ADDIS ABABA, ETHIOPIA
WAZIRI Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed, amesema kuwa muhula wa siku tatu uliokuwa umetolewa kwa ajili ya waasi wa eneo la Tigray kuweka chini silaha umemalizika na kuonya kuwa sasa jeshi la Taifa hilo litaendelea na operesheni yake ya kuukomboa mji mkuu wa eneo hilo Mekelle, kutoka mikononi mwa waasi.
Kupitia ujumbe aliouandika jana Jumanne katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Facebook, Abiy alisema kuwa kwa kutilia maanani kwamba muhula uliokuwa umetolewa na Serikali Kuu umemalizika, sasa jeshi la Taifa litaanza kutekeleza operesheni ya kijeshi katika siku chache zijazo kwa ajili ya kuwafagia kabisa waasi na kuuchukua tena mji wa Mekelle.
Novemba 4, Waziri Mkuu Ahmed alitoa amri ya kushambuliwa eneo la Tigray baada ya wanachama wa Tigray People’s Liberation Front (TPLF) kushambulia kituo cha jeshi katika jimbo hilo.
Mapigano hayo yamepelekea mamia ya watu kupoteza maisha na zaidi ya Waethiopia wengine 25,000 kukimbilia katika nchi jirani ya Sudan. Mapigano hayo pia yanatishia kulitumbukiza eneo zima la Pembe ya Afrika katika mgogoro mpya.
Kwa kutilia maanani taathira hasi za mapigano hayo, Umoja wa Mataifa (UN) na Umoja wa Afrika (AU) zimemuomba Ahmed aanzishe mazungumzo na waasi wa Tigray ili kufikia suluhu na kuepusha maafa na hasara zaidi nchini humo.
OBASANJO KUWA MPATANISHI
Rais wa zamani wa Nigeria, Olusegun Obasanjo siku chache zijazo anatazamiwa kuelekea Ethiopia kwa ajili ya kupatanisha mzozo huo baina ya serikali ya Ethiopia na TPLF.
Msemaji wa Rais huyo wa zamani wa Nigeria, Kenny Akinyemi alieleza kuwa, Obasanjo hivi karibuni ataongoza ujumbe wa upatanishi katika mzozo huko Ethiopia.
Serikali ya Ethiopia na Umoja wa Afrika hata hivyo zimetangaza kuwa hazina taarifa yoyote kuhusu safari ya Obasanjo nchini Ethiopia.
Tigray ni eneo la jamii ya wachache lakini wenye nguvu ambao kwa miongo kadhaa wamekuwa wakiongoza muungano tawala nchini Ethiopia.
Muungano mpya wa utawala ulioundwa miaka miwili iliyopita baada ya kuingia madarakani Waziri Mkuu wa Ethiopia, Ahmed umesusiwa na jamii ya watu wa Tigray.
Mapigano hayo yanayoendelea sasa huko Kaskazini mwa Ethiopia kati ya vikosi vya serikali na wapinaganaji wa harakati ya TPLF yameutia wasiwasi mkubwa Umoja wa Mataifa.
AP