32.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

ACT Wazalendo yaongeza muda fomu kwa wagombea

Mauwa Mohammed -Zanzibar

CHAMA cha ACT Wazalendo kimetangaza kuongeza muda wa uchukuaji fomu za kugombea nafasi za urais, ubunge, uwakilishi na udiwani hadi Julai 20 badala ya Julai 13 ya awali.

Hatua hiyo imetokana na kile kilichoelezwa hatua ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kufuta na kuanzisha majimbo mapya ya uchaguzi.

Hayo yalisemwa jana na Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad wakati wa ziara yake aliyoifanya ya kuhakiki uhai wa chama Shangani, Mkoa wa Kaskazini Unguja.

“Uamuzi huo umetokana na hatua ya kukatwa kwa baadhi ya majimbo na mengine kuongezwa,” alisema Maalim Seif.

Alisema hali hiyo imesababisha uchukuaji wa fomu za kugombea uongezwe ili kuwapa muda wale ambao majimbo yao yameathirika na mengine yamepunguzwa.

Maalim Seif alisema sasa kuna idadi ya majimbo 50 badala ya majimbo ya awali  yaliyokuwa 54 kwa Unguja na Pemba.

“Hatua hiyo ya kuongeza muda itawapa nafasi  wagombea kujipanga katika safu za kugombea katika majimbo yao,” alisema Maalim Seif.

Hata hivyo ameitaka ZEC na Tume ya Taifa Uchaguzi (NEC) kufanya uchaguzi wa huru na wa haki ili kila mmoja aweze kuridhika na uendeshwaji wa uchaguzi huo.

Maalim Seif alisema chama chake kimejizatiti na kiko tayari kwa uchaguzi, wanachosubiri ni tume itoe tamko la tarehe ya uchaguzi.

“Siku yeyote itakayotangazwa tupo tayari, tumejizatiti kwa uchaguzi,” alisema Maalim Seif.

Aidha Maalim Seif aliendeleza msisitizo wake wa kukemea rushwa na kudai kuwa yeyote atakayekwenda kinyume na agizo hilo basi amejiondoa mwenyewe.

“Hatupo tayari kuona mtu anaingia katika uongozi kwa kupitia njia ya rushwa, hatutolifumbia macho suala hilo,” alisema Maalim seif

Aidha aliwataka wanawake kuchukua nafasi za kugombea katika majimbo ili kuongeza uwakilishi wao katika vyombo vya uamuzi.

Awali Katibu wa Habari na Uenezi wa ACT Wazalendo, Salim Bimani, alivitaka vyama vingine vya upinzani kuzungumzia matatizo ya wananchi na kuacha hujuma dhidi ya chama chao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles