23.2 C
Dar es Salaam
Friday, June 9, 2023

Contact us: [email protected]

ACT  YAZIDI KUNG’ANG’ANIA ZILIPO TRIL 5.1/-

Na ELIZABETH HOMBO-DAR ES SALAAM


CHAMA cha ACT-Wazalendo  kimesema kimebaini udanganyifu wa Serikali katika ufafanuzi wa suala la Sh Trilioni 1.5  lililoibuliwa na Mbunge wa Kigoma Mjini kupitia chama hicho, Zitto Kabwe, baada ya kufanya uchambuzi wa ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG).

Katika uchambuzi wake wa ripoti hiyo ya CAG alioutoa wiki mbili zilizopita, Zitto alisisitiza inaonyesha fedha hizo Sh trilioni 1.5 kati ya Sh trilioni 25.3 za mapato yaliyokusanywa,   hazina nyaraka zinazothibitishwa katika matumizi ya Serikali.

Kutokana na hilo, Serikali ilitoa ufafanuzi kupitia Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Ashatu Kijaji ambaye alisema Sh bilioni 689.3 za mapato tarajiwa na Sh bilioni 203.9 ni mapato yaliyokusanywa kwa niaba ya Zanzibar.

Katibu wa Itikadi, Mawasiliano kwa Umma na Uenezi wa ACT- Wazalendo, Ado Shaibu alisema baada ya kuchunguza, wamebaini akaunti ya Zanzibar  na Hesabu za Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa mwaka unaoishia Juni 30 mwaka jana, hazionyeshi taarifa ya Sh bilioni 203 kupelekwa Zanzibar.

Alisema bajeti ya Zanzibar ya mwaka 2016/17 ilikuwa ni Sh bilioni 841.5 , Sh bilioni 482.4 kutoka katika vyanzo vya ndani, Sh bilioni  324.8 mapato ya nje, Sh bilioni 93.3 ruzuku, Sh bilioni 231 mikopo huku mkopo wa ndani ukiwa Sh bilioni 34.3.

“Mpaka  Juni 30, 2017 akaunti ya Zanzibar BoT ilikuwa na Sh bilioni 14 tu. Fedha za Zanzibar kwenye akaunti zake Benki Kuu (BOT) zinaweza kuonekana kwa urahisi kwenye Hesabu za Benki Kuu.

“Hesabu za BoT kwa mwaka unaoishia Juni 30, 2017 hazionyeshi uwepo hizo Sh bilioni 203.9 ambazo wanadai kuikusanyia SMZ.

“Hata wakati wa kufunga hesabu za BoT kwa mwaka 2016/17 fedha pekee zilizokuwa kwenye akaunti hiyo zilikuwa ni Sh bilioni 14.

“Hivyo si sahihi hata kidogo kwa taarifa ya Naibu Waziri Fedha kuonyesha kuwa kulikuwa na ‘transfer to Zanzibar’ kutoka makusanyo ya mapato ya Serikali ya Muungano,”alisema Shaibu.

Alisema ni vema Serikali ikajibu chanzo cha mapato ya kodi ya Sh bilioni 203.9 kwa kuwa fedha zilizokusanywa na TRA Zanzibar, zimeonyesha na SMZ kwenye Baraza la Wawakilishi Zanzibar kuwa zimekusanywa, kubaki na kutumika, hivyo hizo ambazo Serikali inadai kuikusanyia Zanzibar ni zipi?

“Fedha hizi zimekusanywa na kulipwa Zanzibar kupitia akaunti gani? Zanzibar wamepewa lini fedha hizi? Matumizi yake ni yapi kwa mujibu wa bajeti iliyopitishwa?

“Je utaratibu wa makusanyo ya Zanzibar umebadilika na sasa fedha za Zanzibar zinakaa Hazina ya Muungano? Kama umebadilika, ulibadilika lini na je, utaratibu mpya una ridhaa ya Baraza la Wawakilishi?

“Kwa taarifa ile ya Serikali bungeni, mpaka Juni 30, 2017, ni wazi kuwa SMT bado ilikuwa imezishikilia fedha za SMZ, ambazo kwa kawaida hutolewa kila mwezi   kuwezesha Zanzibar kujiendesha.

“Tukiamini kuwa huu ndiyo ukweli na kuwa Bunge halijadanganywa, basi ni dhahiri kuwa tunapaswa kuamini kuwa Serikali ya Zanzibar ilikuwa inajiendesha kwa miujiza, ikikusanya mapato hewa na kufanya matumizi ya kufikirika ya mishahara, ruzuku, pensheni kwa wazee na miradi ya maendeleo,”alisema.

Alisema Sh trilioni 1.5 ni karibu mara mbili ya bajeti ya Zanzibar, hivyo kupotea huku maelezo yake yakiwa hajaridhishi ni kuidharau Zanzibar.

“Vinginevyo ni wazi kwamba wanatengeneza kero mpya ya muungano wetu kwa SMT kuitupia madudu yake SMZ.

“Ni hadaa kwa umma, ni kutudharau Watanzania. Hatutakubali. Tutaendelea kuhoji ziliko Sh trilioni 1.5 zetu mpaka tujue ziliko,”alisema Shaibu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
213,351FollowersFollow
568,000SubscribersSubscribe

Latest Articles