Na BENJAMIN MASESE-MWANZA
WATU wawili wamefariki dunia jijini Mwanza kwa matukio tofauti yakiwamo ya wizi wa kuku na kujinyonga, huku wengine watatu wakishikiliwa na Jeshi la Polisi kwa kosa la kukutwa na dawa za kulevya (heroin) pamoja na bangi.
Akizungumza na waandishi wa habari juzi, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Zarau Mpangule, alisema tukio la kwanza lilitokea juzi saa 12 alfajiri Mtaa wa Kitangiri wilayani Ilemela, mtu mmoja aliyejulikana kwa jina la Kulwa Mabula (37), mkazi wa mtaa huo alijinyonga hadi kufa kwa kutumia kamba ya manila aliyokuwa ameifunga kwenye mti kando ya barabara ya Kitangiri.
Inadaiwa kuwa marehemu alikuwa na mgogoro wa muda mrefu wa kimapenzi na mtu aliyekuwa na mahusiano naye ndipo tarehe tajwa hapo juu aliamua kujitoa uhai.
Kamanda Mpangule alisema wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo na mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando kwa uchunguzi.
Katika tukio la pili, Kamanda Mpangule alisema mtu mmoja ambaye hakufahamika jina wala makazi yake mwenye umri kati ya miaka 25 na 30, aliuawa na kundi la wananchi katika Kijiji cha Mwanangwa Kata ya Mabuki Wilaya ya Misungwi kwa tuhuma za kuiba kuku wawili.
Kamanda alisema kundi hilo la watu ambao walijichukulia sheria mkononi, lilimpiga fimbo, mawe na baadaye kumchoma moto hadi kufariki dunia.
Kamanda Mpangule alisema kutokana na mauaji hayo, polisi wanawashikilia watu watano kwa mahojiano zaidi na watafikishwa mahakamani baada ya upelelezi kukamilika.
Wakati huo huo, watu watatu wanashikiliwa na jeshi hilo kwa makosa ya kukutwa na bhangi na heroine Mtaa wa Sabasaba wilayani Ilemela.