24.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

ACACIA YAKUBALI KULIPA ZAIDI

Na MWANDISHI WETU

KUTOKANA na hatua ya hivi karibuni ya kuhuisha sheria zinazosimamia sekta ya madini nchini, Kampuni ya Uchimbaji Dhahabu ya Acacia sasa imetangaza kuongeza kiwango cha malipo ya mrabaha kutoka asilimia nne hadi sita.

Katika taarifa yake kwa umma jana, Kampuni hiyo imesema imechukua hatua hiyo ili kukidhi matakwa ya marekebisho hayo ya Serikali na kupunguza vikwazo kwa uendeshaji wa biashara zake.

Imesema imeongeza kiwango hicho cha mrabaha unaolipwa  katika madini ya dhahabu, shaba na fedha.

“Acacia imeona katika Gazeti la Serikali kumechapishwa sheria mpya zitakazokuwa zinaongoza uendeshaji wa rasilimali za nchi ya Tanzania. Sheria hiyo mpya ambayo imefanya marekebisho ya Sheria ya Madini ya mwaka 2010, sasa ndiyo inayotumika na mamlaka za Tanzania.

“Ili kupunguza usumbufu kwa uendeshaji wa Kampuni tutachukua hatua za muda, kuzingatia matakwa yote ya sheria mpya, kama kuongeza kiwango cha malipo ya mrabaha kwa vito vyote,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

Taarifa hiyo ilisema, kiwango hicho kinajumuisha asilimia moja ambayo sasa inatozwa kama ada ya kusafirisha mizigo nje ya nchi (clearing fee on exports).

Hivi karibuni Bunge lilipitisha miswada mitatu kwa hati ya dharura iliyohusu pamoja na mambo mengine, kurekebisha sheria za madini ili Taifa liweze kulipwa mrabaha wa haki kutoka kwa makampuni ya madini.

Taarifa ya Acacia imekuja siku chache baada ya mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Kampuni hiyo, Balozi Juma Mwapachu, kutangaza kustaafu nafasi hiyo, baada ya kuitumikia kwa vipindi viwili.

Mwapachu alitangaza uamuzi huo juzi, baada ya muhula wake wa pili wa miaka mitatu mitatu wa ujumbe wa bodi hiyo kumalizika.

Juni 12, mwaka huu, Rais Dk. John Magufuli alikabidhiwa ripoti ya pili ya mchanga wa madini iliyowasilishwa na Mwenyekiti wa tume hiyo, Profesa Nehemiah Osoro.

Kutokana na hali hiyo, Kampuni ya Acacia ilieleza imesikitishwa na kushangazwa na matokeo ya ripoti hiyo aliyokabidhiwa Rais Magufuli.

Taarifa iliyotolewa na Acacia   kupitia tovuti yake, saa chache baada ya ripoti hiyo kusomwa na Mwenyekiti wa tume hiyo, Profesa Osoro, ilisema Kampuni hiyo imesikitishwa na ripoti ya kamati ambayo ni historia katika uchumi wa nchi hii na mambo ya sheria ya kusafirisha mchanga wa madini.

Kwa mujibu Acacia, ripoti ya pili imejikita katika matokeo ya ripoti ya kwanza iliyotolewa Mei 24, mwaka huu, ambayo kampuni hiyo imekuwa ikiipinga vikali.

Taarifa hiyo inasema ripoti hiyo ilihusisha matokeo ya sampuli za makotena 44.

Pia Acacia ilisema kwa taarifa zake za miaka zaidi ya 20 ni vigumu kupatanisha matokeo hayo, ambayo yametaja kiwango kikubwa cha thamani ya zaidi ya mara 10.

Kwa mujibu wa ripoti iliyowasilishwa na kamati ya pili,   Acacia haijawahi kutangaza mapato na kulipa kodi kwa kipindi cha miaka mingi ambayo ni mabilioni ya dola za Marekani.

Ripoti ya pili inaishutumu Acacia kutoonyesha mapato halisi pamoja kutolipa kodi ya mabilioni ya dola za Marekani.

Kwa matokeo hayo, kamati hiyo imetoa mapendekezo ya kuitaka Acacia ilipe kiasi chote cha kodi inachodaiwa, kufanya mazungumzo ya makubaliano ya uchimbaji wa madini, umiliki wa Serikali katika migodi na mwendelezo wa kupiga marufuku usafirishaji nje   mchanga wa madini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles