29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

ACT- Wazalendo yaishukia Serikali pembejeo za korosho

NA VERONICA ROMWALD

– DAR ES SALAAM

CHAMA cha ACT Wazalendo kimeshangazwa na kitendo cha Serikali kushindwa kutekeleza ahadi yake ya kugawa pembejeo za kilimo bure kwa wakulima wa korosho.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Katibu wa Kamati ya Itikadi, Mawasiliano ya Umma na Uenezi, Ado Shaibu, alisema Serikali inapaswa kutekeleza ahadi yake hiyo kabla wakulima hawajapata hasara kubwa.

“Mei mwaka huu, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Charles Tizeba mbele ya Waziri Mkuu, ambaye alikuwa mgeni rasmi, alitangaza uamuzi wa kugawa pembejeo bure kwa wakulima wote wa korosho kwenye kikao cha mwaka cha wadau wa zao hilo kilichofanyika Dodoma,” alisema.

Alisema kutangazwa   uamuzi huo kuliibua shangwe kubwa kwa wakulima wa korosho ambao walifurahia kupunguziwa mzigo wa kununua pembejeo.

“Kwa uamuzi huo, Serikali ilifuta mfumo wa pembejeo ya ruzuku.

“Awali mfumo huo ulikuwa ukiendeshwa na Vyama vya Msingi vya ushirika (Amcos) ambavyo vilikuwa vinakusanya fedha kwa wakulima wakati wa mauzo (Sh 15,000 tu kwa mfuko) za kununua pembejeo nje ya nchi na kugawa kwa wakulima,” alisema.

Alisema kwa uamuzi huo, AMCOS iliamuriwa kurejesha fedha kwa wakulima na   waagizaji binafsi wa pembejeo waliacha kuleta bidhaa hiyo nchini.

“Wakulima walizitumia fedha zao wakitumaini kuletewa pembejeo za bure, kinyume na ahadi ya serikali ya kuleta pembejeo ya bure ya kutosha na kwa wakati, hali imekuwa tofauti mno,” alisema.

“Je, Serikali ilikuwa na hakika au ilikuwa inafanya mzaha na siasa tu kwa ahadi yake hewa ya pembejeo za bure inayogharimu maisha ya wakulima.

“Je, Serikali ilifanya uchambuzi wa kina kuhusu mahitaji halisi ya pembejeo ya wakulima wa korosho nchini na uwezo wa Serikali au ilikurupuka tu,” alihoji.

Alisema Waziri Mkuu, Waziri wa Kilimo na Mwenyekiti wa Bodi ya Korosho walipohakikishia wakulima kuwa pembejeo itapatikana kwa wingi walimaanisha hiyo iliyokuja kwa kuchelewa, isiyo na ubora na iliyogawiwa kwa uchache au kuna nyingine inakuja?

“Serikali ilipovunja mfumo wa pembejeo ya ruzuku chini ya vyama vya msingi vya ushirika vya walikuwa ina nia njema na wakulima? Ni dhahiri imeshindwa kuwajali wakulima hawa na imeshindwa kuendesha uchumi wa nchi,” alisisitiza.

Alisema ni lazima Serikali itekeleze ahadi yake hiyo haraka kuwafikishia wakulima pembejeo kulingana na kiasi cha mahitaji.

“ Serikali ichukue hatua za dharura kuagiza pembejeo kuondoa uhaba wake, inunue pembejeo zote kutoka kwa wafanyabiashara binafsi na kuigawa bure kwa wananchi kama ilivyoahidi   au itoe ruzuku kuhakikisha   wakulima watanunua kwa bei ya Amcos ya 15,000 kwa mfuko mmoja,” alisema.

Alisema Serikali inapaswa kuwachukulia hatua kali za  sheria wauzaji wa pembejeo wanaopandisha bei ya pembejeo kila siku bila huruma.

“Ongezeko la sasa la hadi Sh 100,000 kwa mfuko mmoja wa sulphur halina utetezi wowote wa  biashara zaidi ya uchu wa kutumia uhaba wa pembejeo uliosababishwa na uzembe wa serikali kujitajirisha,” alisema na kuongeza:

“Serikali ichunguze ubora wa sulphur inayogawiwa ambayo inalalamikiwa na wakulima kuwa na ubora duni na ichukue hatua kali dhidi ya wafanyabiashara wanaolalamikiwa kuchanganya unga wa nafaka kwenye sulphur ili kujipatia faida maradufu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles