25.3 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 30, 2022

Contact us: [email protected]

Aeleza jinsi alivyomudu kuachana na dawa za kulevya

very-akiwa-na-mwanaeNA CHRISTINA GAULUHANGA, DAR ES SALAAM

WATU wengi wamekuwa wakiwatenga waathirika wa dawa za kulevya na kuona kama ni watu wasiofaa katika jamii.

Kuendelea kupuuzwa kwa kundi la watu hawa kulisababisha kila kukicha idadi ya watu wanaojihusisha na matumizi ya dawa za kulevya kuendelea kuongezeka.

Baada ya Serikali kuona nguvu kazi ya Taifa inazidi kupotea kwa sababu hii, iliamua kubuni mbinu mbalimbali kukabiliana nayo.

Serikali kwa kushirikiana na asasi mbalimbali zilianzisha mipango mikakati ya kutokomeza matumizi ya dawa za kulevya ili kupunguza athari za kiafya ndani ya jamii pamoja na maambukizi ya Ukimwi, ugonjwa wa ini na mengineyo.

Verry Kunambi (50), ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Mtandao wa wanaotumia dawa za kulevya (TANPUD), anasema naye ni miongoni mwa walioathirika na matumizi ya dawa za kulevya.

Anasema TANPUD ilianza mwaka 2011 ambapo mwaka 2015 ilipata usajili wa kudumu ambapo malengo makubwa ni utetezi wa watumiaji dawa za kulevya ili waweze kuthaminiwa na kupata huduma muhimu ndani ya jamii.

Kunambi anasema alisoma Shule ya Msingi Ilala Boma na baada ya hapo alijiunga na Sekondari ya Lomwe iliyopo Usangi, Kilimanjaro.

Anasema mwaka 1987 – 1991 alijiunga na ubaharia na ndipo alipoanza kutumia dawa za kulevya akiwa Iran baada ya kukutana na kundi la vijana wengi wakitumia dawa hizo.

Anasema wamezaliwa watoto sita ambapo yeye ni mtoto pekee wa kiume katika familia ya Theresphory Kunambi na Catheline Bruno.

Kunambi anasema mama yake mzazi alifariki mwaka 1985 wakati yeye akiwa bado hajaanza kutumia dawa za kulevya.

Anasema Februari mwaka 1991 alirejea nchini ambapo alikuwa na fedha nyingi na ndipo matumizi ya dawa za kulevya yalivyoongezeka na alienda tena Pakistan kuchukua dawa hizo huku akishirikiana na mtandao wa wafanyabiashara wakubwa.

“Nilijiunga na mtandao wa wafanyabiashara wakubwa wa ndani na nje ndipo nilipoenda zaidi ya mara mbili nje ya nchi kufuata mzigo,”anasema Kunambi.

Anasema mwaka 1998 aliishiwa fedha na ndipo alipojiingiza kwenye matumizi makubwa na kuanza kujidunga sindano.

“Katika kipindi hiki ndicho nilichokuwa nimezidiwa. Nilihama nyumbani kwa sababu familia yangu yote ilinitenga.

“Baba yangu alifuatilia nyendo zangu kwa karibu na kunipa ushauri mara kwa mara ili niachane na matumizi ya dawa hizo,”anasema Kunambi.

Anasema mwaka 2010 alipata elimu ya kuzuia dawa za kulevya na ilipofika mwaka 2011 alianza tiba katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), na mwaka 2013 alimaliza tiba na ndipo alipopelekwa shule kwa ajili ya kuongeza ujuzi wa kutoa elimu kwa wengine waweze kuachana na matumizi ya dawa hizo.

Kunambi anasema mwaka 2013 alimuoa Edna Kunambi na walibahatika kupata mtoto mmoja aitwaye Davis.

“Mke wangu alikuwa ni mlokole na kipindi chote cha uchumba alikuwa akifahamu kama mimi natumia dawa hizo na alikuwa akijitahidi kuniombea hadi Mungu alivyotoa kibali cha kuoana,” anasema Kunambi.

Kunambi anasema watumiaji wengi wa dawa za kulevya wanakumbana na changamoto ya kutengwa na jamii na kuonekana kama ni watu wasiofaa katika shughuli mbalimbali.

Anaishauri Serikali na jamii kwa ujumla kujitahidi kuendelea kuwapa ushauri na huduma za matibabu watumiaji wa dawa za kulevya ili waweze kuachana na matumizi hayo.

Anasema kuzidi kuwaacha wakihangaika peke yao kunazidi kuchangia ongezeko la matumizi hayo hapa nchini.

“Inasikitisha hadi leo kuna baadhi ya familia zimewatenga vijana wao kwa sababu tu eti wanatumia dawa za kulevya, jambo ambalo limekuwa likisababisha kundi hili kukosa elimu sahihi ya madhara ya matumizi ya dawa hizi na jinsi ya kujikinga,”anasema.

Anasema yeye binafsi alipokea ushauri kutoka kwa watu mbalimbali kuhusu kuachana na matumizi ya dawa hizo na anashukuru Mungu hadi alipofikia ameweza kupata mafanikio makubwa ikiwamo kuwa tegemeo la familia yao.

“Nakumbuka wakati nimeingia kwenye matumizi makubwa ya dawa za kulevya dada zangu walikuwa wakiumia mno kwa sababu ni mtoto pekee wa kiume. Hali ile nikikumbuka nasikitika mno na sihitaji irudie tena kwenye familia nyingine,” anasema Kunambi.

Pia anaishauri serikali itunge sheria kali kwa waagizaji wa dawa hizo kwakuwa wao ndiyo wachochezi wa matumizi hayo hapa nchini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
205,436FollowersFollow
558,000SubscribersSubscribe

Latest Articles