31.8 C
Dar es Salaam
Thursday, November 14, 2024

Contact us: [email protected]

Aboud Jumbe ni Gorbachev wa Zanzibar

Marehemu Aboud Jumbe Mwinyi
Marehemu Aboud Jumbe Mwinyi

NA BALINAGWE MWAMBUNGU,

NILIKUWA Mwandishi wa kwanza kuandika habari za Baraza la Wawakilishi Zanzibar nikiyawakilisha magazeti ya Daily/Sunday News Januari mwaka 1979.

Namfananisha Aboud Jumbe Mwinyi na  aliyekuwa Rais wa Urusi (1990 – 1991), Mikhail Gorbachev, mwanzilishi wa sera ya ‘Glasnost (sera ya uwazi) na Perestroika—mfumo mpya wa kisiasa na kiuchumi.

Gorbachiev alipojaribu kuleta sera hiyo, alipingwa vikali na wahafidhina ambao walizoea kuhodhi madaraka na upangaji wa mambo ya biashara, uchumi na kuikandamiza demokrasia.

Pamoja na Jeshi la Urusi kumpindua na kumweka kizuizini, Gorbachev alirejeshwa madarakani kwa nguvu ya wananchi ambao walifanya maandamano ya kumunga mkono.

Jumbe aliteuliwa kushika nafasi ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Wawakilishi, baada ya kuuawa kwa Rais Abeid Amani Karume, mnamo Aprili, 1972.

Alianza kuonesha nia ya mabadiliko mara alipoingia madarakani kwa kuachana na siasa na sera za mabavu za mtangulizi wake na kuwafanya wananchi wa Zanzibar waanze kupumua na kujisikia huru zaidi.

Rais Jumbe ndiye aliyeleta Katiba ya Zanzibar (1979) baada ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964, Katiba ambayo ilitenganisha madaraka ya Baraza la Mapinduzi na Baraza la Wawakilishi.

Jumbe akiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, alizindua kwa mara ya kwanza, Baraza la Wawakilishi na kufungua milango ya uhuru kwa Wazanzibari ambapo mtangulizi wake Karume, alitawala kwa Amri (Decree) za Baraza la Mapinduzi na kulikuwa hakuna mwenye ubavu wa kuhoji.

Kabla ya kuwa Rais, Jumbe, alikuwa mmoja wa wanasiasa wakongwe na alishika nafasi mbalimbali za uongozi ikiwa ni pamoja na ile ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar baada ya Khasim Hanga, aliyekuwa anashikilia wadhifa huo, kupotea katika mazingira tatanishi.

Wakati wa mauaji ya Karume, Jumbe alikuwa ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais (Muungano).

Baada ya uchaguzi wa kwanza wa Zanzibar 1985, Jumbe alichaguliwa na kuhalalishwa kuwa Rais wa Zanzibar, wadhifa ambao pia ulimpa nafasi ya kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na Mwenyekiti wa Afro-Shirazi Party (ASP).

Kwa nyadhifa hizo na kufuatana na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, moja kwa moja akawa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano.

Kwa ufupi Jumbe, ambaye aliaminiwa sana na Rais wa kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere hata kumtuma kumwakilisha kwenye mikutano ya kimataifa, alikwaa kisiki na kumtibua nyongo Nyerere alipoanza kujihusisha zaidi na masuala ya dini.

Nyerere alikuwa anapinga jambo hili kwamba viongozi wa juu wa Serikali wasijihusishe na mambo hayo kwa kuwa Katiba inatamka kwamba Serikali haina dini.

Baada ya kuviunganisha vyama vya ASP na TANU (Tanganyika African National Union), Jumbe kwa nafasi yake ya Rais wa Zanzibar, pia akawa Makamu wa Mwenyekiti wa CCM Taifa, lakini mnamo mwaka 1984, katika kile kilichoitwa na CCM, uchafuzi wa kisiasa wa hali ya hewa Zanzibar, alilazimishwa kujivua nyadhifa zote katika Chama na Serikali. Kosa lake kubwa ni kuhoji muundo wa Muungano.

Hadi anafariki dunia, Mzee Jumbe, ambaye baada ya kuvuliwa uongozi, hakuruhusiwa kurudi Zanzibar, alikuwa muumini wa Serikali Tatu na maandishi yake yanadhihirisha hivyo.

Alitengeneza mashitaka akisaidiwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Bashir K. Swanzy, raia wa Ghana na kutaka kuyapeleka kwenye Mahakama ya Katiba kama inavyotamkwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano, akionesha kuwa 1+! = 3. Mantiki yake ikiwa: ni kuna nchi huru mbili zilizoamua kuungana, zikazaa nchi inaitwa Tanzania—Zanzibar ipo, inaonekana, mbona Tanganyika haipo, iko wapi? Kiurahisi ni kwamba mke na mume wanapoana, wakizaa mtoto, familia ina kuwa ya watu watatu! Hati ile ya mashtaka haikuona mwanga, ilipotea na kutua mezani kwa Rais Nyerere.

Aidha, kama ule upotevu wa document ya Mashitaka haukutosha, Mzee Jumbe akaandika barua kwenda kwa Mwalimu Nyerere akionyesha kuwa Mkataba wa Muungano na Sheria ya Muungano, vilikuwa vimekiukwa na akataka pia vyama vilivyokuiwa vinatawala kabla ya Muungano, yaani TANU na ASP virudi—kila kimoja upande wake. Hii ilitafsiriwa kwamba Alhaj Aboud Jumbe alikuwa na nia ya kuvunja Muungano.

Barua hiyo, kama ile Hati ya mashitaka, iliibiwa mezani kwa Rais wa Zanzibar na kumfikia Mwalimu Nyerere. Mizengwe na mikwara iliyofuata kwenye Halmashauri Kuu ya CCM, hatimaye ikamwondoa Mzee Jumbe katika ulingo wa siasa Tanzania.

Suala la glasnost na perestroika lilipoibuka ndani ya CCM na Wajumbe wa Baraza la Katiba, kidogo wakabane makoo upande mmoja ulipohoji Mkataba wa Muungano na Sheri ya Muungano—mambo ambayo alihoji Mzee Jumbe mwaka 1984.

Wakati wa kutafuta maoni kupitia Tume ya Jaji Joseph Sinde Warioba, viongozi karibu wote kutoka Zanzibar na taasisi zake, walipendekeza kubadilika kwa Muungano kuwa Serikali Tatu kama ilivyokusudiwa katika hati ya Muungano, yaani kuwe na Serikali ya Tanganyika yenye madaraka kamili na kuwe na Serikali ya Zanzibar yenye madaraka kamili. Juu ya serikali hizi mbili iwepo Serikali ya Muungano wa Tanzania.

Wajumbe wa Baraza la Katiba kutoka Zanzibar, ambao walijiapiza kwamba safari hii hawatakubali kuondoka Dodoma na kurudi Zanzibar bila Zanzibar yao. Wakasema Zanzibar inazidi kupotea kwa kuwa mambo mengi ambayo hayakuwa ya Muungano, yameongezwa kinyemela na ndio yanachangia kuidhoofisha Zanzibar. Kwenye Hati ya Muungano kulikuwa na mambo 11 tu na ndio waliyotaka yabaki, walitaka mengine 15 yaliyoongezwa yaondolewe.

Cha kushangaza ni kwamba, walipofika Dodoma hali ya hewa na hoja madhubuti za upinzani ambao walitaka Serikali Tatu vikawachanganya, wajumbe wa CCM kwenye Baraza la Katiba, ikiwa ni pamoja na wajumbe waliojiapiza wakati wanaenda Dodoma kwamba safari hii hawatakubali kuburuzwa na Bara, sauti zao zikafifia na mwisho kupotea kabisa.

Miguu yao ikaota matende, wakashindwa kuandamana kama walivyofanya Warusi, kumwunga mkono Rais wao Gorbachev, wakashindwa hata kutaja jina la Aboud Jumbe kwenye hotuba zao!

Hii ilitokana na ukweli kwamba wajumbe kutoka Zanzibar, wangekomalia hoja ya Serikali Tatu kama ilivyopendekezwa na Tume ya Warioba, wangeonekana kwamba wanaungana na wapinzani na CCM ingeangamia.

Ikumbukwe kwamba mwaka huo ulikuwa wa Uchaguzi Mkuu na kisiasa Chama Cha Mapinduzi kilikuwa hakiko vizuri. Kulikuwa na dalili zote za kukipoteza kama kilivyopotea katika duru za siasa chama kilichokuwa kinatawala nchini Kenya—Kenya African National Union.

Alhaj Mzee Aboud Jumbe Mwinyi, ameaga dunia akiwa na umri mkubwa wa miaka 96 akiwa amepanda mbegu ya mageuzi na demokrasia, japo ameondoka bila kuyaona matunda ya harakati zake, tofauti na Nelson Mandela wa Afrika Kusini ambaye ameiacha nchi yake ikiwa huru na imeondokana na siasa chafu ya ubaguzi wa rangi, historia itamdhirisha kwamba alipigania haki ya Wazanzibari.

Adieu Mzee Jumbe.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles