23.1 C
Dar es Salaam
Monday, September 25, 2023

Contact us: [email protected]

ADC: Hatuko tayari kujiunga na Ukawa

NA AZIZA MASOUD, TANGA
CHAMA cha siasa cha ADC, kimesema hakiwezi kujiunga na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kwa kuwa umoja huo una lengo la kuua vyama vidogo vya siasa.
Akizungumza katika viwanja vya Kwediboma wilayani Kilindi, mkoani Tanga juzi, Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho, Said Miraji, alisema Ukawa wana lengo la kuvidhoofisha vyama vidogo kupitia mpango wao wa kugawana majimbo kwa sera ya maeneo wanayokubalika.
“Ukawa wameonyesha udhaifu mkubwa wa kugawana majimbo kwa hoja ya kukubalika. Utaratibu huo ni mgumu kwa vyama vyetu vipya na kama tukiamua kujiunga nao tutakuwa tukivipa faida vyama vyenye nguvu.
“Sisi hatukubaliani na utaratibu huo kwa sababu huwezi kusema chama hakina nguvu katika uchaguzi wakati unajua chama hicho pia kinafanya kazi ya siasa kama vyama vikubwa.
“Kwa hiyo kama tutajiunga nao kwa kutumia vigezo vya kukubalika, tutashindwa kusimamisha wagombea pamoja na kukosa fursa ya kuendelea kujitangaza mikoani kupitia uchaguzi mkuu,” alisema Miraji.
Alisema ADC hadi sasa wana uhakika wa kushinda katika baadhi ya majimbo ya uchaguzi kisiwani Zanzibar na Pemba na kwamba masharti ya Ukawa yatasababisha wapoteze nafasi hizo kwa sababu hawatoweza kusimamisha wagombea.
“Kama watu mko makini, hamuwezi kujiunga Ukawa kwani kupitia utaratibu wao kuna baadhi ya vyama vitashuka umaarufu na vingine vitapata mafanikio makubwa,” alisema.
Ili vyama vya upinzani viweze kuiondoa CCM madarakani, Miraji alisema kuna haja viongozi wa vyama hivyo kuungana kwa kuvunja vyama vyao ili wakiunge mkono chama kimoja.
“Kama kutatokea makubaliano ya kuvunja vyama na kutumia jina la chama kimoja bila kuwa na uroho wa madaraka mimi nipo tayari kuachia uenyekiti wangu na sitotaka cheo ili tuiondoe CCM madarakani lakini kama mpango huo haupo, sitajiunga na Ukawa,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,717FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles