Oscar Assenga, Tanga
Abiria 52 akiwamo dereva wamenusufika kifo baada ya basi walilokuwa wamepanda la Kampuni ya Kilimanjaro linalofanya safari kati ya jiji la Dar es Salaam na Arusha kuacha njia na kupinduka.
Basi hilo lilikuwa likitokea mkoani Arusha kwenda Jijini Dar limepinduka saa 09:20 mchana, eneo la Mkata wilayani handeni mkoani Tanga, kutokana na hali ya hewa.
Akizungumza na Mtanzania Digital leo Mei 5, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Edward Bukombe, amesema katika ajali hiyo majeruhi ni 18 ambao sita kati ya hao wamepata majeraha makubwa na kulazimika kupelekwa
kwenye kituo cha Afya cha Mkata kwa ajili ya matibabu zaidi.
“Kati ya majeruhi hao wanawake ni 15 na wanaume ni watatu, niwatake madereva kuhakikisha mnachukua tahadhari kwenye kipindi hiki cha mvua kutokana na kuwepo kwa utekelezi kwenye barabara,”amesema.
Hata hivyo amewataka madereva pia kuhakikisha wanazingatia sheria za
usalama barabarani, kuacha kuendesha basi mwendokasi ambao unaweza kusababisha abiria kupoteza maisha wawapo safarini.
Aidha Kamanda huyo amesema hali ya dereva wa basi hilo ambaye jina lake halikupatikana bado ni mbaya.