NA UPENDO MOSHA-MOSHA
UONGOZI wa Mkoani Kilimanjaro umelaani vitendo vyote vya uvunjifu wa amani vinavyofanywa na baadhi ya watu ikiwemo watu,kujeruhiwa,kuumizwa,kutekwa na kupotezwa na kisha kutupwa katika madaraja na mito.
Pia kutokana na matukio hayo,watu zaidi ya watano wanashikiliwa na jeshi la polisi mkoa wa Kilimanjaro kwa ajili ya uchunguzi wa tuhuma hizo.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Moshi jana ,Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mgwhira alisema matukio hayo yanatisha na hayapaswi kuvumiliwa.
Mgwhira ambaye pia Ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wa mkoa huo,alisema matukio ya uvunjifu wa amani ikiwemo watu kupigwa,kutekwa,kuuwawa na kutupwa yamejitokeza ya Hai,Moshi na Rombo jambo ambalo halivumiliki.
“Kipindi hiki kumejitokeza baadhi ya matukio ya uvunjifu wa amani katika majimbo matatu ya uchaguzi yalio katika wilaya hizi,kumekuwa na matukio ya watu kupigwa,kujeruhiwa,kutekwa na watu kupotezwa na kutupwa maeneo ya mito na madaraja”alisema
Alisema pia kumekuwa na matukio ya wapiga kura kunyweshwa pombe kupita kiasi kwa malengo mbalimbali, jambo ambalo serikali haita weza kumvumilia na kwamba suala la uchaguzi ni amani na sio vurugu.
Katika hatua nyingine,alikemea baadhi ya tabia ya wanasiasa kuingilia mikutano ya ndani ya vyama vingine, suala ambalo kumekuwa likisababisha hatari ya mapigano baina ya pande hizo mbili.
“Kutokana na matukio haya yasioendana na kanuni na sheria ya uchaguzi watu kadhaa wamekamatwa, wanalisaidia jeshi la polisi katika uchunguzi sambamba na kufungua majalada lakini pia wengine wataendelea kushiriliwa,”alisema
Alisema uchunguzi ukikamalika katua mbalimbali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya watu wote watakaokuwa wamehusika.
Mbali na hilo, alitoa agizo kwa wakuu wa wilaya zote za mkoa huo zenye vihashiria vya uvunjifu wa amani kuhakikisha wanathibiti hali hiyo.
“Nawataka wakuu wa wilaya kudhibiti vitendo hivi, ikiwa ni pomoja na kuhakikisha mikutano ya wagombea wote was ngazi mbalimbali na vyama vyote wanapewa ulinzi wa kutosha ….nasisitiza vurugu za aina hii sio asili ya chaguzi za Tanzania na si asili ya watuku wa Kilimanjaro.
“Kuna chuki inapandikizwa ili kuona mkoa unakuwa na taharuki muda wote, nasema hapana nakataa jambo hili, nawaomba viongozi wote wa vyama kutoa ushirikiano wa kutosha kudumisha amani,”alisema
Alisema ofisi ya mkuu wa mkoa kwa kushirikiana na taasisi za dini wameandaa kongamano la siku moja ambalo litahusisha viongozi wa vyama mbalimbali vya siasa ikiwemo wagombea wa udiwani na ubunge,wakuu wa wilaya,wakurugenzi pamoja na timu zote za kampeni kwa lengo la kutoa elimu.
“Kutokana na matukio yanayoendelea tumeona ipo haja ya kuwaleta wadau hawa pamoja Septemba 28, mwaka huu ili tuwape elimu ya pamoja ambayo itawasaidia,”alisema