24.1 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

ACT, Chadema, CCM vinachuana kukubalika kwenye jamii – Utafiti

 LEONARD MANG’OHA -DAR ES SALAAM 

WAKATI kampeni za Uchaguzi Mkuu zikishika kasi kwa vyama vya ACT Wazalendo, Chama cha Demokrasisa na Maendeleo (Chadema) na Chama Cha Mapinduzi (CCM), shirika liliso la kiserikali linalo jishughulisha na utafiti wa masuala ya kijamii (SSSRC), limetoa matokeo ya utafiti unaoonesha namna vyama hivyo vinavyochuana kwenye kukubalika kwa jamii. 

Akitoa matokeo ya utafiti huo katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa shirika hilo, Dk. Maximillian Makori, alisema utafiti huo umehusisha watu 1,876 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar. 

Dk. Makori alisema takwimu za utafiti huo zilipatikana kwa njia ya dodoso na mahojiano ya ana kwa ana na mahojiano kwa njia ya simu ambapo kwa Tanzania Bara watu 1,316 walihusishwa huku Zanzibar waliohojiwa wakiwa 560. 

“Utafiti huu ulijikita kujua mwenendo wa masuala ya kisiasa kwenye vyama vya kisiasa ikiwamo ACT-Wazalendo, CUF, Chadema, Chama cha Mapinduzi (CCM) na vyama vingine vyote vinavyoshiriki katika uchaguzi wa mwaka huu. 

“Tafiti zilifanyika sehemu mbalimbali nchini kwa kushirikisha makundi yote ya wapiga kura wakiwamo wazee, vijana, wanawake na wenye ulemavu waliopo mijini na vijijini na jumla ya mikoa 27 ilifikiwa. 

“Kundi la vijana lilijumuisha watu wenye umri kati ya miaka 18 hadi 35 na kundi la wazee lilijumuisha watu wenye umri zaidi ya miaka 60,” alisema Maximillian. 

Kuhusu matokeo ya utafiti huo alisema unaonesha chama cha ACT-Wazalendo ni chama kinachokuwa kwa kasi kuliko chama chochote nchini hasa upande wa Zanzibar huku umaarufu wa Chama cha Wananchi (CUF) ukiporomoka hasa visiwani humo. 

“Chama cha ACT kimeonesha kuimarika zaidi katika miaka mitatu ya hivi karibu na Chadema kuonekana kuwa ni chama kikuu cha upinzani kilicho imara licha ya misukosuko iliyopata ikiwamo kuondokewa kwa makatibu wake wakuu mahiri ndani ya kifupi cha miaka mitano,” alisema Makori. 

Pia alisema kwa upande wa vyama vya upinzani Chadema kinaonesha kuongoza katika kukubalika zaidi mijini na miongoni mwa watu wenye umri kati ya miaka 18 na 40 ikifuatiwa na ACT-Wazalendo. 

“Kwa ujumla miongoni mwa vyama vyote CCM inaongoza kukubalika na watu wa rika zote maeneo yote nchini. Miongoni vijana katika kundi la miaka 18 hadi 40, CCM inakubalika kwa asilimia 43, Chadema asilimia 42, ACT-Wazalendo asilimia 10 na vyama vingine vinakubalika kwa asilimia tano,”alisema. 

Dk. Makori alisema katika kundi la wazee wenye umri zaidi ya miaka 55, CCM inakubalika kwa asilimia 59, Chadema asilimia 35, ACT asilimia saba na vyama vingine asilimia mbili. 

Kuhusu kukubalika kwa vyama kimaeneo, utafiti huo unaonesha wagombea wa vyama vingine ukitoa CCM, Chadema wanakubalika zaidi mijini kuliko vijijini. 

Ulionyesha pia kuwa mgombea wa CCM Dk. John Magufuli anakubalika kwa asilimia 83 vijijini na asilimia 73.1 mijini akifuatiwa na Tundu Lissu (Chadema) anayekubalika kwa asilimia 13 vijijini na asilimia 20 mijini. 

Pia ulionyesha wagombea wa vyama vingine wanakubalika kwa asilimia moja hadi tatu vijijini na moja hadi nne mijini. 

Utafuti huo unaonesha CCM inakubalika kwa asilimia 79.9 kwa wanawake na asilimia 58 kwa wanaume, Chadema inakubalika miongoni mwa wanaume kwa asilimia 34 na asilimia 17 kwa wanawake, ACT-Wazalendo inakubalika kwa asilimia tatu kwa wanawake na asilimia saba kwa wanaume huku vyama vingine vikiambulia chini ya asilimia moja kwa wanawake na wanaume. 

“Hivyo basi endapo uchaguzi ungefanyika leo (jana), mgombea urais kwa tiketi ya CCM Dk. John Magufuli, atashinda kwa asilimia 81.3, akifuatiwa na mgombea uraisi kwa tiketi ya Chadema Tundu Lissu kwa asilimia 14.7, Bernard Membe asilimia tatu, Lipumba asilimia moja na wagombea wengine asilimia 0.5,” alisema Dk. Makori. 

Mtafiti Mwandamini wa SSSRC, Peter Kasera, alizitaja baadhi wa sababu zilizotolewa na wananchi walihojiwa kuhusu kumuunga mkono Dk. Magufuli kuwa uchapa kazi wake katika kuboresha miundombinu, kudhibiti matumizi mabaya ya Serikali, kupambana na rushwa na kurudisha nidhamu kazini. 

Kuhusu wale wanaomuunga mkono Lissu alisema sababu walizozitoa zilihusisha uwezo wake wa kujenga hoja na kuhurumiwa kutokana na kupigwa kwake risasi. 

“Vile vile katika utafiti huu ilibainika kuwa zoezi la kuboresha daftari la wapiga kura lilifanikiwa kwa kiasi kikubwa. Asilimia 98 ya wahojiwa walisema kwamba taarifa zao ziko sahihi na wengine walifanikiwa kuhamisha na kuhakiki taarifa zao na zikovizuri sasa. 

“Pamoja na kujiandikisha kupiga kura asilimia 99.4 ya wananchi walisema wamejiandikisha na wanadhamiria kupiga kura katika uchaguzi wa mwaka huu,”alisema. 

Pia Kasera alisema wananchi waliorodhesha changamoto kuu wanazoziona nchini kuwa ni pamoja na huduma za afya, maji safi na salama na ajira kwa vijana ingawa walisema zimepungua kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na awamu zilizopita. 

“Upande wa miundombinu walisema changamoto katika awamu hii zimepungua kwa zaidi ya asilimia 72, vivyo hivyo kwenye huduma za afya changamoto zimepungua kwa kiasi kikubwa na pia katika mapambano za kupunguza umasikini juhudi kubwa zimeonekana,” alisema Kasera. 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles