24.8 C
Dar es Salaam
Friday, October 4, 2024

Contact us: [email protected]

Abiria wanaosafiri kwenda mikoani wasota Dar


LEONARD MANG’OHA, DAR ES SALAAM

ABIRIA wanaosafiri kutoka Dar es Salaam kwenda mikoa mbalimbali kwa mapumziko na sikukuu za mwisho wa mwaka wamekumbana na adha ya ukosefu wa usafiri kutokana na upungufu wa mabasi.

MTANZANIA Jumapili lilishuhudia idadi kubwa ya abiria katika Kituo Kikuu cha Mabasi cha Ubungo Dar es Salaam (UBT) wakiwa hawajui cha kufanya baada ya kukosa uhakika wa usafiri kutokana na mabasi kujaa.

Idadi kubwa ya watu ilifurika katika ofisi mbalimbali za kukatia tiketi hususani kwa mabasi yanayokwenda mikoa ya Kanda ya Ziwa, huku mabasi madogo yanayofanya safari katikati ya jiji yakiruhusiwa kusafirisha abiria kwenda Arusha na Kilimanjaro.

Mabasi hayo ni pamoja na lenye namba za usajili T 192 DPF ambalo hutoa huduma kati ya Temeke na Mbezi na lenye namba T 232 DKK ambalo hufanya safari kati ya Makumbusho na Kibamba Shule.

Licha ya mabasi hayo kupewa vibali vya muda, yalilalamikiwa na abiria waliokuwa kituoni hapo kuwa yanatoza viwango vikubwa vya nauli tofauti na vile vilivyoelekezwa na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra).

Mmoja wa makondakta wa mabasi hayo ambaye alikataa jina lake lisiandikwe gazetini, alisema wanalazimika kuongeza nauli hizo ili kumudu gharama kubwa za mafuta wanayotumia kwenda huko.

“Hili gari kila siku likiwa hapa mjini tajiri anataka hesabu yake shilingi 200,000, sasa ili umshawishi aruhusu gari lake liende Moshi au Arusha, lazima umpe uhakika wa kumletea hesabu ya siku mbili kisha upate mafuta ya kwenda na kurudi ndiyo maana tunaongeza kidogo nauli,” alisema kondakta huyo.

Hali hiyo pia ililalamikiwa na baadhi ya abiria waliokuwa wakisafiri kwenda Dodoma ambao baadhi walidai kutozwa nauli hadi Sh 30,000 kutoka Sh 20,000.

Mmoja wa abiria, Nicolaus Chitembele, alidai alifika kituoni hapo saa 12:00 asubuhi kwa lengo la kusafiri kwenda Gairo mkoani Morogoro, lakini alijikuta akisubiri hadi saa nne asubuhi bila kujua hatima ya safari yake.

“Hakuna gari za kwenda Dodoma kwa sababu kila unakokwenda unaambiwa zimejaa, nimejaribu kutafuta gari ya Morogoro walau nikapande gari jingine kule pia imeshindikana. Kibaya zaidi hata nauli wamepandisha, kwa mfano Gairo kawaida tunakwenda kwa shilingi 15,000, leo (jana) wanataka hadi 30,000,” alisema Chitembele.

Pia hali kama hiyo imeshuhudiwa katika ofisi za mabasi yanayokwenda Kanda ya Ziwa na mikoa ya katikati ya nchi ambako hadi saa tatu asubuhi hakukuwa na nafasi katika mabasi yanayokwenda huko siku iliyofuata.

Wakati huo huo, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Ramadhan Kailima, alidai kushuhudia madudu katika ukaguzi wa mabasi uliofanyika jana alfajiri kituoni hapo.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni ya Nenda Salama Barabarani inayoratibiwa na taasisi isiyo ya kiserikali ya Mabalozi wa Usalama Barabarani (RSA) iliyofanyika kituoni hapo jana, Kailima alisema katika ukaguzi huo ulioanza jana saa 11 alfajiri, mabasi 12 yalibainika kuwa na hitilafu.

Alisema baadhi ya mabasi hayo yalibainika kutokuwa na mikanda ya usalama kwa abiria, huku mengine mawili yakibainika kutokuwa na sifa za kuendelea na safari na kulazimika kuyazuia.

Kailima alisema pamoja na baadhi ya mabasi kubainika kuwa na hitilafu, mengine yamebainika kukiuka sheria kwa kuwauzia abiria tiketi kwa bei ya juu tofauti na zile zilizopangwa na Sumatra.

“Kuna basi tumekuta halina mikanda ya usalama, basi jingine halina bima, mengine yamezidisha bei za tiketi na kibaya zaidi basi jingine unakuta abiria wamekatiwa tiketi si la basi husika.

“Moja ya kazi za Serikali ni kulinda usalama wa raia na mali zao, jukumu ambalo limekabidhiwa Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani. Lakini suala hili haliwezi kufanikiwa kama mdhibiti mkuu ambaye ni mwananchi mwenyewe ataona mambo na kukaa kimya,” alisema Kailima.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles