Na Nora Damiani, Mtanzania Digital
Chama cha ACT Wazalendo kimeitaka Serikali kuongeza nguvu katika kudhibiti taasisi za fedha zisizo rasmi ambazo zimekuwa zikiwafilisi wananchi mali kutokana na kuwakopesha kwa riba kubwa na kushindwa kulipa.
Akizungumza Januari 8,2024 jijini Dar es Salaam na waandishi wa habari, Waziri Mkuu Kivuli wa ACT Wazalendo, Isihaka Mchinjita, amesema wananchi wengi wamekuwa maskini kutokana na kufilisiwa mali zao kwa mikopo ya kausha damu.
Mchinjita alikuwa akitoa tathmini ya hali ya nchi kwa mwaka 2024 na mwelekeo wa Baraza Kivuli la ACT Wazalendo kwa mwaka 2025.
“Mwaka 2024 wananchi wengi waliokopa walishindwa kurudisha mikopo na kupoteza mali zao, tunaomba sekta hii isimamiwe vizuri,” amesema Mchinjita.
Waziri Mkuu huyo Kivuli pia ameitaka Serikali kuharakisha mchakato wa bima ya afya kwa wote kwa sababu baadhi ya wananchi wamekuwa wakishindwa kumudu gharama za matibabu na kusababisha kukosa huduma au kuzuiwa kutoka hospitali kutokana na kudaiwa hadi madeni.
Chama hicho kimesema kitatumia mwaka 2025 kusimamia haki za wananchi, uwajibikaji wa Serikali na kupigania mageuzi ya kweli ya kidemokrasia.