Afariki Kisimani akimuokoa mbuzi kwa ujira wa Sh 6,000

0
1016

14594

Na MAKUNGA PETER, BUKOMBE

MKAZI wa Kijiji cha Kazibizyo Kata ya Ng’anzo, Wilayani Bukombe, Sebastian Lumbe (36), amefariki dunia kisimani alimoingia   kumuokoa mbuzi kwa ujira wa Sh 6,000.

Tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia jana katika Mtaa wa Misheni   baada ya mbuzi huyo kutumbukia kwenye kisima kinachodaiwa kuwa na urefu wa futi 30.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Misheni, Antony Kuya alithibitisha kutokea   tukio hilo.

Alisema baada ya mbuzi huyo kutumbukia kisimani, mmiliki wake, Marco Sylvester alitangaza ujira wa Sh 6,000 kwa mtu ambaye angefanikiwa kumtoa   na ndipo Lumbe alipojitolea kuingia kisimani humo.

Alisema kabla ya Lumbe kuingia kisimani humo na kukutwa na mauti, walijitokeza watu wawili tofauti lakini kila walipoingia waligundua kisima hicho kilikuwa kirefu.

Kwa sababu hiyo  walighairi  hadi alipofika yeye na kujitosa.

“Baada ya kuingia kisimani alianza kupiga kelele za kuomba msaada.

“Watu waliokuwa karibu na kisima hicho walimtupia kamba lakini wakati anajaribu kuivuta kupanda ilikatika na akaanguka kurudi kisimani.

“Baadaye kijana mmoja, Leonard Mathayo aliingia kujaribu kumuokoa lakini wakati akiwa humo ndani alisema baada ya kukaribia kufika mwisho wa shimo alimkuta akitupa miguu.

“Alipoanza kumfunga kamba ili wamvute  aliishiwa nguvu na kukosa hewa na hivyo ilimlazimu kuomba msaada kutoka nje,” alisema Kuya.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Mponjoli Mwabulambo aliwaonya wananchi kuwa waangalifu na visima virefu kama hivyo kwa sababu  ni hatari.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here