MAPUTO, MSUMBIJI
MAMLAKA ya bandari nchini Msumbiji imekanusha madai kwamba meli yake ilikuwa imebeba mzigo uliosababisha mlipuko wa Beirut, nchini Lebanon.
Kwa mujibu wa AFP,Meli hiyo ambayo ilikuwa inatokea bandari ya Beira, nchini Msumbiji inadaiwa kuwa ilishusha mzigo Beirut na shehena ya mzigo ambao ulihifadhiwa katika ghala ya bandari.
“Mamlaka ya bandari haikuwa inajua kuwa meli ya MV Rhosus iliacha mzigo katika bandari ya Beira,” imeeleza mamlaka ya bandari ya Beira.
Inasema hakukuwa na tangazo la kuwasili kwa meli bandarini hapo ndani ya siku saba hadi 15.
Lakini maofisa wa bandari ambao hawakutaka majina yao yatajwe, wameimbia AFP kuwa ingawa meli hiyo ilikuwa imewasili katika bandari ya Beira, lakini safari yake ilikuwa haipaswi kuishia Msumbiji bali Zimbabwe au Zambia, kwa sababu ilikuwa imebeba kemikali inayotumika kutengeneza mlipuko kwa ajili ya sekta ya migodi.
Mamlaka ya bandari inayofuatilia mienendo ya Meli,imesema kuwa vyombo vya majini vinavyopepeza bendera ya Moldoval viliwasili Beirut tangu Nov,20, 2013 na havijawahi kuondoka.
Wakati huo huo, maofisa wa uokoaji bado wanaendelea kuitafuta miili ya watu waliofukiwa kwenye kifusi katika bandari ya Beirut baada ya kutokea mlipuko mkubwa siku tatu zilizopita.
Kulingana na mamlaka ya Lebanon miili mingine mitatu imepatikana katika muda wa saa 24 zilizopita.
Maofisa wa uokoaji kutoka Ufaransa na Urusi wakisaidiwa na mbwa maalumu wanaendelea na zoezi la kuitafuta miili ya watu pamoja na uchunguzi katika eno la bandari mjini Beirut baada ya Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron kulitembelea eneo palipotokea milipuko hiyo na kuahidi misaada.
Macron pia amesema ataendelea kuwasisitizia viongozi wa kisiasa wa Lebanon juu ya mageuzi.
Pamoja na maofisa hao wa uokoaji wadau wa kujitolea wengi pia wamejitokeza kutoka pembe zote za mji mkuu wa Lebanon, Beirut kusaidia katika juhudi kubwa za usafishaji baada ya kutokea mlipuko siku ya Jumanne.
Milipuko mikubwa miwili ilitikisa bandari ya Beirut na kusababisha vifo vya watu 149 na zaidi ya watu 5,000, wamejeruhiwa.
Wakati huo huo, Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa chakula duniani WFP linapanga kupeleka nchini Lebanon unga wa ngano kwenye viwanda vya uokaji na nafaka kwenye kampuni za kusaga unga ili kuepuka uhaba wa chakula.
Msemaji wa shirika la WFP ameeleza kwenye mkutano wa Umoja wa Mataifa mjini Geneva amesema WFP ina wasiwasi kwamba uharibifu katika bandari uliosababishwa na mlipuko utazidisha hali mbaya ya usalama wa chakula katika nchi hiyo inayokabiliwa hali mbaya ya kifedha na hasa katika wakati huu wa janga la COVID-19.
Msemaji huyo ameeleza kuwa WFP itatoa vifurushi vya chakula kwa maelfu ya familia na pia iko tayari kutoa usimamizi wa ugavi na msaada wa vifaa na utaalam kwa Lebanon.