27.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 1, 2023

Contact us: [email protected]

Aangua kilio kizimbani akikiri kumuua mkewe

KULWA MZEE-DAR ES SALAAM

MHANDISI Novath Kaberwa, ameangua kilio kizimbani baada ya kukiri kumuua bila kukusudia mkewe Clara Munisi, alipokuta watoto wake hawajala saa tano usiku na mama yao amerudi muda huo akiwa amelewa.

Munisi aliangua kilio jana katika Mahakama Kuu iliyoketi Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam mbele ya msajili Pamela Mazengo.

Mahakama ilimtia hatiani mshtakiwa na kumuhukumu kifungo cha miaka miwili jela baada ya msajili Mazengo kuzingatia hoja zilizowasilishwa na mawakili wake wakiomba apunguziwe adhabu.

Wakili wa Serikali, Justus Ndibarema, alidai mshtakiwa aliua bila kukusudia mkewe Clara Munisi Januari 13 mwaka 2016 maeneo ya Keko Mwanga.

Alidai Clara aliondoka nyumbani kwenda kununua mafuta ya kupikia, aliongozana na dada yake Veronica Munisi, walirudi nyumbani saa tatu usiku na kumkuta mshtakiwa amerudi nyumbani.

Anadai mshtakiwa alianza kumpiga Clara, dada yake akafanikiwa kukimbia akimwacha akipigwa na majirani wakajitokeza kuamulia.

Inadaiwa mshtakiwa alipoona majirani wamejitokeza alikimbia, majirani walimchukua Clara na kumkimbiza Hospitali ya Temeke ambako hali yake iliendelea kutetereka na ilipofika Januari 14 mwaka 2016 alifariki dunia.

“Uchunguzi ulipofanyika Januari 16, ilibainika kifo cha marehemu kilitokana na kuvia kwa damu,” alidai wakili Ndibarema.

Alidai Julai 15 mwaka 2016 mtuhumiwa alikamatwa maeneo ya Kilosa mkoani Morogoro, alikiri maelezo hayo yote na mahakama ilimtia hatiani.

Mawakili wa mshtakiwa, Hashimu Mziray, Venance Victor na Neema Kahakabuka kwa nyakati tofauti waliiomba mahakama impunguzie adhabu mteja wao kwa sababu amekaa gerezani zaidi ya miaka mitatu.

Walidai mshtakiwa anajutia kosa alilofanya, amekuwa mtu mwema kwani hakuna kosa alilowahi kufanya akiwa gerezani.

Victor alidai mshtakiwa ni mhandisi wa barabara, alisomeshwa na Serikali na alipewa mradi wa marekebisho ya barabara ya Morogoro maeneo ya Mikumi na Kilosa, mradi huo hadi sasa umeshindwa kutekelezwa kwa wakati.

“Mazingira ya tukio lenyewe, mshtakiwa alirudi nyumbani saa tano usiku anakuta watoto wake wamelala njaa na mkewe hajulikani alipo ukizingatia mke wa mtu.

“Mkewe anarudi kalewa pamoja na mdogo wake, mazingira hayo mtu yoyote anaweza kufanya tukio lolote,” alidai Victor.

Wakili Neema akiomba apunguziwe adhabu mshtakiwa huyo, alidai ni baba anayetegemewa na watoto wawili Robert Novath (19) na Caren Novath (11) ambao wanakosa malezi ya wazazi, wanaishi kwa ndugu, haijulikani kama wanatendewa haki au la.

“Tunaomba mteja wetu apunguziwe adhabu au aachiwe kwa masharti na endapo hatatimiza arudishwe kutumikia adhabu,” alidai. Msajili Mazengo alisema mahakama imezingatia hoja zilizowasilishwa, ni kweli mshtakiwa hastahili kupata adhabu kubwa, hivyo mahakama ilimuhukumu kwenda jela miaka miwili na kama haridhiki anaweza kukata rufaa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,404FollowersFollow
564,000SubscribersSubscribe

Latest Articles