27.2 C
Dar es Salaam
Thursday, November 7, 2024

Contact us: [email protected]

ACT watafuta wadhamini kwa mgombea urais kivuli

ACTNA SHABANI MATUTU, DAR ES SALAAM

CHAMA cha ACT –Wazalendo kimetuma timu ya viongozi wake kutafuta wadhamini wa mgombea urais ambaye hadi sasa hajapatikana.

Akizungumzia hilo jana kwa njia ya simu, Ofisa Habari wa chama hicho, Abdallah Khamis, alisema suala la mgombea urais kwa chama hicho bado lipo palepale na linatarajia kutatuliwa kwenye kikao cha Kamati Kuu.

“Kwa kuwa tunaamini kwamba lazima tusimamishe mgombea urais, imekuwa sababu kubwa kuanza safari za kuzunguka mikoani kumtafutia wadhamini.

“Wakati sisi tunaendelea na kazi ya kutafuta wadhamini, Kamati Kuu inaendelea na taratibu zake za kupitia jina linalofaa na kuliteua, kesho litafikishwa mbele ya Halmashauri Kuu na baadaye kupitishwa katika Mkutano Mkuu,” alisema.

Kuhusu kuchelewa kuwahi muda wa mwisho kwa mgombea kuchukua na kurejesha fomu Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), alisema chama hicho hakiwezi kuchelewa kutokana na umakini wanaoutumia katika kazi hiyo.

“Hadi wakati huu tunakaribia kumaliza kazi ya kutafuta wadhamini wa mgombea wetu, siwezi kukutajia ila tambua kwamba ni mgombea bora asiyekuwa na doa katika utendaji wake,” alisema Khamis.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Katibu wa Mipango na Mikakati wa chama hicho, Habibu Mchange, alisema chama hicho kina uwezo wa kujaza fomu hiyo asubuhi na kuirejesha jioni.

“Tunao uwezo wa kujaza fomu hiyo asubuhi na kuirejesha jioni ikiwa imekamilika bila ya kuwa na makosa yoyote,” alisema Mchange.

Kwa mujibu wa Mchange, chama hicho kimepata makada watatu waliojitokeza kuwania nafasi hiyo.

Chama cha ACT –Wazalendo kimejikuta katika wakati mgumu wa kutafuta mgombea urais baada ya aliyekuwa amependekezwa na Kamati Kuu, Profesa Kitila Mkumbo kukataa.

Hata hivyo taarifa kutoka kwa watu walio karibu na viongozi wa juu wa chama hicho, zinasema kwamba kuna mgawanyiko wa wazi juu ya ama kumuunga mkono mgombea urais wa Umoja wa Katiba ya Wananchi Ukawa kupitia Chadema, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa na jingine likitaka chama hicho kisimamishe mgombea wake.

Habari hizo zinasema baadhi ya viongozi wenye ushawishi mkubwa ndani ya chama hicho wamependekeza kumuunga mkono mgombea wa Ukawa ili kuweka nguvu ya pamoja kuiondoa CCM madarakani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles