Na Kulwa Mzee, Dar es Salaam
CHAMA cha ACT-Wazalendo kimetangaza operesheni Majimaji katika majimbo 59 yaliyopo katika mikoa 19 nchini ikiwa na lengo la kukiwezesha kushinda katika Uchaguzi Mkuu wa udiwani, ubunge na Rais wa Oktoba 25 mwaka huu.
Operesheni hiyo ni moja ya maazimio ya kikao cha Kamati Kuu ya chama hicho iliyokutana Mei 23 na 24 mwaka huu chini ya Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo, Anna Mghwira na kiongozi wake, Zitto Kabwe.
Taarifa iliyolewa jana na Ofisa Habari wa ACT Wazalendo, Abdallah Khamis, ilieleza kuwa kikao hicho pia kilifanya uteuzi wa nafasi za manaibu katibu wakuu bara na Zanzibar.
“Kwa upande wa Naibu Katibu Mkuu Bara, Kamati Kuu imemteua Msafiri Mtemelwa ambaye ni mwanasiasa mzoefu katika siasa za Tanzania na kwa upande wa Zanzibar ameteuliwa Juma Said Sanani.
Khamis alisema kikao hicho kimefanya uteuzi wa makatibu mbalimbali ambako Peter Mwambuja (Fedha na Rasilimali), Habibu Mchange (Mipango na Mikakati), Richard Sabini (Mawasiliano na Uenezi).
Wengine ni Mohamed Masaga (Kampeni na Uchaguzi), Deus Chembo (Katiba na Sheria), Venance Msebo (Mambo ya Nje) na Gibson Kachinjwe (Katibu Kamati ya Maadili).
“Pia imemteua Estomih Mallah kuwa mwenyekiti wa Kamati ya Fedha na Rasilimali na Mwanasheria, Albert Msando, Mwenyekiti wa Kamati ya Katiba na Sheria. Japhari Kasisiko na Hamad Mussa Yusuph wakuteuliwa kuwa wajumbe wa Kamati Kuu,” alisema Khamis
Kutokana na hali ya siasa nchini, Kamati Kuu ya ACT-Wazalendo, imewateua Profesa Kitilla Mkumbo na Tery Bermunda (mama Tery) kuwa washauri wa Chama.