25.7 C
Dar es Salaam
Saturday, December 4, 2021

Adhabu barabarani sasa Sh milioni tatu

Na RAMADHAN HASSAN-DODOMA

KWA Muswada wa Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Ardhini wa mwaka 2018, uliopitishwa na Bunge, sasa adhabu za barabarani zitatoza mpaka kufikia Sh milioni tatu.

Hata hivyo kifungu hicho kilionekana kupunga na Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na Kamati ya Bunge ya Miundombinu.

Tozo zinazolalamikiwa ni kiwango cha asilimia 1.5 ya pato ghafi na kifungu cha 42(1) na (2) kinachotoa adhabu kubwa ya faini na kifungo kwa mtu aliyetenda kosa.

Adhabu inayotajwa katika kifungu hicho ni Sh milioni tatu kwa mtu mmoja na Sh milioni tano kwa kampuni au kifungo cha miaka miwili.

Msemaji wa Kambi ya Upinzani wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, James Mbatia, alisema lengo la muswada huo lisiwe kuwatesa au kuwapa adhabu watumiaji wa huduma za usafiri wa ardhini.

Alisema lengo liwe kuweka mazingira rafiki ili kila mdau anufaike na wakati huohuo uchumi wa nchi uimarike.

Mbatia alisema katika muswada huo kuna tozo kubwa na adhabu kwa watu watakaopatikana na makosa mbalimbali.

“Kwa mfano kifungu cha 35(3) ambacho kimeweka kiwango cha tozo ya asilimia 1.5 ya pato ghafi badala ya kutozwa kwenye faida.

“Kifungu cha 42(1) na (2) kinatoa adhabu kubwa ya faini na kifungo kwa mtu aliyetenda kosa, Sh milioni tatu kwa mtu mmoja na Sh milioni tano kwa kampuni au kifungo cha miaka miwili jela au vyote kwa pamoja,” alisema.

Alisema kambi ya upinzani inashauri kwamba adhabu hii ni kubwa na inatoa taswira ya kukomoa badala ya kurekebisha tabia.

Mbatia alisema watu wanahitaji usafiri wa uhakika kwenda maeneo mbalimbali kwa shughuli za kiuchumi na kijamii.

Alisema pamoja na kutambua uwepo wa uchumi wa soko huria na uhuru wa watu kufanya shughuli mbalimbali wanazotaka katika zama hizi za utandawazi, bado Serikali za mataifa mbalimbali duniani zimeweka utaratibu wa udhibiti ili kuondoa uholela katika uendeshaji wa mambo na hivyo kuongeza ufanisi.

Mbatia alisema pamoja na kutambua umuhimu wa udhibiti, lakini muswada huo haupaswi kuwa chanzo cha mateso na adhabu kwa watumiaji wa usafiri wa ardhini.

“Siku za nyuma na hata mpaka sasa, kumekuwa na malalamiko mengi juu ya vitendo vya askari wa usalama barabarani kuwabambika makosa mengi madereva na wamiliki wa vyombo vya usafiri barabarani kwa lengo la kuongeza mapato ya Serikali kupitia faini wanazotozwa.

“Tuhoji hivyo kwa kuwa Serikali inafurahia mapato yanayotokana na makosa ya barabarani bila kujua kwamba kufurahia mapato hayo ni kushabikia makosa yaendelee kufanyika ili kipato kiongezeke na wakati huohuo athari za makosa hayo ni pamoja na maelfu ya Watanzania kupoteza maisha kutokana na ajali za barabarani,” alisema.

Alisema kifungu cha 7(1) cha muswada huo kinaanzisha Bodi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Ardhini ambayo itakuwa na wajumbe saba, hivyo kambi ya upinzani inapendekeza uwiano wa kijinsia uzingatiwe angalau wajumbe watatu wawe ni wanawake.

Mbatia alisema kifungu cha 7(2) kinaelekeza kwamba mtendaji mkuu wa mamlaka atakuwa ndiye katibu wa bodi.

“Suala la kumfanya mtendaji mkuu kuwa katibu wa bodi litadumaza ufanisi kiutendaji. Hii ni kwa sababu kwa mujibu wa kifungu cha 8(1) cha muswada huu, bodi pamoja na mambo mengine ina jukumu la kuisimamia menejimenti katika utekelezaji wa shughuli za mamlaka akiwemo mtendaji mkuu.

“Hivyo kumfanya mtendaji mkuu kuwa sehemu ya usimamizi huo kunaondoa dhana ya ufanisi, kuaminika na uwajibikaji,” alisema.

 Mbatia alisema kambi ya upinzani inapendekeza kwamba mtedaji mkuu asiwe katibu wa bodi, na badala yake muswada huu uasili (adopt) kifungu cha 3(1) cha jedwali la kwanza la Sheria ya Sumatra 2001.

“Kambi ya upinzani inashauri kwamba hatua zote zinazochukuliwa katika kufanya mabadiliko yoyote, lazima zizingatie kukuza utu wa binadamu,” alisema.

MAONI YA KAMATI

Akiwasilisha maoni na ushauri wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu muswada huo, mjumbe wa kamati hiyo, Dk. Rashid Chuachua alisema kamati hiyo inaona asilimia 1.5 inayotozwa katika pato ghafi ni kiwango kikubwa sana.

Chuachua alisema kamati inapendekeza kiwango hicho cha asilimia 1.5 kirekebishwe na kiwe asilimia moja kwenye kifungu cha 35 (3) ambacho kinazungumzia tozo katika sheria hiyo.

 “Katika maoni yetu ya jumla, kamati inaona viwango vya tozo za watoa huduma kubadilisha tozo ni mlolongo mrefu na kwa muda mrefu viwango hivyo havijafanyiwa marekebisho.

“Tunashauri katika kanuni kuwe na kikokotoo kinachotokana na gharama ya uendeshaji ili kutatua changamoto hii,” alisema.

SERIKALI

Akiwasilisha muswada huo kwa upande wa Serikali, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe alisema unakusudia kuanzisha Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Ardhi (LATRA) ambayo itakuwa na jukumu la udhibiti wa sekta ya usafiri wa ardhini nchini.

Alisema mambo muhimu katika muswada huo ni kuanzisha Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Ardhini, kuainisha utaratibu wa uteuzi wa bodi ya wakurugenzi na majukumu yake, kuratibu masuala ya usalama wa ardhini na kuweka utaratibu wa kuanzisha Baraza la Ushauri.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,897FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles