kuna uwezekano mkubwa wa klabu zenye majina kumfuata na kisha kuichukua saini yake.

Licha ya klabu za Ufaransa na Italia kutajwa kumfuatilia, pia Crystal Palace imeonesha nia ya kuitaka huduma yake.

Hakim Ziyech (Morocco)

Anahusishwa na klabu zote kubwa barani Ulaya, hasa baada ya nyota huyo wa Ajax kuumaliza msimu huu wa Ligi Kuu ya Uholanzi akiwa amezipasia nyavu za timu pinzani mara 29 katika mechi 29.

Licha ya sasa kutajwa kuhitajika Arsenal, Manchester United na Real Madrid, Ziyech atakuwa ameirahisisha zaidi safari ya kwenda kwa moja kati ya vigogo hao endapo atafanya vizuri katika fainali za Afcon 2019.

Mbwana Samatta (Tanzania)

Msimu huu ulikuwa mzuri zaidi kwa Samatta mwenye umri wa miaka 26, ambapo aliumaliza akiwa amewatungua walinda mlango mara 32 katika mechi 53.

Kwa kukumbushia, msimu huu ulimalizika akiipeleka timu hiyo Ligi ya Mabingwa, akishika nafasi ya pili katika orodha ya wafungaji bora, pia akichaguliwa kuwa Mchezaji Bora kwa wale wenye asili ya Afrika nchini humo.

Unaweza kusema fainali za Afcon 2019 zinaweza kuwa tiketi ya Samatta kutimiza ndoto zake za kucheza Ligi Kuu ya England, La Liga, Bundesliga, Serie A au Ligue 1, endapo ataipaisha Stars kule Misri.

Salif Sane (Senegal)

Ukiutazama msimamo wa Bundesliga, kikosi chake cha Schalke 04 hakikufanya vizuri msimu huu kwani ilimaliza ikiwa nafasi ya 14. Hata hivyo, hiyo haikumzuia Sane kuzivutia klabu kubwa, akitajwa kuwa mmoja kati ya walinzi wa kati bora.

Akiwa na umri wa miaka 28, nyota huyo mwenye urefu wa futi sita na inchi tano, licha ya kuwa ‘kitasa’, alimaliza msimu akiwa na mabao manne.

Kwa mafanikio hayo, ameweza kuisogeza AC Milan ambayo imepania kukifanyia marekebisho kikosi chake kilichokosa nafasi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao. 

Moussa Marega (Mali)

Waliofuatilia Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu, watakiri kuwa mshambuliaji huyo wa Porto ni moto wa kuotea mbali mbele ya mabeki na walinda mlango. 

Msimu huu wa Ligi Kuu ya Ureno, alichangia mabao 18 ya Porto, akifunga mwenyewe mara 11 na kutoa ‘asisti’ saba.

Hivyo basi, kuhamishia makali hayo katika fainali za Afcon 2019 kutazisogeza karibu zaidi klabu za Wolves na West Ham zinazomtolea macho.

Andre Onana (Cameroon)

Kama si uimara wa mlinda mlango huyo mwenye umri wa miaka 23, basi huenda Ajax isingefika nusu fainali ya Ligi ya Europa. Tayari Man United imeanza kumnyatia, ikielezwa kuwa ni mpango wa kuliziba pengo la David de Gea.

Wakati huo huo, klabu za Barcelona, Arsenal, Tottenham na West Ham nazo zimetajwa kuwa mlangoni kule Ajax, kila moja ikiulizia uwezekano wa kumpata.

Huenda mambo yakawa mazuri zaidi kwa Onana endapo atang’ara katika lango la Cameroon wakati wa fainali za Afcon 2019.

Knowledge Musona (Zimbabwe)

Huyo ni mshambuliaji wa Anderlecht anayecheza kwa mkopo Lokeren. Mashabiki wa Lokeren wanamwita ‘The Smiling Assassin’, ikimaanisha ‘Muuaji Anayetabasamu’. 

Kama ilivyo kwa Samatta, tayari jina lake limeanza kuhusishwa na klabu kadhaa za barani Ulaya, hivyo kuna uwezekano mkubwa kuwa kung’ara nchini Misri kukaziongezea kasi klabu zinazomtaka.

Si tu Bayern Leverkusen, pia Borussia Dortmund inahusishwa na mpango wa kumpa nafasi Bundesliga. 

Nicolas Pepe (Ivory Coast)

Winga huyo alikuwa moto msimu uliopita wa Ligi Kuu ya Ufaransa ‘Ligue 1’, alichangia mabao 33 katika kikosi chake. Alifunga 22 na kutoa asisti 11, akiwa ameshuka dimbani mara 37.

Kwa nyota huyo mwenye umri wa miaka 23, huenda akaondoka Lille mapema zaidi, kwa maana ya kabla ya kuanza kwa fainali za Afcon 2019 kwani tayari Manchester City na Arsenal zinatoana nduki kuifukuzia saini yake.

Ikiwa atabaki Lille hadi kuanza kwa fainali za Afcon 2019, basi hiyo inaweza kuwa tiketi ya kurahisisha dili lake la kuondoka Lille na kujiunga na moja kati ya klabu kubwa katika ulimwengu wa soka.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles