Adaiwa kumuua mkewe kwa kumkaba

0
403

Na Gurian Adolf-Sumbawanga

JESHI la Polisi mkoani Rukwa linamshikilia mwanaume mmoja mkazi wa Tarafa ya Kilyamatundu wilayani Sumbawanga kwa tuhuma za kumkaba hadi kumuua mke wake Namsonga Boniface (53) kutokana na kile kinachodaiwa kuwa ni mgogoro wa kifamilia.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Justine Masejo alisema kuwa tukio hilo lilitokea Mei 9, mwaka huu saa mbili asubuhi wakati wanandoa hao wakiwa nyumbani kwao.

Alisema kuwa kabla ya tukio hilo wanandoa hao walirudi nyumbani usiku wakiwa wametoka kilabuni kunywa pombe na kisha wakaingia ndani ya nyumba yao kulala.

“Asubuhi ya siku iliyofuata mmoja wa majirani hao alifika kwa lengo la kuwasalimia na kutaka kujua nini kilichotokea katika nyumba hiyo kwani nyakati za usiku alisikia wanandoa hao wakizungumza kwa kujibizana maneno makali.

“Baada ya kufika hapo na kugonga hodi, mtuhumiwa huyo aliitika, lakini hakutoka nje hali iliyomlazimu jirani huyo kusukuma mlango na kuingia ndani na alikuta mwili wa marehemu ukiwa umelala sakafuni. 

“Alipoona tukio hilo alitoa taarifa kwa uongozi wa Serikali ya kijiji ambao ulitoa taarifa polisi ndipo walipofika na kumkamata mtuhumiwa huyo,” alisema Kamanda Masejo. 

Alisema kuwa polisi bado wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo na watamfikisha mahakamani baada ya upelelezi kukamilika.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here