Na Mathew Kwembe – Dar es Salaam
ABIRIA wanaotumia mabasi yaendayo haraka katika Barabara ya Morogoro wamefikia 200,000 kutoka 50,000 kwa siku, hivyo kuchangia kupunguza msongamano wa magari katika njia hiyo.
Akizungumza baada ya kutembelea Kituo Kikuu cha Kimara Mwisho kama sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi Yaendao Haraka (DART), Mhandisi Ronald Rwakatare, alisema idadi hiyo ya abiria ni moja ya mafaniko ambayo imepata mradi huo ambao ulianza rasmi mwaka jana.
“Mradi huu umeweza kuokoa muda wa wananchi ambao kabla ya mradi kuanza walikuwa wakitumia usafiri mwingine uliokuwa ukichukua hadi saa mbili, wakati sasa wanatumia dakika 45 tu kwa safari ya kutoka Kimara hadi Posta kwa kutumia mabasi yaendayo haraka,” alisema Mhandisi Rwakatare.
Alifafanua mabasi hayo mbali na kuwapunguzia mzigo wa nauli watumiaji wa kawaida wa mabasi ya daladala, mradi wa mabasi yaendayo haraka umeokoa gharama ya usafiri kwa wenye magari binafsi ambao wengi wao wamekuwa wakiutumia zaidi usafiri huo.
“Watumishi wa Wakala wa Mabasi yaendayo haraka wamekuwapo katika vituo vya Gerezani na Kimara Mwisho kwa siku hizi mbili ili kusikiliza kero na maoni kutoka kwa wananchi wetu, na tunafurahi kuona huduma hii ikizidi kushika kasi, hasa kwa kuzingatia kuwa tupo katika kipindi cha mpito,” alisema.
Hata hivyo alisema kuwa maoni na ushauri walioupata kutoka kwa wananchi wataufanyia kazi na kurekebisha kasoro mbalimbali zilizojitokeza katika kipindi cha mpito ili kuhakikisha huduma hiyo inakuwa bora zaidi.
Alisema wakala upo mbioni kumpata mtoa huduma ya ukusanyaji mapato ambaye atakuwa na jukumu la kushughulikia suala la kadi ili kuondokana na changamoto mbalimbali za usafiri zinazowakabili watumiaji wa mabasi hayo.
“Natambua kuwa kadi zimeisha na wakala unalishughulikia jambo hili na tutahakikisha kuwa tunaongeza kadi, nawasihi wananchi watambue kuwa tupo katika kipindi cha mpito, mapungufu mengi yaliyojitokeza tutayarekebisha,” alisema Mhandisi Rwakatare.
Alibainisha kuwa suala la kadi limechukua muda mrefu kwa vile mchakato wake unahusisha mfumo wa kibenki na hivyo kuwataka wananchi wa Jiji la Dar es Salaam kuwa na uvumilivu katika kipindi hiki cha mpito kutokana na changamoto mbalimbali zilizojitokeza, hususani suala la kadi ambalo aliahidi kulitafutia ufumbuzi mapema iwezekanavyo.
Alisema kuwa wakala unatarajia kuongeza njia za mwisho katika maeneo ya Mwenge, Kawe na Mabibo.
Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka ulianza rasmi Mei 16, mwaka jana.