26.1 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Acha kuruhusu SmartPhone ikuendeshe

id157535

Na FARAJA MASINDE,

UTANDAWAZI unaendelea kuchukua nafasi na kila mtu anataka kuonekana mjuzi wa kutumia SmartPhone, kuonekana hodari kwenye kuchukua matukio, kupiga picha na mambo mengine mengi.

Hata hivyo dhamira hiyo ya kusaka uhodari na kutaka kuwa mstari wa mbele kuwahi kuchukua matukio inaendelea kuwa mwiba kwa wengi.

Ni kweli kwamba wengi wanachukua matukio mbalimbali kwa nia njema kabisa ya kubaki na kumbukumbu kwenye simu zao lakini hata hivyo wamekuwa wakisambaza picha hizo hasa za video bila kujua na kujikuta wakisababisha madhara kwa wenzao.

Nguvu ya kuandika makala hii leo inatokana na kuwapo kwa mfululizo wa matukio mengi ambayo yamekuwa yakiibuliwa kupitia mitandao ya kijamii.

Miongoni mwa matukio hayo ni lile la wiki chache zilizopita ambalo lilitokea mkoani Mbeya likiwahusisha walimu waliokuwa kwenye mafunzo ambao walimuadhibu bila huruma mwanafunzi, Sebastian Senguku bila kujua kuwa walikuwa wakirekodiwa kupitia Smartphone.

Acha hilo, tukio lingine ni lile la askari wa usalama barabarani ambaye alikuwa akiomba rushwa kwa raia mmoja wa kigeni huko Visiwani Zanzibar bila kujua kuwa alikuwa akichukuliwa video kupitia SmartPhone.

Wahusika wa matukio yote haya wamejikuta wakiadhibiwa kwa kufutwa kazi huku walimu hao wakifutwa vyuo.

Kama wewe unatumia simu hizi za kisasa acha kabisa mchezo wa kumuamini kila mtu kwa maana ya kwamba usiruhusu mtu akuchukue video huku ukifanya vitu vya kijinga na visivyopendeza kinyume na maadili.

Wala usikubali kumtumia mtu yeyote video za mambo yako ya siri kwani huwezi kujua anakuchuuliaje au yeye ataifanyaje kwani mambo yamebadilika sana maamuzi yanachukuliwa papo hapo.

Hivyo usiruhusu kabisa teknolojia ikuendeshe bali kubali kuiendesha, acha kuamini kila mtu.

Haijalishi ni mtumishi wa umma au mtu wa namna gani jambo la msingi ni kuwa na nidhamu na simu yako, kamwe usiiruhusu ikutese ama kukutia matatani.

Kama huna kitu cha kuposti ni bora ukakaa kimya hata kama uko kwenye kundi la namna gani kwani hakuna aliyetunukiwa tuzo kwa kuweka video au picha nyingi kwenye mitandao ya kijamii.

Hivyo mnaotumia Smartphone hamna budi kutambua kuwa mambo yamebadilika kwani ukisema unashirikishana na rafiki yako aliyeko Mtwara video inayokiuka maadili kwa kuamini kuwa ni nyie tu wawili itakutokea puani, vitu vinasambaa kama upepo.

Lazima mjue kuwa mitandao hii kwasasa ina wadadisi wa kila namna na watu wengi wamejikuta wakiathirika kisaikolojia kutokana tu na simu hizi za smartphone.

0653045474

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles