24.5 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

ACT Wazalendo mtihani Zanzibar

Grace Shitundu -Dar es salaam

CHAMA cha ACT Wazalendo ni kama kipo kwenye mtego unaowaweka njiapanda viongozi wa juu wa chama hicho baada ya kupewa nafasi ya kupeleka jina la Makamu wa kwanza wa Rais ili kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) visiwani Zanzibar.

Hali inatokea kutokana na chama hicho kutangaza kutokukubaliana na matokeo ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 28 mwaka huu na Rais Dk. Hussein Mwinyi kutangazwa mshindi wa kiti cha urais Zanzibar.

Dk. Mwinyi alitangazwa kushinda uchaguzi huo kwa kupata kura 380,402 sawa na asilimia 76.27 akifuatiwa na Maalim Seif Sharif Hamad wa chama cha ACT Wazalendo aliyepata kura 96,103 sawa na asilimia 19.87.

Matokeo hayo yanawapa nafasi ACT Wazalendo kuwa kuundaSerikali ya umoja wa kitaifa kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar iliyobadilishwa mwaka 2010 ambayo inaruhusu chama cha mgombea aliyepata kura zaidi ya asilimia 10 kuwa ndani ya serikali.

Wakati akitangaza baraza lake la mawaziri Rais Wa Zanzibar Dk. Mwinyi alisema kuwa ameshakiandikia chama hicho barua ya kutaka wapeleke jina la Makamu wa Kwanza wa Rais ili kuunda serikali kwa mujibu wa sheria.

Aidha Rais Mwinyi alisema pia ameacha nafasi mbili ya uwaziri kwa ajili ya kuwateua wawakilishi wa ACT Wazalendo watakaojisajili na kuapa katika Baraza la Wawakilishi.

Pamoja na kuunda baraza dogo la mawaziri Rais Mwinyi amekiachia chama ACT- Wazalendo Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda, na Wizara ya Afya Ustawi wa Jamii, Jinsia na Watoto .

Nafasi zote hizo baadhi ya wafuatiliaji wa siasa za Zanzibar wanaona ni mtego kwa ACT-Wazalendo licha ya kuwa  wanastahili kupewa kisheria, kutokana na chama hicho kutangaza kutotambua matokeo ya uchaguzi huo lakini pia viongozi wake na wafuasi wake wengi kupigwa na vyombo vya dola.

Viongozi wa ACT wazalendo walikataa matokeo ya uchaguzi visiwani humu kwa madai kuwa kulikuwa na figisufigisu katika mchakato mzima na kudai haukua huru na haki.

Endapo chama hicho kitakubali kuunda Seikali ya Umoja wa Kitaifa maana yake uamuzi huo utafuta kauli yao ya kutotambua matokeo yaliyomwingiza Dk. Mwinyi madarakani na hivyo kukubaliana na uchaguzi huo.

Vile vile wakikataa kushiriki katika serikali ya umoja wa Kitaifa watapoteza nafasi ya uwakilishi hasa kwa waliowapigia kura.

Msemaji wa ACT-Wazalendo kwa upande wa Zanzibar, Salim Bimani alipoulizwa kuhusiana na suala hilo zima alisisitiza kuwa bado hawajakutana kujadili suala hilo.

“Hili jambo ndio kwanza tumelipata  jana (juzi) bado hatujakaa vikao vya chama, tunatarajia hadi Jumatatu tutakuwa tumejua ratiba ya vikao vinakuwaje,” alisema

Mwenyekiti wa chama hicho ambaye pia alikuwa mgombea urais Zanzibar Maalim Seif akizungumza na gazeti moja la kila siku sio Mtanzania  juzi alisema ataheshimu maamuzi yoyote yatakayotolewa na chama chake.

Gazeti hili lilimtafuta kwa njia ya simu Kiongozi wa chama cha ACT Wazalendo Zitto Kabwe kutaka kupata taarifa za kina kuhusu suala hilo hatma ya wawakilishi na wabunge waliochaguliwa lakini hakupokea wala kujibu ujumbe mfupi wa maneno.

Hiki ni kipindi cha tatu tangu kuanziswa kwa mfumo wa  Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar ambapo 2010 Chama cha Wananchi CUF  kilifanikiwa kushika nafasi ya pili katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25 mwaka huo.

Katika uchaguzi huo aliyekuwa mgombea wa CCM Dk. Ali Mohamed Shein alifanikiwa kupata ushindi wa asilimia 50.1 ya kura zilizopigwa dhidi ya  aliyekuwa mpinzani wake Seif Sharrif Hamad wa chama cha upinzani CUF ambaye alipata asilia mia 49.1 ya kura zote.

Hivyo kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar iliyofanyiwa marekebisho 2010, Maalim Seif kupitia chama cha CUF alikuwa Makamu wa Kwanza wa Rais na pia wawakilishi wanne wa chama hicho walifanikiwa kusimamia wizara nne za serikali ya umoja wa kitaifa.

Waliokuwa mawaziri katika baraza lililoteuliwa na Dk Shein ni pamoja na Fatuma Ferej aliyeteuliwa katika Wizara ya Nchi, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Juma Duni Haji aliyesimamia Wizara ya Afya, Nassor Mazrui alipelekwa Wizara ya Viwanda na Biashara na Abubakari Khamis Bakary aliteuliwa kusimamia Wizara ya Katiba na Sheria.

Abubakari Khamis Bakary ambaye katika uchaguzi wa Oktoba 28, 2020 alikuwa ni mmoja wa wanachama wanne wa ACT-Wazalendo aliyeshinda uchaguzi huo kupitia jimbo la Pandani lakini alifariki dunia siku chache baada ya uchaguzi huo.

Kipindi cha pili cha uongozi wa Dk Shein, nafasi ya Makamu wa Kwanza wa Rais ilikuwa wazi kutokana na kilichokuwa chama kikuu cha upinzani CUF kususia uchaguzi wa marudio  baada ya uchaguzi wa mwanzo kufutwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC).

Vyama vingine vya upinzani vilivyoshiriki uchaguzi huo vilishindwa kufikisha zaidi ya asilimia 10 ya kura zilizopigwa.

Hata hivyo Rais Shein alimteua Hamadi Rashid Mohamedi wa chama cha ADC kuwa Waziri wa Kilimo na Said Soud Said wa chama cha AAFP kuwa Waziri asiye na wizara maalum.

Mfumo wa serikali ya Umoja wa Kitaifa visiwani Zanzibar uliundwa mwaka 2010 baada ya aliyekuwa Rais wa Zanzibar wakati huo Aman Abeid Karume na aliyekuwa Mwenyekiti wa CUF, Maalim Seif kufikia maridhiano ambayo yalipekelea kuitiwa kura ya maoni ya kutaka serikali ya umoja wa kitaifa.

Katika kura ya maoni iliyofanyika Julai 31 mwaka 2010 asilimia 66.4 ya Wazanzibar walipiga kura ya ndio kukubali kuundwa Serikali ya umoja wa kitaifa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles