CAIRO, MISRI
NAHODHA wa timu ya taifa ya Zimbabwe, Knowledge Musona, ameweka wazi kuwa, watahakikisha wanapambana kuizuia Misri na sio kuangaika na mchezaji wao mmoja Mohamed Salah kwenye mchezo wa kwanza wa ufunguzi wa Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), Juni 21.
Wamedai hawana mpango wa kumfikiria mchezaji huyo, ila watahakikisha kila mchezaji anatakiwa kuchungwa kwa ajili ya kuwazuia wasilete madhara.
“Lengo letu kubwa kwenye mchezo huo ni kuhakikisha tunamzuia kila mchezaji na sio kumuangalia mchezaji mmoja, lakini wote tunajua ubora wa Salah, sio mchezaji wa kumuacha kwa kuwa uwezo wake ni mkubwa.
“Lakini kitu ambacho tunakiogopa ni kupambana kumzuia Salah kumbe kuna wachezaji wengine ambao wanaweza kuleta madhara, hivyo ni lazima tuwe makini kwa ajili ya kila mchezaji.
“Tunatakiwa kuwa bora kila idara na kutumia nafasi ambazo tutazitengeneza, tunakwenda kwa ajili ya kushindana na sio kuongea, hivyo tunaamini mchezo huo wa ufunguzi utakuwa na ushindani wa hali ya juu.
“Hatupo tayari kuwaangusha mashabiki kwa kuwa wanatusapoti kila wakati bila ya kujali matokeo, hivyo lazima tupambane kwa ajili yao na kwa ajili ya taifa,” alisema Musona.